Simba SC ipo mbioni kuinasa saini ya kiungo Polisi Tanzania
Muktasari:
Majogoro alipoulizwa kuhusu kupata dili hilo alisema kuna kiongozi wa Simba (jina kapuni) aliwahi kumpigia simu na kumwambia wanamfuatilia na anatakiwa kuzidi kujituma.
KIUNGO fundi wa mpira anayekipiga Polisi Tanzania, Baraka Majogoro yupo mbioni kujiunga na Simba kuungana na kocha wake Seleman Matola anayehusishwa kwenda kuwa kocha msaidizi Msimbazi.
Taarifa zilizonaswa na Mwanaspoti, Matola atakapoondoka Polisi anatarajiwa kuambatana na Majogoro.
Hata hivyo, ili kumnasa kiungo huyo ni lazima itumike nguvu kubwa ya kuvunjwa kwa mkataba wa mchezaji huyo, kwani bado amebakiza miezi nane ya kuitumikia.
Inaelezwa kwa upande wa Simba hautaki kufanya mambo yao kwa presha na jambo lililopo kwa sasa ni kutaka kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ifikapo dirisha dogo (Desemba 15).
Makamu Mwenyekiti wa Polisi, Robert Munisi alipoulizwa juu ya taarifa hizo alisema kwa namna wachezaji wao wanavyojituma haishangazi kuona wakihitajika na klabu mbalimbali.
Munisi alisema kwa taarifa ya Majogoro kuhitajika Simba kwake ni ngeni, ila hilo haliwezi kuwazuia Simba kumsajili mchezaji huyo kama tu wakifuata taratibu zilizopo kwenye mkataba.
“Kwenye mkataba kuna vipengele vya kuingia na pia kuvunja mkataba, kwa hiyo kama Simba wanamtaka Majogoro na wanatakiwa wakaisome hiyo mikataba ndio wajue wanaivunjaje,” alisema.
Majogoro alipoulizwa kuhusu kupata dili hilo alisema kuna kiongozi wa Simba (jina kapuni) aliwahi kumpigia simu na kumwambia wanamfuatilia na anatakiwa kuzidi kujituma.
“Siwezi kusema lolote kwani bado nina mkataba na Polisi, ngoja tuone itakavyokuwa ikifanikiwa sawa, lakini ni uongozi ndio utakaoamua,” alisema nyota huyoa aliyepo pia timu ya taifa.