Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi TZ v Yanga kupigwa Usharika Bodi yathibitisha

Muktasari:

  • Uthibitisho huo umekata mzizi wa tetesi zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kuhusu uwezekano wa mchezo huo kuhamishiwa uwanja mwingine, huku mashabiki wa soka mkoani Kilimanjaro wakisubiri kwa hamu kuiona Yanga ikishuka dimbani kwenye ardhi yao.

HATIMAYE fumbo la mahali utakapochezwa mchezo wa Polisi Tanzania dhidi ya Yanga, limepatiwa majibu baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kuthibitisha kuwa pambano hilo litapigwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, Novemba 20, 2026.

Uthibitisho huo umekata mzizi wa tetesi zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kuhusu uwezekano wa mchezo huo kuhamishiwa uwanja mwingine, huku mashabiki wa soka mkoani Kilimanjaro wakisubiri kwa hamu kuiona Yanga ikishuka dimbani kwenye ardhi yao.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Kaimu Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Yahya Abushekhe, amesema hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote kuhusu uwanja utakaotumika katika pambano hilo.

“Mpaka sasa mechi itachezwa hapo hapo Uwanja wa Ushirika, Moshi. Hakuna taarifa yoyote ya marekebisho ya uwanja huu kwa msimu huu,” amesema Abushekhe.

Kauli hiyo inamaanisha kuwa Yanga italazimika kusafiri hadi Moshi kukabiliana na Polisi Tanzania katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hasa kutokana na mwenendo wa timu hizo katika Ligi Kuu.

Yanga inafika kwenye pambano hilo ikiwa na kasi ya ushindi, baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 4-0, ushindi uliofuatia ule wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC Oktoba 27, 2026.

Ushindi huo wa pili mfululizo umekuja katika kipindi cha mabadiliko ya benchi la ufundi, baada ya kuondoka kwa Manqoba Mngqithi, huku Simo Dladla akiongoza timu kama kaimu kocha mkuu kabla ya ujio wa Fadlu Davids.

Katika mechi 10 ilizocheza, Yanga imeshinda nane, sare moja na kupoteza mmoja, ikiwa na pointi 25 katika nafasi ya pili, nyuma ya watani wao wa jadi Simba wenye pointi 30 katika msimamo wa ligi.

Kwa upande wa wenyeji, Polisi Tanzania inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 11, ikishinda nne, sare tatu na kupoteza nne. Timu hiyo imefunga mabao 13 na kuruhusu 12.

Polisi ilirejea kwenye ushindi Novemba Mosi baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 Ushirika, matokeo yaliyokuja baada ya kupoteza kwa Namungo kwa bao kama hilo Oktoba 29 wakiwa ugenini Lindi.

Hata hivyo, kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, amesema bado ana maeneo mawili ya kufanyia kazi kabla ya kukutana na Wananchi, ambayo ni umaliziaji wa nafasi za mabao na uimara wa safu ya ulinzi.

“Tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini bado hatujawa na kasi nzuri ya kuzitumia. Kwenye mpira kutengeneza nafasi pekee hakutoshi, tunatakiwa pia kuzifunga,” amesema Makata.

Naye Ofisa Habari na Mawasiliano wa Polisi Tanzania, Inspekta Frank Lukwaro, amesema kikosi hicho kimerejea kambini baada ya mapumziko ya siku tatu na kinaendelea na maandalizi kwa ajili ya pambano hilo.

Lukwaro amesema Uwanja wa Ushirika umeimarika na kuwahakikishia mashabiki kuwa Yanga haitapata mchezo rahisi itakapofika Moshi.

“Tunajua wenzetu wameleta mwalimu mpya, wamesema wanaleta El Nino, sasa sisi tutakuwa na kimbunga kwa ajili ya kufunika hiyo El Nino.

“Dar es Salaam Young Africans wanapokuja katika Uwanja wa Ushirika, wasitarajie mchekea. Mechi zetu na Yanga, hususan inapokuwa Ligi Kuu, hazijawahi kuwa nyepesi,” amesema Lukwaro.

Kabla ya pambano hilo la wakubwa, kikosi cha Polisi Tanzania chini ya miaka 20 pia kinatarajiwa kucheza Uwanja wa Ushirika Novemba 13 dhidi ya timu ya Simba SC.

Mara ya mwisho Polisi Tanzania na Yanga kukutana kwenye Uwanja wa Ushirika ilikuwa Februari 18, 2020, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na mambo kadhaa ya kukumbukwa.

Katika mchezo huo, Yanga iliyokuwa chini ya kocha Luc Eymael ilipata bao kupitia Tariq Seif Kiakala dakika ya 40, ambaye kwa sasa anaitumikia Polisi Tanzania, kabla ya wenyeji kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 70, wakati Polisi ikiwa chini ya kocha Malale Hamsini.

Hata hivyo, Polisi iliwahi kupata bao dakika ya 67 kupitia Matheo Anton, lakini mwamuzi akalikataa kwa madai kuwa mchezaji huyo alimchezea faulo beki wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, wakati akipiga kichwa.

Kwa hiyo, macho ya mashabiki wa soka Kilimanjaro sasa yanaelekezwa Novemba 20, siku ambayo Ushirika utakuwa mwenyeji wa pambano la Polisi Tanzania na Yanga, huku Wananchi wakisaka pointi za kuendelea kuisakama Simba kileleni na wenyeji wakitaka kutumia nguvu ya nyumbani kuwazuia.