Kapera jembe la Kagera linaloitesa Simba
Muktasari:
Hata hivyo, Wekundu si kuwa wamelala badala yake wanaendelea kufukuza mwizi kimyakimya ili kuona kikosi chao kinakuwa na makali zaidi msimu ujao.
MWANZA.BAADA ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 kumalizika kwa Simba kutetea taji lao, sasa akili zote zinafikiria jinsi ya kurudi kwa nguvu mpya ili kuendelea kujaza mataji kwenye makabati msimu ujao.
Ikumbukwe kuwa Wekundu wa Msimbazi bado hawajapoa kutokana na kusaka rekodi ya watani zao, Yanga kufikisha ubingwa mara tatu mfululizo. Wanateseka.
Licha ya kuwa Yanga imelikosa tena taji la Ligi Kuu Bara, lakini wanaendelea kuwatesa Simba kwa rekodi waliyoiweka kwa kutwaa ubingwa misimu mitatu mfululizo.
Hadi sasa Yanga tayari wameshasainisha nyota kadhaa ikiwa ni Issa Bigirimana, Patrick Sibomana, Abdul Azizi Makame, Lamine Moro na Kalengo Maybin, huku taarifa zingine zikidai kumnasa beki Mustapha Suleiman, raia wa Burundi kutua pale Jangwani.
Hata hivyo, Wekundu si kuwa wamelala badala yake wanaendelea kufukuza mwizi kimyakimya ili kuona kikosi chao kinakuwa na makali zaidi msimu ujao.
Miongoni mwa wachezaji ambao Simba inawahitaji ni straika wa Kagera Sugar, Ramadhan Kapera ambaye ameendelea kuwaumiza akili za mabosi wa mabingwa hao kusaka saini yake.
Wakati Simba ikitajwa zaidi kumuwinda kinda huyo, imebainika kuwa si wao tu bali kuna timu zingine zinamsaka kwa nguvu kuhakikisha msimu ujao anahamishwa kwenye mashamba ya miwa huko Bukoba.
Mwanaspoti imepiga stori na straika huyo ambapo anaeleza msimamo wake na matarajio katika msimu ujao, uzi gani atavaa na jinsi alivyojipanga kimataifa.
Kuhusu Simba
Anasema wazi kuwa moja ya timu zinazommezea mate kila wakati ni Simba, lakini inapokuja ishu ya maslahi ndio wanatofautiana na kuwa bado anawasikilizia.
Anasema hadi sasa kila kitu kinakwenda vizuri ikiwamo mazungumzo ya mwisho kujua wanamshawishi vipi, huku akieleza kuwa yupo tayari kuvaa uzi mwekundu.
“Ni kweli Simba wananitaka na mazungumzo yanaendelea vizuri hivyo, lolote linawezekana katika soka kwani, ndio kazi yangu,” anasema Kapera.
Kinda huyo anaongeza kuwa Simba imemtengea kitita cha Sh 15 milioni, huku mwenyewe akihitaji Sh30 milioni ili aweze kuhamisha makazi na kwamba, hata timu zingine zimemtangazia dau nono.
Anabainisha kuwa miongoni mwa timu zinazomnyatia kila hatua ni KMC ya Dar es Salaam ambayo yenyewe imeweka mzigo wa Sh 25 milioni huku Azam FC pia wakimtangazia dau kubwa.
“Kwa hiyo nitaangalia licha ya kuwa Simba kuna faida kubwa ikiwamo kucheza michuano ya kimataifa, lakini kimaslahi wapo chini sana bora niende kwingine au nibaki Kagera,” anasema.
Msimamo
Nyota huyo aliyefunga mabao tisa kwenye Ligi Kuu msimu huu, anasema msimamo wake ni kupiga chini ofa ya Sh 15 milioni za Simba ili kuitumikia miaka miwili.
Anasema kama wapo siriasi kweli waandae Sh30 milioni iliaweze kumwaga wino kiroho safi na msimu ujao aweze kuvaa jezi nyekundu na kufanya kazi yake.
“Hapana hicho kiasi kwa miaka miwili ni kidogo, siwezi kabisa kusaini kwa miaka miwili lazima waongeze fungu ili niende kufanya kazi,” anasema Kapera.
Ajipanga kimataifa
Kapera anasema kutokana na mazungumzo baina yake na Wekundu kuwa safi, kwa sasa anajiandaa kimataifa kwani dili litakapotiki anaamini atacheza mechi za Klabu bingwa Afrika.
Anaamini atakapojiunga na Simba lazima aonyeshe kitu tofauti ili kulishawishi benchi la ufundi na kumpanga kila mchezo.
Anafafanua kuwa hana shaka na kiwango chake kwani kazi anayoifanya uwanjani si ya kitoto, hivyo mashabiki watarajie makubwa kama atatua.
“Nikipata nafasi lazima nionyeshe uwezo kwa sababu najua ushindani utakuwa mkubwa pale Simba kwani, ni klabu kubwa inayojiandaa na kimataifa.
“Lazima nionyeshe kitu cha pekee ili kocha atambue mchango wangu, kumbuka soka ni mchezo wa nafasi.”
Malengo yake
Kapera anasema pamoja na mafanikio yake, lakini kwa sasa hapati usingizi kutokana na timu yake kuwa katika wakati mgumu wa kukwepa kushuka Daraja.
Anasema Kagera Sugar imekuwa na matokeo yasiyoridhisha licha ya wachezaji kupambana, lakini mambo yamewia magumu hadi kusubiri mechi za play off.
Mkakati wao ilikuwa ni kumaliza ligi katika nafasi nne za juu, lakini kilichotokea hawana jinsi zaidi ya kukabiliana nacho na kueleza kuwa, lazima wapambane kuinusuru timu kutoshuka daraja. Tayari Kagera Sugar imeanza kucheza mechi za Playoff ikianza na Pamba ikilazimisha sare pale CCM Kirumba, Mwanza na mechi ya mwisho itapigwa Kaitaba, Bukoba.
“Mpira una matokeo ya ajabu, kikosi chetu kiko vizuri lakini matokeo umeona, lakini kimsingi tutatumia nafasi hii ya kuhakikisha tunapata ushindi na kubaki kwenye ligi,” anasema.
UONGOZI SAFI
Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamis Madaki anasema hawategemei biashara ya mpira na hivyo mchezaji anayepata nafasi timu nyingine ni ruksa kuondoka.
Anasema Kagera Sugar haijawapa mikataba mirefu ya kuwabana wachezaji, wakiamini soka ndio maisha yao hivyo anayetaka kuondoka wanamtakia kila la heri.
“Hatusajili wachezaji kwa mikataba mirefu, hatutegemei biashara ya mpira, inapotokea nafasi kwa yeyote hatuna shida tunamtakia kheri,” anasema Madaki.
Kuhusu matokeo ya Klabu kwa ujumla, Katibu huyo anasema hawawezi kumlaumu yeyote kwani mpira wanaujua kuwa na matokeo ya maajabu huku akiweka wazi sababu za Kagera Sugar kucheza Ligi ya mchujo.
Madaki anasema timu haikuwa na maandalizi mazuri na kwamba hata usajili hawawezi kuujadili zaidi kwani mpira unachezwa wazi na kiwango kinaonekana.
Anaeleza kuwa kwa sasa ni kila mmoja kushiriki kwa nafasi yake kuhakikisha kwenye mechi za play off wanapambana kupata ushindi ili timu isishuke daraja.
“Ukikosea maandalizi,usajili usitegemee matokeo mzuri,lakini yote kwa yote tunajipanga na play off kuhakikisha tunashinda na timu inabaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao,” anasema Madaki.