Yanga, Simba zatangaziana vita ya siku 28
MWANDISHI WETU KWA siku 28 kuanzia leo Jumamosi; Yanga, Azam na Simba zitakuwa katika vita kubwa kwani katika siku hizo anaweza kufahamika bingwa pamoja na mshindi wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba, Yanga na Azam kila moja imesaliwa na mechi sita za kijanja kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara na zina mtihani wa kucheza na hesabu kwenye mechi nne tu ndani ya siku 28 kutibuliana zenyewe kwa zenyewe. Mechi nne zijazo kwa Yanga, Azam na Simba zitaanza leo Jumamosi mpaka Aprili 27, na zinaweza kumaliza ubishi kati ya miamba hiyo mitatu, licha ya ukweli kuwa ligi yenyewe itamalizika Mei 18. Timu hizo zote ziko mikoani leo Jumamosi zikicheza mechi za Ligi Kuu Bara. Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 48 ipo Morogoro ikicheza na Polisi na ili iwe salama na kufuta ndoto za Azam kuchukua ubingwa inapaswa kushinda mechi nne tu. Azam yenye pointi 40 ikishinda michezo yake sita itaishia pointi 58 ambazo Yanga ikishinda mechi nne inazivuka na hivyo kutangazwa mabingwa wapya wa Tanzania Bara. Mechi hizo nne za Yanga ni dhidi ya Polisi Morogoro (Morogoro), JKT Oljoro (Dar es Salaam), Mgambo JKT (Tanga) na JKT Ruvu (Dar es Salaam). Lakini ikiweza kukamilisha rekodi hiyo bado itakuwa na chenji au mechi mbili za kukamilisha ratiba dhidi ya Coastal Union mjini Tanga na Simba jijini Dar es Salaam. Lakini, kasheshe nyingine ipo kwa Simba na Azam ambayo imesababishwa zaidi baada ya Simba inayocheza leo Jumamosi dhidi ya Toto African mjini Mwanza kupoteza mechi yake Jumatano iliyopita dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba. Azam ikishinda mechi nne tu na sare moja itafuta matumaini ya Simba kupata nafasi ya pili kwani itakuwa na pointi 53 ambazo itamzidi Simba kwa pointi pointi moja na bado Azam itakuwa na mechi nyingine mkononi. Ngumu zaidi ni kwamba Simba kupata pointi 52 inahitaji kushinda mechi zote sita ikiwamo ya Yanga, Mei 18. Ukianzia na mechi ya leo Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting huko Pwani, Azam ina mechi nyingine dhidi ya Lyon, Simba (zote Dar es Salaam), Coastal Union (Tanga), Mgambo (Dar es Salaam) kabla ya kumaliza kwa JKT Oljoro mjini Arusha. Simba ikimalizana na Toto African leo Jumamosi itafuatiwa na mechi dhidi ya Azam, Ruvu Shooting, Polisi Morogoro, Mgambo JKT na Yanga michezo yote ikiwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa wenye nyasi za kuteleza zinazozitoa jasho timu za mikoani. Mechi nyingine za leo Jumamosi ni Oljoro JKT dhidi ya wanajeshi wenzao wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha huku Kagera Sugar na Mtibwa Sugar ambao ni ndugu wakicheza kwenye Uwanja wa Kaitaba wakati African Lyon inayoshika mkia ikimenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam. Ligi Kuu Bara inamalizika Mei 18 na timu tatu zitapaswa kushuka daraja na mpaka sasa JKT Ruvu, Polisi Morogoro na African Lyon ndizo zinazong'ang'ania nafasi hizo kuzipisha Rhino ya Tabora, Ashanti ya Dar es Salaam na Mbeya City zilizopanda msimu huu.