Benchi lamnyima raha Martin

Muktasari:

Kitendo cha Emmanuel Martin wa Yanga, kukosa kibali cha kuiminiwa mbele ya kocha wake Mkongomani Mwinyi Zahera kinamnyima usingizi na kufanya ajitume zaidi akiamini ipo siku Mungu atamshushia neema yake.

KAMA ulikuwa unadhania Emmanuel Martin anafurahia kuishia kucheza mazoezini na anapofika uwanjani anageuka mtazamaji wa wenzake basi utakuwa umechemka hali hiyo inamuumiza sana mchezaji huyo.
Katika kupiga stori mbili tatu na MCL Digital  likabaini kuwa Martin anatamani sana itokee siku apangwe mojawapo ya mechi katika msimu huu ili aweze kuondoa gundu.
Anafunguka kuwa "Si kitu kizuri kwa mchezaji kutocheza, inaniumiza na kunifunza kujituma kwa bidii ili niweze kumshawishi kocha ili kunipa nafasi ya kucheza.

"Msimu huu kwangu unanifanya niwaze mbali zaidi, tofauti na uliopita ambao nilikuwa na nafasi kubwa, naendelea kujituma ili msimu huu usinipite bure, hii ndio kazi ninayoitegemea"anasema.
Lakini kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amewahi kukaririwa kwamba ndani ya kikosi chake anahitaji ushindani ambao utafanya kikosi hicho kifikie malengo.
"Sitaki ndani ya kikosi changu kuona mchezaji nampa nafasi halafu haonyeshi hilo ni jambo baya ambalo litafanya tushindwe kufikia malengo, tunayoyahitaji,"ni kauli ya kocha Zahera.