Fei Toto: Mfumo ndio ulimfanya Chama ang'are
Muktasari:
Kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema, timu yao ilionekana kuzidiwa na Simba katika mchezo wao wa Jumapili ya Septemba 30, ni kwa sababu ya maagizo waliyopewa na mwalimu wao.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema, sababu kubwa iliyofanya Simba wang’are sehemu ya katikati inayochezwa na Mzambia Cletus Chama, Mghana James Kotei na Jonas Mkude katika mchezo wao ni maagizo waliyopewa na kocha wao, Mwinyi Zahera.
Safu ya kiungo ya Simba iliyoundwa na wachezaji hao, iliwapoteza kabisa wale wa Yanga kama Mkongo Papy Tshishimbi na Fei Toto katika eneo hilo la katikati.
Fei Toto amesema, hawakuhofia viungo wa Simba, lakini walicheza kwa maelekezo waliyopewa na mwalimu wao.
"Mwalimu alihitaji sisi tukabe kuliko kushambulia, mfumo wake ndio ulitaka hivyo lakini kama angetuambia tucheze tungefanya hivyo na kuacha kujilinda," alisema Fei Toto.
Aliongeza kwa kusema, licha ya kukaba, walikutana na changamoto kubwa kutoka kwa viungo wa Simba ndaninya dakika 90 katika mchezo huo.
"Wenzetu walikuwa wengi kwenye kiungo kwa hiyo mchezo ikafanya mchezo kuwa mgumu kwetu na kuzuia muda wote lakini juhudi zetu tulizionyesha katika kipindi chote," alisema kiungo huo maarufu Yanga.