Huko Yanga kumenoga aisee

Muktasari:

  • Mwandila Yanga ina wachezaji wengi kila mmoja anatamani kucheza kikosi cha kwanza naamini kujituma kwao na kukosekana kwa baadhi ya nyota ambao walikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa kushindwa kujiunga mapema kwaajili kujiandaa na mchezo dhidi ya Allayance kunaweza kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji kuanza kucheza.

ACHANA na ufundi wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kiasi cha kumduwaza Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, unaambiwa huko Yanga kwa sasa mambo yamenoga na kilichobaki ni vijana wa Jangwani kufanya yao tu katika Ligi Kuu inayoendelea kesho. Ni hivi. Inaelezwa kitendo cha beki Gadiel Michael kujumuishwa kikosi cha Stars, kimeleta neema kwa Mwinyi Haji anayatarajiwa kuvaa uzi watakapoikabili Alliance ya Mwanza, Jumamosi hii Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Lakini pia nyota wengine ambao hawakuwa wakipata nafasi katika kikosi cha kwanza wana nafasi kubwa ya kujumuishwa kwenye mchezo huo ambao Yanga watautumia kuendeleza rekodi yao ya kupototeza hata mchezo mmoja hadi sasa.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila aliwahakikishia nyota wake wa kikosi cha pili akiwamo Haji Mwinyi, Emmanuel Martin, Yusuf Mhilu kuvaa uzi Jumamosi dhidi ya Alliance na kuleta shangwe kwa vijana hao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwandila alisema katika mchezo wao wa kirafiki wa kumuaga nahodha wao wa zamani Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alitoa nafasi kwa nyota wake wanaoanzia benchi na kufanya vema kwa kuibuka na ushinfi wa 2-0 dhidi ya Malindi, huku akibaini mambo mazuri kutoka kwa wachezaji hao.

“Kuna baadhi ya wachezaji bado hawajaungana na timu baada ya kumaliza majukumu ya taifa, ila leo wanaweza kujiunga na wenzao katika mazoezi nafikiri watakuwa na siku mbili za mazoezi kabla ya kuwavaa Alliance naweza nikawapa mapumziko na kuwatumia nyota wengine niliokuwa nao pamoja tangu mwanzo wa maandalizi yetu.”

“Sipendi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja katika timu kikubwa ninachoweza kusema walifanya vizuri na ndio maana tuliweza kufanikiwa kuibuka na ushindi muda wao ukifika kucheza katika kikosi cha kwanza cha ligi watacheza kikubwa ni wachezaji wa Yanga na ndio maana muda wote wapo katika timu,” alisema.

PENGO LA DANTE

Beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ anatarajia kuwakosa Alliance katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi kutokana na kukabiliwa na adhabu aliyopewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la SOka nchini (TFF) kumfungia kucheza mechi tatu kutokana na utovu wa nidhamu kocha alisema ni pengo kubwa kwa timu lakini anaamini nyota waliopo watafanya vizuri.

“Ni mchezaji muhimu katika timu na amekuwa akitegemewa katika kikosi cha kwanza kukosekana kwake ni pengo lakini linaweza kuzimwa na wachezaji wanaocheza namba yake kwa kutumia nafasi ya kucheza vizuri na kumuaminisha mwalimu kuwa na wao wanaweza hata bila Dante,” alisema

“Yanga ina wachezaji wengi wazuri pamoja na kushindwa kupata nafasi ya kucheza wamekuwa wakijitahidi kupambana mazoezini lengo ni kuhakikisha wanatushawishi waalimu tuweze kuwapa nafasi sasa ni wakati wao sahihi kuonyesha watanzania pamoja na mashabiki wa timu kuwa sio Dante tu ambaye amezaliwa kwaajili ya kuisaidia Yanga katika nafasi hiyo,” alisema.

AJIBU ASHANGAZA

Tofauti na alivyozoeleka Ibrahim Ajibu kuonekana ni mtu mwenye kutega mazoezi na alishaingizwa katika listi ya nyota kadhaa wanaokatwa mishahara kutokana na kukosa mazoezi, hali imekuwa tofauti sasa kiasi cha kimemshangaza kocha Mwandila.

Mwandila alisema Ajibu amekuwa mchezaji wa kwanza kufika mazoezi na amekuwa akiwahimiza wenzake, jambo ambalo ni mabadiliko makubwa kwa mchezaji huyo na kumtabiria makubwa hapo mbele kama ataendelea kufanya hivyo.

“Huwezi kuamini Ajibu tangu tumeanza Jumatatu siku moja baada ya kutoka Zanzibar tayari kujiandaa na mchezo dhidi ya Alliance, ndiye anayeongoza kwa kuwahi mazoezi na muda mwingine anaonekana kuwahimiza wenzake ni tofauti na nilivyomzoea ni mtu ambaye alikuwa anapenda kutega na kutoa sababu zisizokuwa na msingi.”

FEI TOTO NOMA

Katika hatua nyingine mpira mwingi alioupiga kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndani ya dakika 32 alizopewa na Kocha Amunike wa Taifa Stars zimemkuna kocha huyo na kumwagia sifa.

Feisal anayekipiga Yanga, aliingia akichukua nafasi ya Mudathir Yahya dakika 58 katika mechi dhidi ya Cape Verde na kubadilisha kabisa mchezo kutokana na jinsi alivyocheza kwa kutoa pasi za uhakika na kulainisha safu ya kiungo pale katikati.

Kocha Amunike alisema jinsi Fei alivyoitwa Stars mazoezini alikuwa anafanya vitu vya kawaida, ila alimwambia Stars ni kama Ligi ya Italia anatakiwa apambane na ameonyesha.

“Alinisikia na kunielewa na hata alipoingia alifanya timu ikae sawa katika upande wa kiungo na hiki ndicho ambacho tunakihitaji katika timu yetu.” Alisema.