Jamani Yanga hivi mmemskia Mzee Akilimali
KATIBU wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali buana haishiwi vituko, kwani unaambiwa baada ya kuona mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo ukienda freshi, amekula kiapo kwa Wanayanga wenzake.
Mzee Akilimalio amefichua kuwa, anaweza kuchinja mbuzi kama sehemu ya kusheherekea upatikanaji wa viongozi wapya wa klabu hiyo, siku safu mpya ya Jangwani ikitangazwa.
Akilimali alisema tatizo pekee linaloisumbua Yanga ni uongozi na kama watapatikana wapya ina maana watakuwa wametatua tatizo hilo ambalo matokeo yake ni ukata wa kifedha.
“Tunahitaji viongozi ambao wanajua thamani ya nembo yetu ya Yanga. Nachukizwa na mambo ya kupitisha bakuli ni aibu kwetu na hiyo yote inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo viongozi.
“Uwepo wa viongozi ungeweza kutukwamua kwenye aibu ya kuchangishana. Sisemi kuwa ni vibaya wanachama kuichangia klabu, lakini kwa ukubwa wa Yanga si vema kutegemea fedha kutoka kwa wachama wake pekee.
“Nitawafurahia na kuwaunga mkono viongozi ambao kwa pamoja wanayanga tutawapa ridhaa ya kutuongoza. Kwa namna mchakato wa uchaguzi unavyoenda nadhani tutapata viongozi bora,” alisema Akilimali.
Mzee huyo aliongeza kwa kuwataka mashabiki na wanachama wa Yanga kuunga mkono kwa asilimia zote uchaguzi wao ambao unatarajiwa kufanyika Mei 5, mwaka huu.