Akili ya Mbelgiji yote CAF

Muktasari:

Simba itacheza mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuiwakilisha Tanzania na ratiba imetangazwa leo Ijumaa na wamepangwa kucheza na Mbabane Swallows ya Swaziland.

MABINGWA  wa Ligi Kuu Bara Simba wanaendelea kujifua katika uwanja wa Boko Veterans huku baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza wakikosekana wakienda kuzitumikia timu zao za Taifa.
Simba msimu huu watacheza mashindano ya Kimataifa kombe la klabu bingwa Afrika huku wakisubiri ratiba kamili kutoka Shirikisho la soka Afrika (CAF) ambao muda wowote watatangaza ratiba hiyo na Simba kufahamu wataanza na timu gani kutoka katika nchi gani.
Msimu huu Simba malengo yao makubwa ni kuona chama hilo linafanya vizuri zaidi katika mashindano ya Kimataifa tofauti na miaka yote ambayo wamecheza na tayari kocha wa timu hiyo ameshaanza kuandaa na kupiga mahesabu makali ya mashindano hayo yanayoandaliwa na CAF.
Katika ligi Simba wapo kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa wakiwa na pointi 26 sawa na Yanga ila wakiwazidi mabao ya kufungwa na kufanga wakati Azam ndio vinara wakiwa na pointi 30.
Kocha wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems amesema wamecheza mechi 11 mpaka sasa wakiwa wamepoteza moja, sare mbili na kushinda zilizobaki lakini kwake wala hana presha yoyote na matokeo hayo.
Aussems alisema ligi imesimama lakini amekifanyia tathimini kikosi chake na kubaini kuwa hakina mapungufu katika sehemu yoyote ila anachotakiwa kufanya ni kuwaongezea mbinu nyingi wachezaji wake ili kufanya vizuri zaidi ya walipo sasa.
"Mechi hizi 11 na matokeo ambayo tumeyapata wachezaji wangu wamefanya vizuri na kama kuna mapungufu ni ya kawaida ila kuna vitu vya kiufundi zaidi ambavyo nitaongeza ili waweze kufanya vizuri zaidi kama vile ambavyo nataka," alisema.
"Niwapongeze viongozi wamefanya usajili wa wachezaji wa maana kabla sijafika hapa kwani wameonesha uwezo kila mmoja kwa nafasi yake niliyompa na kunifanya kuona timu yangu haina mapungufu yoyote makubwa.
"Kama ningekuwa na mapungufu ya wachezaji ningeanza kufikilia kuongeza nguvu katika dirisha dogo lakini ukweli ni kwamba timu inakwenda vizuri na kama kuna makosa ni yale ya kawaida ambayo kama kocha ni kazi yangu kuyafanyia kazi," alisema.
"Kwangu naona maendeleo ya timu ni mazuri na kadri siku zinavyozidi kwenda timu inabadili na huenda tukawa vizuri na kupata mafanikio zaidi ya hapa tulipo," aliongezea Aussems.
Aussems alisema malengo ya timu ni kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa, kutetea ubingwa wa ligi lakini hata katika mashindano mengine na kadri timu inavyozidi kukaa pamoja anaimani kuna uwezo wa kulifikia hilo.
"Nafikilia ligi lakini tupo na mipango ya muda mrefu kwenye mashindano ya Kimataifa kwa maana hiyo kwangu kama ambavyo tunafanya vizuri katika mashindano ya hapa ndani tutapambana na kufanya hivyo katika kombe la klabu bingwa Afrika," alisema.
"Taratibu ndani ya timu naweka faslasa na mipango yangu kuona Simba msimu huu inatetea ubingwa na katika mashindano ya Kimataifa kufika katika hatua za mbele zaidi kwani hata maandalizi ya mashindano hayo yatakuwa na nyongeza ndani yake tofauti na haya ambayo tunafanya kwa ajili ya mashindano ya ndani.
"Kama kutakuwa na maboresho ya kikosi katika dirisha dogo tutalenga zaidi katika mashindano ya Kimataifa kwani kama wataweza kufanya vizuri huko katika mashindano ya ndani haitakuwa shida kwao.
"Kiujumla wachezaji wangu wote niliokuwa nao wameonesha viwango bora kwani hata wale ambao hawakucheza si kama hawana uwezo wanao bali wamekutana na changamoto ya kupata nafasi," alisema Aussems.
Mratibu wa Simba Abbas Selemani alisema katika kipindi hiki ligi ikiwa imesimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa(Taisa Stars) inajiandaa kucheza na Lesotho wao watacheza mechi ya kirafiki.
"Wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wameondoka lakini tupo na wale ambao pia hawapati nafasi na kama tukicheza mechi ya kirafiki inaweza kuwa nafasi yao kumuonesha kocha wanakitu cha kufanya ndani ya timu," alisema.
"Tunaangalia timu ya kucheza nayo lakini hatutacheza timu chini ya ligi daraja la pili ambao naima watatupa ushindani kutokana na mazoezi ambayo tunafanya kipindi hiki," alisema Selemani.