Simbu, Manula, wabeba tuzo za BMT

Muktasari:

  • Simbu aliyeibuka pia mshindi kwa upande wa riadha nchini, aliweka heshima mwaka jana kwa kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Madola iliyofanyika Birmingham, England na kwenye tuzo ya jumla za juzi aliwashinda  Yusuph Changarawe, Kassim Mbutike ambao ni mabondia wa ngumi za ridhaa na bondia nyota wa ngumi za kulipwa, Ibrahim Mgandera 'Ibrahim Class'.

KIPA tegemeo wa Simba na Taifa Stars, Aishi Manula ametwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka 2022 zilizotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), huku nyota wa riadha, Alphonce Simbu akibeba tuzo ya Mwanamichezo Bora wa jumla wa tuzo hizo zilizotolewa juzi usiku Jijini Dar.

Simbu aliyeibuka pia mshindi kwa upande wa riadha nchini, aliweka heshima mwaka jana kwa kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Madola iliyofanyika Birmingham, England na kwenye tuzo ya jumla za juzi aliwashinda  Yusuph Changarawe, Kassim Mbutike ambao ni mabondia wa ngumi za ridhaa na bondia nyota wa ngumi za kulipwa, Ibrahim Mgandera 'Ibrahim Class'.

Mgeni rasmi katika tuzo hizo zilizofanyika  ukumbi wa Mlimani City, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana alimkabidhi Simbu tuzo hizo zilizoandaliwa na BMT chini ya uratibu wa kampuni ya Radian na kudhaminiwa na Azam Media Limited, taasisi ya kifedha ya Faidika na NBC.
Katika usiku wa tuzo hizo, Rais Samia pia alipewa tuzo ya heshima ya kuchangia na kutia hamasa kuwa katika maendeleo ya michezo. Tuzo hiyoalipokea Waziri Chana kwa niaba yake.

Akizungumza mara baada ya kushinda tuzo hizo, Simbu alisema amepata faraja kubwa na ushindi huo umemuongezea ari ya kufanya vyema katika mashinadano ya kimataifa ikiwa pamoja na Olimpiki ya mwakani mjini Paris, Ufaransa.

“Nimefarijika sana kwa ushindi huu na umenipa hamasa ya kufanya vyema zaidi. Naipongeza serikali kwa kuandaa tuzo hizo na pongezi za dhati kwa Rais Samia Suluhu kwa kuweka hamasa kubwa katika michezo,” alisema Simbu.
Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga alisema tuzo hizo zitakuwa zinafanyika kila mwaka huku kukiwa na uboreshaji mkubwa kwa lengo la kuleta hamasa nchini hasa kwa wanamichezo chipukizi, huku Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha alipongeza wadau wote kwa kufanikisha tuzo hizo na kuwaomba kuwaendelea kuwaunga mkoni.


Washindi wengine
Rehema Saidi alishinda tuzo mbili, ya kwanza ya mwanamichezo bora wa mwaka kwa upande wa tenisi  kwa wenye ulemavu (Wheel Chair) na tuzo ya mwanamichezo bora wa kike kwa upande wa watu wenye ulemavu.

Halfani Kianga: Mchezaji Bora wa kiume na Mchezaji Bora wa Mwaka kwa Soka la wenye ulemavu.
Tembo Warriors: Timu bora ya mwaka kwa upande wa wanaume soka la wenye ulemavu
Kabaddi: Timu bora ya Kabaddi ya taifa wa wanawake
Kabaddi: Timu bora ya Kabaddi ya taifa wa wanaume                  
Gofu: Timu bora kwa mchezo huo ni timu ya Taifa ya wanawake Serengeti Girls
Soka Wanawake: Timu Bora ni Simba Queens
Gofu: Mchezaji bora wa wanawake: Madina Idd
Kriketi: Timu bora ya wanawake ya chini ya miaka 19
Kriketi Wanawake: Fatuma Kibaso
Kriketi Wanaume: Evan Ismail
Ngumi Ridhaa: Yusuph Changalawe
Ngumi za Kulipwa: Ibrahim Class
Riadha Wanawake: Failuna Matanga
Riadha Wanaume: Alphonce Simbu
Soka Wanaume: Aishi Manula
Soka Wanawake: Clara Luvanga
Michezo ya Shule Wanaume: Raphael Sanga
Michezo ya Shule Wanawake: Regina Serikali
Kuogelea: Timu ya Taifa ya The Tanzanite
Soka Wanawake: Serengeti Girls
Kabaddi: Mchezaji bora wa kike: Amina Ally
Mchezaji bora wa kiume: Juma Sultan
Kuogelea: Mchezaji bora wa kike: Sophia Latiff
Kuoegelea: Mchezaji bora wa kiume: Collins Saliboko