Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Oura apiga mbili, Simba ikiendeleza moto Ligi Kuu

Muktasari:

  • Katika mchezo huo, Simba ilijikuta ikipambana kurejesha uongozi baada ya Namungo kugeuza matokeo na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, lakini Wekundu wa Msimbazi walionyesha tabia ya kutokata tamaa na hatimaye kuibuka na ushindi kupitia bao la dakika ya 89.

SIMBA SC imeendelea kuthibitisha ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2026-27 baada ya kuichapa Namungo FC mabao 3-2 katika mchezo mkali uliopigwa leo Novemba 2, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ushindi unaoifanya timu hiyo kuendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 30 baada ya kushinda michezo yote 10 iliyocheza.

Katika mchezo huo, Simba ilijikuta ikipambana kurejesha uongozi baada ya Namungo kugeuza matokeo na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, lakini Wekundu wa Msimbazi walionyesha tabia ya kutokata tamaa na hatimaye kuibuka na ushindi kupitia bao la dakika ya 89.

Shujaa wa Simba katika mchezo huo alikuwa mshambuliaji Anicet Oura aliyefunga mabao mawili, likiwamo bao la ushindi lililofungwa dakika ya 89, huku beki Rushine De Reuck akiisaidia timu hiyo kurejea mchezoni kwa bao la penalti dakika ya 80.

Kwa upande wa Namungo, Raymond Lulendi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioipa timu hiyo matumaini ya kupata matokeo mazuri baada ya kufunga mabao mawili ndani ya kipindi cha kwanza, lakini juhudi hizo hazikutosha kuizuia Simba kuondoka na pointi zote tatu.


MCHEZO ULIVYOKUWA

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na kuonyesha mapema kwamba ilikuwa na dhamira ya kuendelea na mwenendo wake mzuri wa ushindi katika ligi.

Dakika ya nne, Oura aliandika bao la kwanza kwa Simba akiunganisha kwa kichwa pasi ya Elie Mpanzu ambaye naye alipiga kichwa mpira wa kona uliochongwa na Nathaniel Chilambo. Bao hilo lilikuwa muhimu kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi kwa kuwa liliwapa utulivu na nafasi ya kuendelea kuutawala mchezo.

Hata hivyo, Namungo haikukubali kukaa kinyonge, ilianza kujipanga upya na kutafuta namna ya kurejea katika mchezo.

Dakika ya 36, juhudi za Namungo zilizaa matunda baada ya Lulendi kufanikiwa kuisawazishia timu hiyo na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Bao hilo liliamsha matumaini kwa Namungo na kuongeza ushindani wa mchezo, huku Simba ikilazimika kuendelea kuwa makini ili kuzuia mpinzani wake asipate nafasi nyingine ya kuadhibu safu yake ya ulinzi.

Namungo haikuishia hapo, kwani dakika ya 43, Lulendi alifunga bao la pili na kuifanya timu hiyo kugeuza matokeo kuwa 2-1. Mabao yote yaliyofungwa na Lulendi, yalitokana na pasi za Rashid Chambo.

Bao hilo liliifanya Namungo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja, hali iliyoiweka Simba katika nafasi ya kufanya kazi kubwa zaidi kipindi cha pili ili kuepuka kupoteza mchezo huo.

Namungo kwenda mapumziko ikiwa mbele, ilikuwa nafasi nzuri ya kujenga ushindi dhidi ya timu ambayo ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa ligi msimu huu, lakini kwa Simba, ilikuwa inahitaji kwenda vyumbani kujiuliza inarudi vipi kuepuka aibu ya kupoteza nyumbani.

Kipindi cha pili kilianza huku Simba ikiwa na jukumu la kutafuta bao la kusawazisha, wakati Namungo ikihitaji kulinda uongozi wake na ikiwezekana kuongeza bao lingine ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kupata ushindi.

Kadiri dakika zilivyokuwa zikisonga, Simba iliendelea kutafuta njia ya kuingia katika eneo la hatari la Namungo na kujaribu kurejesha matokeo katika hali ya sare.

Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 80, baada ya Rushine De Reuck kufunga kwa mkwaju wa penalti na kuifanya Simba kusawazisha matokeo kuwa 2-2. Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji Ibrahim Doumbia kuchezewa vibaya eneo la hatari na Rogers Gabriel.

Bao hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wekundu wa Msimbazi, ambao walikuwa wamejikuta nyuma kwa mabao 2-1 baada ya kipindi cha kwanza. Kusawazisha kulirejesha matumaini ya kupata ushindi na kuongeza msisimko katika dakika zilizobaki.

Namungo, ambayo ilikuwa imebakiza dakika chache kulinda uongozi wake, sasa ililazimika kuanza upya kutafuta namna ya kuzuia Simba isifunge bao lingine.

Hata hivyo, Simba haikuonyesha dalili za kuridhika na sare. Iliendelea kutafuta bao la ushindi huku mchezo ukiwa unaelekea ukingoni.

Dakika ya 89, Oura alifunga bao lake la pili na la tatu kwa Simba, akiipa timu hiyo ushindi wa mabao 3-2.

Bao hilo liliamsha furaha kwa upande wa Simba, kwani lilikuja katika wakati ambao timu hiyo ilikuwa imebakiza muda mchache wa kucheza, hivyo kuipa ushindi muhimu katika harakati zake za kuwania ubingwa.

Mwisho wa mchezo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2, ikiwa imeonyesha uwezo wa kupambana hadi dakika za mwisho licha ya kuwa nyuma kwa bao moja wakati wa mapumziko.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 30 baada ya kucheza michezo 10, ikiwa imeshinda yote na haijapata sare wala kupoteza. Imefunga mabao 23 na kuruhusu sita.

Matokeo hayo yanaifanya kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi, ikiwa na pengo la pointi tano dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 25, huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu na pointi 23.

Kwa upande wa Namungo, kipigo hicho kinaifanya kubaki na pointi 15 baada ya michezo 11, ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.