Senzo: Najua siri yao, tutawapiga tena Kigoma

Muktasari:

SIMBA wanatamba wametangulia mkoani Kigoma lakini Yanga wamesikia hizo taarifa kisha wakashtukia jamaa wamepania na kuwaambia wajiangalie watapigwa tena.

SIMBA wanatamba wametangulia mkoani Kigoma lakini Yanga wamesikia hizo taarifa kisha wakashtukia jamaa wamepania na kuwaambia wajiangalie watapigwa tena.

Simba inapigana kuhakikisha wanalipa kisasi cha kufungwa na Yanga kama ilivyotokea Julai 3 pale Uwanja wa Mkapa Wekundu wakilala kwa bao 1-0, matokeo ambayo yalitibua sherehe za ubingwa wa nne mfululizo kwa mabingwa hao.

Yanga inajua Simba imepania kulipa kisasi na bosi wao Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti unaweza kupania kulipa kisasi lakini hatua hiyo isifanikiwe na ndani kwao kuna hesabu nzito za kuwapiga tena watani wao kwani wanawafahamu vizuri.

Senzo ambaye amewahi kufanya kazi Simba kama Mtendaji Mkuu alisema wao pia wana hesabu nzito kuelekea mchezo huo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na wanataka kufunga msimu wakiwa na ndoo ya pili mbele ya wekundu hao ikiwemo ubingwa wa Kombe la Mapinduzi walioifunga kwa penalti 5-4.

“Tunajua wamepania kulipa kisasi, hizo ni hesabu zao na sisi Yanga tuna zetu, kuna wakati unaweza kupania kupata kitu na kisha usikipate na hatupo tayari kuliruhusu hilo.

“Tunahesabu kubwa sana katika mchezo huu wa fainali tunataka kuufunga msimu kwa mafanikio zaidi, tunahitaji kuongeza kombe lingine ili tuwe na kitu fulani cha tofauti zaidi kufanikia hayo ni lazima tushinde tena,” alisema Senzo. Yanga inakutana na Simba Julai 25 kule Kigoma katika mchezo wa fainali hiyo itakayopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika,

Senzo alisema hatua kubwa zaidi ndani ya klabu yao kuna umoja umeongezeka kwa viongozi kuwa pamoja na wanachama woa kuhamasika kuipambania timu yao.

Alisema tayari kila makundi yapo katika maandalizi ya mchezo huo huku akiwataka baadhi ya wanaoendelea kushangilia ushindi wa awali kusitisha kwa muda hilo na warudi vitani.

“Naijua Yanga sasa, ukiangalia huku juu kwenye uongozi kuna umoja mkubwa sana, viongozi wote sasa wanazungumza kitu kimoja lakini wanachama na mashabiki wetu nao hawako mbali na timu yao wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaipigania timu yao.

“Hii ni hali fulani ambayo inavutia sana hapa ndio unapokamilisha kuiita timu ya wananchi kwa kuwa wananchi na viongozi wao wako kwa ajili ya timu yao.

“Kwenye timu nako maandalizi yanaendelea tunafuatilia kila hatua maendeleo ya timu yetu na wachezaji wanajua umuhimu wa kushinda mechi kama hii kubwa kuna utamu wa aina gani wanaupata na wanajua wanapata kutokana na nguvu ya wadhamini wetu hasa GSM ambao wanafanya kila kitu kuhakikisha akili ya wachezaji inakuwa katika kupigania ushindi.”