Tenga awauma sikio viongozi, makocha akizindua kitabu cha Kayuni
Muktasari:
Maudhui ya kitabu cha Kocha wa Soka hayakulenga walimu peke yao, pia kimelenga kutoa elimu ya kiufundi ya mchezo wa mpira wa miguu kwa viongozi, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Leodgar Tenga amewataka viongozi kuwa na uelewa juu ya masuala ya msingi ya kiufundi ya mpira wa miguu kwani ndio njia pekee ya kuwafanya wawe na sifa ya kushika nafasi walizonazo.
Tenga ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 21,wakati akizundua kitabu kiitwacho 'Kocha wa Soka' kilichoandikwa na mwalimu Sunday Kayuni huku akitoa rai kwa wapenzi wa mpira wa miguu na walimu kukitafuta kitabu hicho kwa kukosoma kwa faida zao binafsi na kwa maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Tenga amesema endapo kiongozi hana uelewa wa mambo muhimu ya msingi ya kiufundi basi hastahili kuongoza.
Tenga amempongeza Kayuni kwa kuandika kitabu hicho na kusema ni wachache waliojaliwa kuyaweka yale wanayosema katika mandishi na ndio maana uandishi ni Taaluma.
Tenga amesema kupitia kitabu cha Kocha wa soka,Mwalimu Kayuni amefanya kazi nzuri ya kuwaelimisaha walimu wa mpira wa miguu sio tu kuhusu mfumo wa njia ya ufundishaji , bali pia sifa na kazi za mwalimu wa mchezo wa mpira wa miguu.
"Hivyo yaliyomo katika kitabu hiki siyo tu yatawawezesha walimu kufundisha vizuri zaidi bali pia kuwafahamisha kuwa wanastahili wawe na sifa zipi ili waheshimike na kuogeza ufanisi kiutendaji".
"Hapana shaka kuwa elimu ya kiufundi ya mpira wa miguu inakufanya uwe kiongozi,mdau na mshabiki bora zaidi kwa vile utakuwa na ufahamu mzuri zaidi wa nini kinaendelea, kujua matatizo ya timu yako hasa ni yapi na nini kifanyike.Uelewa wa mbinu za mchezo utamfanya mdau au mpenzi awe na ubishi wenye tija, yaani ubishi wa hoja na sio ubishi wa kinazi peke yake', amesema Tenga .
Tenga amesema mwalimu Kayuni ametimiza wajibu wake kwa kuandika kitabu hicho katika kuwezesha kupiga hatua kama Taifa katika mchezo wa mpira wa miguu hivyo alitoa rai kwa wengine kuendeleza jitihada ya kuelimisha jamii kwa kuandika vitabu vingi zaidi vya taaluma ya michezo.
Naye mwandishi wa kitabu hicho, Kayuni amesema nia na kusudi kubwa la kuandika kitabu hicho ni kujaribu na kukabiliana na changamoto ambazo zipo kwa makocha na wadau wa mpira wa miguu kwa ujumla katika kuuelewa mpira wa miguu.
"Nimekuwa na watu wanaonizunguka ambao wamekuwa kila wakati wakinipa msukumumo kwa nini siandiki kitabu na yote ilitokana kuna kitu waliona kwangu na ndio maana ikabidi niandike kitabu hiki.
Kayuni amesema kitabu hicho hususani ni kwa ajili ya makocha,kwani maudhui yaliyomo ni pamoja na historia ya mpira wa miguu, kocha ni nani,sifa za mtu kuwa kocha, kazi za kocha,Falsafa ya kocha, Maadili ya kocha, Saikolojia inamsaidia vipi kocha katika kazi yake, Habari ya Mawasiliano na namna bora ya ufundishaji wa mpira wa miguu
"Nimejaribu kudadavua, kuchanganua na kueleza kwa ufasaha ili kuona kwamba kocha akiksoma inaweza kumsaidia kufanya kazi yake kwa umahiri, pia wapenzi na wadau wa soka inaweza kuwapeni ufahamu mzuri wa kimichezo", amesema Kayuni.