Makame awataka Stars kuweka uzalendo mbele

Muktasari:

Makame ambaye yupo kwao Zanzibar kwa mapumziko, alijiunga na Yanga wiki chache zilizopita kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

KIUNGO  mpya wa  Yanga, Abdul Aziz Makame anayetokea timu ya Mafunzo ya Zanzibar, amesema timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itawashangaza wengi kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri.
Makame amekuwa akifanya vizuri na timu ya taifa ya Zanzibar, alisema kikubwa kila mchezaji wa Stars anatakiwa kuwa na moyo wa uzalendo na kupambana.
“Ukiwa mzalendo utaweza kupigana hadi dakika za mwisho, ukiangalia timu tulizonazo kundi leti ni ngumu lakini kama kila mmoja atajitoa na kujituma basi hakuna kitakachoshindikana.
“Walicheza vizuri na Misri jana Alhamisi kikubwa ni kocha kufanyia kazi mapungufu kadhaa yaliyojitokeza ili kufanya vizuri,” alisema Makame.
Alisema ndoto yake ni kuvaa jezi ya Taifa Stars kwa siku za usoni ili kutoa mchango wa kipaji chake kwa taifa.
“Naamini ni suala la muda tu kwangu kila kitu kitakaa sawa,” alisema nyota huyo.