Djuma: Kufukuzwa Simba siyo kifo

Muktasari:

Kocha Msaidizi wa Simba Masudi Djuma amesema hana hofu ya kufukuzwa katika klabu hiyo kwa kuwa ana uwezo wa kufanya kazi kokote.

Mkataba wa Djuma raia wa Burundi, umeingi dosari baada ya kushindwa kuelewana na Kocha Mkuu Patrick Aussems. Djuma alijiunga na Simba Oktoba 2017 akiwa msaidizi wa Joseph Omog.

 

Dar es Salaam.Siku moja baada ya kuthibitika rasmi ameonyeshwa mlango wa kutokea, kocha msaidizi wa Simba, Masudi Djuma amesema kufukuzwa na klabu hiyo sio kifo kwa kuwa kuna maisha baada ya hapo.

Djuma (41) ambaye kabla ya kugeukia ukocha alikuwa mshambuliaji nyota wa timu ya Taifa ya Burundi, ameondolewa Simba baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu Patrick Aussems.

Tangu alipojiunga na Simba Oktoba, 2017, Djuma aliyewahi kuzifundisha na kuipa ubingwa wa Rwanda, Rayon Sports, amekuwa kocha msaidizi chini ya makocha watatu tofauti ambao wawili kati yao waliondoka na kumuacha katika nafasi ya ukocha msaidizi ingawa awamu hii chini ya Aussems yeye ndio ameonyeshwa mlango wa kutokea.

Djuma alipojiunga na Simba kwa mara ya kwanza, timu hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Joseph Omog  kama mkuu wa benchi la ufundi, ingawa miezi miwili baada ya wawili hao kufanya kazi pamoja, kocha huyo raia wa Cameroon aliondolewa baada ya Simba kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA.

Baada ya Omog kutimuliwa, Djuma alisimamia timu kwa muda katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na baadhi ya mechi za ligi kabla ya kurudishwa kwenye nafasi ya kuwa msaidizi wa kocha mkuu pale alipoletwa Mfaransa Pierre Lechantre.

Uhusiano wa Djuma na Lechantre inadaiwa haukuwa mzuri jambo lililochangia mgawanyiko kwa baadhi ya viongozi ndani ya klabu hiyo ambao ulisababisha Simba isimuongeze mkataba na kumuachia timu kwa muda tena Mrundi huyo.

Nuksi ya Djuma kwa makocha wakuu wa Simba imeendelea kuonekana chini ya Aussems ambaye tangu alipoanza kuinoa klabu hiyo, amekuwa hana maelewano na uhusiano mzuri na msaidizi wake.

Mzozo baina ya wawili hao umekwenda mbali zaidi kwa kuwa katika mechi tatu ambazo Simba ilicheza ugenini msimu huu dhidi ya Ndanda, Mbao na Mwadui, Aussems alitoa agizo la kumzuia Djuma asiwe sehemu ya msafara wao abaki jijini.

Kutokana na sintofahamu iliyoibuka baina ya benchi la ufundi, uongozi wa Simba mwishoni mwa wiki iliyopita uliibuka na kufichua kinachoendelea nyuma ya pazia la sakata hilo huku ukifichua uwezekano wa Djuma kuvunjiwa mkataba.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, juzi alikaririwa akifichua kuwa maelewano duni baina ya Djuma na makocha wake wakuu wote waliopita yalikuwa hafifu.

"Tumejaribu kuliweka sawa jambo hili lakini tunaona kadri muda unavyokwenda hali inakuwa ngumu, sisi viongozi hatuna tatizo naye lakini hana maelewano mazuri na kocha mkuu, siwezi kusema Masudi anabaki au anaondoka kwa sababu ni mapema, lakini lolote linaweza kutokea," alikaririwa Try Again na gazeti hili jana.

Hata hivyo, Djuma alipozungumza na gazeti hili japo hakutaka kuweka bayana sababu ya yeye kuhusishwa kufukuzwa Simba na chanzo cha madai ya kutoelewa na kocha mkuu, alisisitiza kuna maisha mengine nje ya mpira na kutoka sehemu moja kwenda nyingine sio kifo kwamba mtu akiondoka hatarudi.

