Haruna Shamte chuma chakavu kilichochapika hatari

Muktasari:

Beki huyo wa kulia aliyewahi kutamba na Toto Africans, Simba, Mbeya City na Lipuli anasema fedha yake kubwa kuishika katika soka ilikuwa ni Sh100,000 kipindi hicho akiwa Toto Africans na anakumbuka ilikuwa mwaka 2007.

KATIKA mafanikio buana hakuna njia ya mkato. Kila unayemwona kafanikiwa, basi lazima utambue kapitia changamoto nyingi, kaanguka sana, lakini aliinuka na kupambana hadi kufika alipo.
Hata beki mpya wa Simba, Haruna Shamte ‘Terminator’ a.k.a Chuma Chakavu, mpaka kufika alipo katika soka lake, buana kachapika. Kala msoto wa maana na kathibitisha ule usemi wa mchumia juani daima hulia kivulini. Kwa sasa Shamte anakula kivulini kama mwenyewe anavyofichua safari yake kisoka mpaka kufika alipo.
Mwanaspoti limefanya mahojiano naye, na amefunguka mambo kadhaa ambayo mengine anadai ni vigumu kusahaulika kichwani mwake. Endelea naye...!

ALIKUMBUKA GODORO
Shamte anafichua ni ngumu kwake kusahau safari yake kisoka ilivyoanza, lakini kubwa ni fedha zake za kwanza kabisa katika soka na kitu cha thamani alichokinunua.
Beki huyo wa kulia aliyewahi kutamba na Toto Africans, Simba, Mbeya City na Lipuli anasema fedha yake kubwa kuishika katika soka ilikuwa ni Sh100,000 kipindi hicho akiwa Toto Africans na anakumbuka ilikuwa mwaka 2007.
“Kwanza nilikuwa naiona kama milioni kipindi hicho, nilipoitia mkononi kitu cha kwanza ambacho nilikifikiria ni godoro buana, enzi hizo ukinunua godoro kwa wenzako unaonekana mjanja kinoma,” anasema.

SOKA LIMENIPA NYUMBA
Soka imekuwa biashara nzuri kwa sasa, hilo linathibitishwa na Shamte kupitia kazi hiyo amefanya vitu vingi vya maendeleo ikiwemo kujenga mjengo anaoishi jijini Dar es Salaam.
Anasema kwa sasa anazidi kupambana hili kuhakikisha anajitengenezea misingi imara ya siku za baadaye pale atakapostaafu kwa kutambua kwenye soka umri wa kustaafu ni mkubwa na kama mtu hajajiandaa huenda akapigika na hata kuwa kero kwa wengine.
“Sio kila kitu lazima nikianike, lakini naendelea kujipanga kuweka kila kitu sawa kwangu na familia yangu, soka halina muamana,” anasema .

SIMBA YAMBEBA KIAINA
Anacheza Simba kwa nyakati tofauti kwa mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2009/14, anakiri kunufaika katika mambo mbalimbali kama kumtambulisha kwa Watanzania na hatua za kimaisha.

TUKIO ASILOSAHAU
Akiwa na Mbeya City mwaka 2017 aliumia mguu wa kushoto aliouuguza kwa mwezi mmoja, jambo ambalo ni tukio ambalo lilimuumiza kupita kiasi.
“Kitendea kazi kikubwa cha mchezaji ni mguu wake, soka ndio kazi nilioichagua kitendo cha kuumia, kilikuwa kinaharibu saikolojia yangu, ingawa nilijiuguza  mwezi mmoja tofauti na wenzangu ambao wanakaa nje  mwaka mzima,” anasema.

SARE YA MAAJABU
Anasema anayemaliza kwa kicheko ndiye mwenye furaha kuliko aliayeanza kwa kicheko akamaliza kwa machungu, anaukumbuka mwaka 2013 kwenye mechi ya nani mtani jembe kati ya Simba na Yanga. Anasimulia kitu kilichoandika alama ya furaha moyoni mwake na bado kinaishi ni kitendo cha Yanga kuwafunga bao 3-0, ambazo wakaja kuzirudisha kipindi cha pili.
“Kipindi cha kwanza nilikuwa natamani kulia, kicheko kikaja kipindi cha pili ambao tukasawazisha mabao 3-3 na kuwaacha Yanga wakilia, kitu hicho kilinifurahisha na sitakisahau,” anasema.

KIKOSI BOMBA KWAKE
Ametaja kikosi ambacho anaamini kilikuwa na wazee wa kazi ambao anasema hatakaa awasahau katika maisha yake ya soka kuwa ni; Juma Kaseja, Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, Haruna Shamte, Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondan, Juma Nyoso.
Wengine ni Joseph Owino, Jerry Santo, Mohammed Banka, Jabir Aziz, Hillary Echessa, Nico Nyagawa, Hassan Mgosi, Emmanuel Okwi, Uhuru Seleman, Ulimboka Mwakingwe, George Nyanda, Ramadhan Chombo ‘Rodondo’, Amri Kiemba, Rashid Gumbo na Haruna Moshi ‘Boban’.
“Kikosi hiki cha mwaka 2011 kilitawanyika kila mchezaji yupo sehemu nyingine, kama Boban, Nyosso, Yondani unaona wote hao ni mafundi wa mpira, kiukweli wakicheza unaona wana kitu fulani mguuni, Kaseja hakucheza muda mrefu kwenye kikosi cha Stars, amepewa nafasi kaonyesha,” anasema.

SOKA LAMPA MKE
“Hii kazi naipenda ndio maana nimeweza kuoa mke niliyemtaka kutokana na kipato cha kumlipia mahari,” anasema na anamtaja mkewe huyo anayeeleza anampenda kinoma kuwa ni Shemsa aliyezaa naye mtoto mmoja wa kiume.

SIMBA YA SASA
Anasema amerejea Simba kwa mara nyingine ikiwa na ushindani wa hali ya juu, akidai anaamini ni wakati rasmi wa kusikika tena mbele ya wadau wa soka nchini.

KWA NINI KAREJEA  SIMBA?
Kama kuna kitu anakiamini ni ridhiki inatoka kwa Mungu, akielezea namna ambavyo amerejea Simba kwa mara nyingine kwamba viongozi walimfuata wakihitaji huduma yake.
“Waliniona kiwango ambacho nilikioonyesha nikiwa na Lipuli ya Iringa, ila niseme tu ni Mungu ameamua kuninyoshea njia, kazi kwangu kupambana na kuhakikisha nafanya kitu kilichotarajiwa kutoka kwangu,” anasema.
 
USHINDANI NA KAPOMBE
Mshindani wa namba wa Shamte ndani ya Simba ni Shomary Kapombe, amekiri ana uwezo wa juu, ila anachokijua yeye, amekwenda kufanya kazi na sio kushanga wenzake wakifanya kazi.
“Napenda kushindana kwani naamini hilo ndilo litanifanya niwe imara na kazi bora, Kapombe ni mchezaji mzuri ila tutashindana na hilo litamfanya kocha Patrick Aussems awe na kikosi anachokiamini, binafsi najiamini sana,” anasema.

KUITWA STARS
Shamte ni kati ya wachezaji wakongwe ambao walijumuishwa kwenye kikosi cha Stars, kilichokuwa kinacheza michuano ya CHAN kwa wachezaji wa ndani Afrika, anasema anaamini kocha aliona kitu kwake.
“Ndio maana nimekutajia kikosi ambacho sitakisahau kule juu, akiwemo Kaseja, Kelvin na wengine, najiamini na nitaendelea kujiamini na ndio maana kipindi nilipokuwa nimeachana na Simba nilikuwa nomo tu,” anasema.
 
NAYE KAMA ANELKA
Kuna baadhi ya wachezaji wanajua kuzurura kutoka timu moja hadi nyingine duniani, watu kama Nicholas Anelka, Zlatan Ibrahimovic na wengine, lakini kumbe hata Shamte naye hajambo, japo hajamfikia Elias Maguri ambaye kwa sasa katimkia Afrika Kusini.
Anayekiri soka ndicho kitega uchumi chake cha kumuingizia riziki, ameanza soka timu za mchangani, jijini Mwanza kabla ya kufahamika rasmi mwaka 2007 akiwa na Toto Africans aliyoichezea kwa misimu miwili kabla ya mwaka 2009 kunyakuliwa na Simba aliyodumu nao hadi mwaka 2014.
Alipotoka hapo alitua JKT Tanzania (zamani JKT Ruvu), kisha kwenda Mbeya City kwa misimu miwili na kisha msimu uliopita kuhamia Lipuli aliofika nao fainali ya Kombe la FA na kupoteza mbele ya Azam.
Msimu huu unaoanza wiki ijayo, amerejea nyumbani Msimbazi akienda kuungana na wakali wengine wa kikosi hicho kitakachotetea taji la Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu.
“Nimepitia timu mbalimbali kwa nia ya kubadilisha changamoto na pia suala zina la masilahi na kwamba huwa sikati tamaa kirahisi katika kuitafuta riziki ukizingatia kuwa, riziki yangu ipo miguuni kwa kusakata soka,” anasema, beki huyo mcheshi.