Hili nalo ni ajabu lingine la Ligi Kuu
Muktasari:
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Salum Chama alisema katika kituo chake cha Kanda ya Ziwa pale Bukoba ana mipira miwili tu ambayo inatumika katika mechi za Ligi Kuu Bara na kabla ya mchezo wowote kuchezwa hapo katika kikao cha maandalizi ya mechi asubuhi huwa anawaambia viongozi wa timu husika kufika na mipira yao.
TULIA buana. Si mnakumbuka tuliowahi kuandika maajabu kadhaa ya Ligi Kuu Bara? Sasa unaambiwa yale maajabu katika soka la Bongo, wala hajayaisha kwani tukio lililoibuka juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwenye katika mechi kati ya Simba dhidi ya Coastal Union, limefichua madudu zaidi yaliyo katika ligi hiyo.
Ni hivi. Watetezi wa Ligi hiyo, Simba jioni ya leo Ijumaa watakuwa Uwanja wa Uhuru ili kuikaribisha dhidi ya Kagera Sugar wakiwa na kiu ya kulipa kisasi cha 2-1 walichopewa mjini Bukoba, wakitoka kupata ushindi wa kishindo wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union.
Katika pambano lao la juzi dhidi ya Wagosi, nyota wake wawili, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi walifunga hat trick na kukabidhiwa mipira, lakini usichojua ni kwamba mipira ile haikutumika kwenye mchezo huo kabisa, bali walichomolewa stoo.
Inawezekana hujaelewa. Kwa kawaida anayefunga hat trick anapewa tuzo ya mipira iliyotumika kwenye mchezo husika, lakini mipira waliyopewa Okwi na Kagere kama tuzo ya kila mmoja ya kufunga hat trick, ilichomolewa sehemu kwa vile iliyotumika ilikuwa ni ya Simba na wala sio ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala Bodi ya Ligi (TPLB).
SIRI NZITO
Inaelezwa kuwa, kwa msimu huu wote, Simba imekuwa ikitumia mipira yao katika kila mchezo wanaocheza katika Ligi hiyo, huku wasimamizi wa ligi wakikosa kabisa mipira ya kuitumia uwanjani kitu ambacho ni maajabu mengine ya soka la Tanzania.
Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu alifichua kuwa, msimu huu katika mechi zao zote wamekuwa wakitoa mipira yao katika kila mchezo ambao watacheza kwani ile iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waliyogaiwa kila timu ili kutumia katika mechi si mizuri.
Rweyemamu alisema mipira ambayo tulipewa na TFF, ni kama ile ambayo walipewa zawadi Kagere na Okwi walipofunga mabao matatu kwenye mechi ya Coastal Union lakini si bora katika kuchezea kwani imekuwa inapea kwa upepo, ila ujumla si mizuri katika kuchezea mechi kwani hata katika mazoezi huwa hatuitumii mara kwa mara.
"Ukiondoka mechi kubwa ambazo tumecheza, michezo mingine yote ya mikoani na hapa Dar es Salaam, tumekuwa tukitoa mipira yetu 10 ili kuitumia katika kila mchezo husika kwani yetu ipo katika hali nzuri ya kuchezea na mara baada ya kumaliza tunaichukua."
"Katika mechi ya Coastal baada ya kumalizika tulichukua mipira yetu kumi kama kawaida Kagere na Okwi walipewa zawadi ile mipira ya kawaida ambayo haikutumika ambayo si ya kwetu," alisema Rweyemamu.
SIKIA HII SASA
Mtoa taarifa aliidokeza Mwanaspoti kuwa mbali ya Simba kutumia mipira yao katika mechi zao zote, lakini katika mechi za mikoani kama walivyocheza dhidi ya Biashara United walipoteza mmoja na kurudi tisa na kwenye mchezo wa Kagera Sugar ambao walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1, kuna ambayo ilifichwa ili kutumika ile ambayo si bora katika kuchezea.
Mwenyekiti wa Bodi ya ligi Steven Mnguto, alikiri kuwepo kwa uhaba wa mipira.
"Ni kweli msimu huu wamekuwa tatizo na uhaba wa mipira kwenye mechi zote za Ligi Kuu Bara na si Simba ambao wanatumia mipira yao, bali hata timu nyingine wanapokuwa wanacheza mechi zao huwa wanatumia mipira yao."
Mnguto alisema Simba wameonekana kutumia mipira yao ni kutokana wamekuwa wakifuatiliwa katika mechi zao, ila si pekee wanaotumia bali ni timu zote huwa zinafanya hivyo, kwani Ligi haina mdhamini.
Alisema mipira ya kutoa zawadi kama mchezaji akifunga mabao matatu katika mchezo mmoja (hat trick), ipo lakini ile ya kuchezea katika hali ya ushindani ndio tatizo kwetu msimu huu baada ya kukosa mdhamini, ila msimu ujao litaisha hili na halitakuwepo tena.
"Juhudi kubwa za kumtafuta mdhamini kwa upande wetu zinafanyika lakini miongoni mwa makubaliano ambayo tataingia nae ni kutupatia mipira iliyokuwa bora na tutaigawa katika kila kituo ili kuweza kutumika katika mechi za ligi na kuondoa kabisa uhaba ambao tumekutana nao msimu huu," alisema Mnguto.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Salum Chama alisema katika kituo chake cha Kanda ya Ziwa pale Bukoba ana mipira miwili tu ambayo inatumika katika mechi za Ligi Kuu Bara na kabla ya mchezo wowote kuchezwa hapo katika kikao cha maandalizi ya mechi asubuhi huwa anawaambia viongozi wa timu husika kufika na mipira yao.
"Siku ya mechi huwa nakwenda katika kikao na mipira yangu miwili na baada ya hapo nawaambia viongozi wa timu waje na mipira yao mitatu ili kuweza kusaidia na kutumika katika mchezo ambao utachezwa jioni," alisema na kuongeza;
"Kama ikitokea kuna mchezaji amefunga hat trick kwa pale huwa tunaonesha kama tumemkabidhi na kumpiga picha, lakini baada ya hapo lazima wauache mpira kwani akiondoka nao kituo kitabaki bila mpira na ile kupata mpire yeye kama zawaidi akienda kucheza mechi Dar es Salaam anatakiwa kwenda ofisi za TFF, atapewa mpira au asubiri niende mjini nikamchukulie na kuangalia jinsi gani nitampatia zawadi yake ya mpira."