Nyota wa Coffee aiwinda rekodi ya Msudani
Muktasari:
- Abdelrahman aliyeshindwa kuonekana uwanjani msimu huu akiwa na kikosi cha wababe hao wa Sudan ikidaiwa ni majeruhi, msimu uliopita aliibuka Mfungaji Bora wa michuano akifunga mabao matano na kuiwezesha Al Hilal kumaliza ya tatu nyuma ya APR na Red Arrows iliyobeba ubingwa.
AMANUAL Admasu wa Coffee ya Ethiopia, leo atashuka uwanjani kukabiliana na Polisi Kenya, akiwa na akili ya kuinasa na hata kuipita rekodi ya mabao ya michuano ya Kombe la Kagame iliyowekwa msimu uliopita na Mohamed Abdelrahman wa Al Hilal ya Sudan.
Abdelrahman aliyeshindwa kuonekana uwanjani msimu huu akiwa na kikosi cha wababe hao wa Sudan ikidaiwa ni majeruhi, msimu uliopita aliibuka Mfungaji Bora wa michuano akifunga mabao matano na kuiwezesha Al Hilal kumaliza ya tatu nyuma ya APR na Red Arrows iliyobeba ubingwa.
Katika michuano ya msimu huu iliyoanza Septemba 2 na kutarajiwa kufikia tamati Jumatatu ijayo, Admasu ndiye kinara wa orodha wa wafungaji hadi sasa (kabla ya mechi za jana) akiwa na mabao matatu akifuatiwa na nyota mwingine wa Coffee, Zelalem Abate na William Togui wa APR wenye mabao mawili kila mmoja. Admasu pia ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat trick hadi sasa akifanya hivyo mbele ya Garde Cotes ya Djibouti.
Nyota wengine 18 wa klabu nyingine walikamilisha orodha ya wafungaji kila moja akifunga bao moja (kabla ya mechi za jana), wakati hatua ya makundi ya michuano hiyo ikifikia tamati kesho Jumanne kwa mechi za Kundi C.
Admasu anahitaji mabao mawili tu kupitia mechi tatu zilizosalia ikiwamo ya fainali, iwapo timu hiyo itafikia huko ili kuifikia rekodi hiyo ya Abdelrahman, kwani leo timu hiyo itacheza dhidi ya Polisi Kenya na kama itafuzu nusu atakuwa na nafasi ya kuongeza mabao na iwapo Coffee itafika fainali atakuwa na nafasi nyingine ya kuipiku rekodi hiyo ya mabao ya msimu uliopita.
Kabla ya mechi za jana jumla ya mechi 10 zilishapigwa na kufungwa mabao 25 ikiwa na maana ya wastani wa mabao 2.5, huku Wadjibouti wa Garde Cotes ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao mengi ikifungwa 10 katika mechi mbili, ikifuatiwa na Mlandege iliyotunguliwa matano, japo yenyewe imefunga mawili tofauti na Cotes ambayo haijafunga bao lolote.
Coffee ndiyo timu iliyofunga mabao mengi ikiwa na sita ikifuatiwa na Polisi Kenya yenye matano na timu hizo zinavaana leo na upo uwezekano wa idadi hiyo kuongezeka kwa timu zote, ilihali KMC na APR zikifuatia kila moja ikiwa na manne na zenyewe zitaumana kesho kumalisha ratiba.
Msimu uliopita jumla ya mabao 43 yalifungwa katika mechi 22, ikiwa na wastani wa 1.95, huku Al Hilal ikiwa vinara kwa kufunga mabao mengi (10) hadi ilipocheza mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Al Wadi ya Sudan na kushinda kwa penalti baada ya sare ya 1-1 ya dakika 90.