"Kufukuzwa ni sehemu ya maisha kwa kocha yeyote duniani, hivyo hata mimi kama nitafukuzwa Simba haitakuwa jambo la ajabu au kusikitisha kwani hicho siyo kifo kwamba ndiyo nimemaliza historia yangu duniani," alisema kocha huyo bila kuweka wazi kama tayari amemalizana na Simba.

Alipoulizwa kuhusu sababu iliyochangia kibarua chake kuota nyasi licha ya kuwa miongoni mwa makocha vijana wanaokubalika sio tu kwa mashabiki, bali pia kwa makocha wengine nchini, Djuma aliguna na kusema sio wakati mwafaka kuzungumza hilo.

"Tuachane na hizo habari, kama umesikia nimefukuzwa Simba basi wacha iwe hivyo, narudia tena mimi kuondoka Simba sio kifo, maisha yataendelea," alisema kwa kujiamini.

Kocha huyo ambaye pia amekuwa akihusishwa kujiunga na baadhi ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwamo Yanga na African Lyon, alisema ni mapema kuzungumzia mustakabali wake.

Djuma aliyewahi kuwa kocha bora wa Ligi ya Rwanda mwaka 2016, aliajiriwa Simba Oktoba mwaka jana kama kocha msaidizi akichukua nafasi ya Mganda, Jackson Mayanja aliyejiuzulu.

Wasikie Kibadeni, Mgunda

Taarifa za kutimuliwa Djuma zimewaibua baadhi ya makocha nchini ambao wamemtaja ni kocha aliyeijenga Simba alipokaimu nafasi ya kocha mkuu kabla ya Mbelgiji kuchukua mikoba.

Kocha wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohammed 'Baresi'  alisema kitendo cha Djuma kutoelewana na kocha mkuu ni makosa ya kibinadamu ambayo uongozi kabla ya kumtimua ilipaswa kuwaweka chini kuwapanisha.

"Ukiachana na mambo ya mpira, kocha mkuu unaweza kuumwa, kupewa adhabu ya kufungiwa au vyovyote vile akakosena kwenye timu, hivyo unapokuwa na msaidizi anaendeleza gurudumu, lakini kama Simba imeamua kumsikiliza kocha mkuu, basi inapaswa mapema sana wapate mtu atakayeziba pengo la Masudi," alisema Baresi.

Alisema anamtakia kila kheri Djuma kokote atakakokwenda kufundisha soka kwa kuwa ni kocha mwenye uwezo mzuri na ameisaidia kuijenga Simba japo sasa amepewa mkono wa kwaheri.

Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema hali ilivyokuwa Simba, ili mambo yakae sawa ilikuwa lazima mmoja kati ya Djuma au Mbelgiji aondoke.

Alisema hata kocha msaidizi atakayekuja Simba asiwe kutoka nje ya nchini, waajiri kocha mzawa ambaye atamsaidia Mbelgiji lakini pia akitumia nafasi hiyo kujifunza kwa kocha wa Kigeni.

"Unajua tatizo linakuja baada ya makocha wote kuwa na ubora unaolingana, hivyo hakuna anayetaka kujishusha kwa mwingine, lakini kama Simba ingekuwa na kocha msaidizi mzawa ambaye anahitaji kujifunza kwa kocha mkuu wala kusingekuwa na mvutano," alisema Kibadeni.

Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda ingawa hakutaka kuingilia kati sakata la Djuma na Simba, alisema kocha msaidizi ndiye kila kitu na kocha mkuu ni mtu wa mwisho.

"Wenzetu kocha mkuu huwa anatafuta mwenyewe msaidizi wake, hata hapa nchini kuna timu zinafanya hivyo na nyingine hazifanyi, lakini katika mpira suala la Simba tuwaachie wenyewe ila kocha msaidizi ni mtu wa muhinu sana ndiye mwenye timu, anakuwa karibu na wachezaji na hata kambini yeye ndiye ana lala," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars.