Abdallah 'Try Again': Simba tumetimiza wajibu wetu

Sunday March 17 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' amesema ahadi walizozitoa kwa wachezaji wao pamoja na maandalizi kambambe vimechangia kuibeba timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliweka rekodi kwa mara nyingine tena kutinga robo fainali baada ya kuwalaza AS Vita ya DR Congo kwa mabao 2-1, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Viongozi tulishikamana. Awali tulikuwa na malengo ya kufika makundi lakini tulivyoona tuna timu nzuri tulikaa chini na kuweka mikakati ya namna ya kuvuka hatua hiyo.

“Hakuna kingine zaidi ya maandalizi mazuri pamoja na ahadi mbalimbali kwa wachezaji wetu, vyote hivyo vimeifanya leo hii Simba kuipeperusha vema bendera ya nchi yetu kimataifa,” alisema Try Again.

Kaimu Rais huyo wa zamani wa Simba alisema kinachofuata kwa sasa ni wao viongozi kusubiri marejesho ya Kocha baada ya kusonga mbele ili kuona kwa namna gani wafanye vizuri.

“Kila kitu kipo mikononi mwa kocha wetu. Mwanzo alitaka michezo mingi ya kirafiki tulifavyo hivyo ili kutekeleza matakwa yake,” alisema.

Try Again alitoa shukrani zake za dhati kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakiisapoti timu hiyo tangu ilipoanza harakati ya kupigania nafasi ya kuingia hatua ya makundi ya michuani hiyo mikubwa Afrika ngazi ya klabu.

Advertisement