Wachezaji wa Simba wajazwa noti kibao

Muktasari:

Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba waliocheza kila mmoja atachukua si chini ya Sh 2 milioni, huku wale walioishia benchi kama kipa Ally Salimu watavuta si chini ya Sh 1 milioni na wale ambao waliishia kukaa jukwaani kama Ibrahim Ajibu watabeba si chini ya Sh 500,000.

Dar es Salaam. Nyota wa Simba mbali ya kuonekana kuwa na furaha kwa kufungua vizuri  msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo wa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam FC, mabao 4-2, lakini kuanza leo Jumatatu muda wote akaunti zao zitajazwa noti.
Hii ni baada ya mabosi wa klabu hiyo kuahidi mapema kwamba wangewamwagia mamilioni kama wangeinyoosha Azam ikiwa sehemu ya utartibu waliojiwekea tangu msimu uliopita na kwa ushindi wa juzi  Jumamosi usiku nyota hao watavuta Sh 50 milioni.
Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba waliocheza kila mmoja atachukua si chini ya Sh 2 milioni, huku wale walioishia benchi kama kipa Ally Salimu watavuta si chini ya Sh 1 milioni na wale ambao waliishia kukaa jukwaani kama Ibrahim Ajibu watabeba si chini ya Sh 500,000.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema huo ni utaratibu ambao umewekwa katika timu yao ili wachezaji watamani kufanya vizuri katika kila mechi ili kuondoka na ushindi lakini inaongeza motisha kila mchezaji kutamani kushindana na kucheza katika kikosi cha kwanza.
“Ni utaratibu wetu ambao tunao tangu msimu uliopita katika mashindano yote ambayo tunashiriki kama tutashinda ujue kila mchezaji atapata motisha ya posho ila huwa zinatofautina kulingana na michezo husika kwani mechi nyingine ni kubwa na zinahitaji matokeo ya ushindi kuliko jambo lolote,” alisema.
“Kuhusu ushindi wa hilo tayari limeshapita na akili zetu zipo katika mechi ya marudiano ambayo tutacheza Jumapili dhidi ya US Songo ambayo kiu yetu ni kuona tunashinda na kusonga katika hatua inayofuata.
“Kama vile ambavyo wachezaji na uongozi wanajitolea katika kuhakikisha wanawapa mashabiki furaha kwa kushinda mechi basi na wao wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika mechi na UD Songo kama ambavyo tulifanya msimu uliopita ili kuendeleza wimbo la ushindi,” alisema Magori.