Yanga yashtukia ishu zote Simba
Muktasari:
Ameitazama ratiba ya Ligi Kuu Bara na kugundua mambo kadhaa, lakini kubwa ni namna timu yake ya Yanga ilivyowekwa kwenye mtego kabla ya kuvaana na Simba ambao wamepania kutwaa ndoo kwa gharama yoyote ile msimu huu.
KOCHA aliyeshinda taji la Ligi Kuu Bara ndani ya miezi sita tu ya kazi hapa nchini, George Lwandamina, amegundua kitu ambacho mashabiki walikuwa hawajajua kuelekea mechi ya Simba Oktoba 28.
Ameitazama ratiba ya Ligi Kuu Bara na kugundua mambo kadhaa, lakini kubwa ni namna timu yake ya Yanga ilivyowekwa kwenye mtego kabla ya kuvaana na Simba ambao wamepania kutwaa ndoo kwa gharama yoyote ile msimu huu.
Lwandamina ambaye kabla ya kutua Yanga alitoka kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu Zambia akiwa na Zesco United, amebaini kama hawatajipanga vizuri wanaweza kuwa na mchezo mgumu dhidi ya watani zao hao waliowatoa nishai kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani.
Ipo hivi. Kabla ya Yanga kucheza na Simba, itakuwa imecheza jumla ya mechi nne ugenini tofauti na watani zao hao ambao watakuwa wametoka mara mbili tu kwenda nje ya Dar es Salaam.
Yanga tayari imecheza mechi mbili za ugenini dhidi ya Njombe Mji na Majimaji na kupata alama nne huko lakini kabla ya kuvaana na Simba, itacheza mechi nyingine mbili dhidi ya Kagera Sugar na Stand United.
Simba kwa upande wao watakuwa wamecheza mechi mbili tu ugenini ambayo ni ya leo dhidi ya Mbao FC kule Mwanza na unaofuata dhidi ya Stand United mjini Shinyanga kisha itatulia Dar es Salaam kuwasubiri watani zao hao wapate dhoruba ugenini.
“Tumewekewa mtego lakini hakuna namna. Mechi nne ugenini kabla ya mchezo wa watani, siyo jambo jepesi hasa ukizingatia mechi ya mwisho tunacheza ugenini ndipo tucheze na Simba,” alisema Lwandamina ambaye makazi yake yako kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam .
“Mechi za ugenini ni ngumu, zinahitaji kujitoa sana kwani huna faida ya kuwa nyumbani. Hata hivyo kila kitu kinafanyika kwa mapenzi ya Mungu, tunapaswa kupambana sana,” alisema Lwandamina ambaye Yanga ndiyo klabu yake ya kwanza kubwa kufundisha soka nje ya Zambia.
“Ratiba kwa ujumla pia ina tatizo, hatuwezi kucheza kwa msimu mzima bila kupumzika, inaumiza sana. Wachezaji hata kama wako fiti vipi, wanahitaji mapumziko,” aliongeza kocha huyo mwenye umri wa miaka 54.
“Timu zitakazoumia ni zenye wachezaji timu za Taifa, hawa ndiyo hawatapumzika kabisa.”