Ni kweli umemchukua brother Kibonde?
Muktasari:
Mbali na hilo, Kibonde pia alichangia maendeleo ya muziki kwa kupiga hewani nyimbo za wasanii mbalimbali pasipo ubaguzi wala kudai rushwa kama ambavyo wasanii wengi wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya watangazaji.
TASNIA ya michezo na burudani imepata pigo tena baada ya kifo cha ghafla cha Mdau wa Michezo na Mtangazaji, Ephraim Kibonde kuaga dunia katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza jana Alfajiri.
Mtangazaji huyo alifariki dunia baada ya kupelekwa hosptali kwa ajili ya matibabu ya presha alilolipata ghafla siku takriban nne zilizopita.
Kifo cha Kibonde ambaye pia alikuwa mshereheshaji na mwandishi wa habari za michezo na burudani, kimetokea ndani ya siku zisizozidi 10 tangu sekta ya habari, michezo na burudani impoteze mdau wake mkubwa Ruge Mutahaba.
Ikumbukwe Kibonde aliyekuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Clouds Media Group, ndiye alikuwa muongozaji/mshereheshaji wa mazishi ya Mutahaba ambaye alikuwa ni bosi wake kwenye kampuni hiyo akihudumu kama Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi iliyofanyika mkoani Kagera, Jumatatu mwanzoni mwa wiki hii.
Marehemu Kibonde alijijengea umaarufu kutokana na kipaji chake cha utangazaji ambacho kilimfanya kuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya michezo na burudani na kutamba katika uchambuzi wa mechi za soka, ushereheshaji kwenye matukio ya burudani na harusi, mashindano ya ngumi, matukio ya kimuziki na burudani na kadhalika.
Mbali na hilo, Kibonde pia alichangia maendeleo ya muziki kwa kupiga hewani nyimbo za wasanii mbalimbali pasipo ubaguzi wala kudai rushwa kama ambavyo wasanii wengi wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya watangazaji.
Maisha hayo ya Kibonde kwa kiasi kikubwa yaligusa kundi kubwa la watu hasa wadau wa burudani na michezo na ndio maana haijashangaza kuona wengi wakitumia kurasa zao za kijamii na vyombo vya habari kuelezea namna walivyopokea kwa masikitiko kifo cha mtangazaji huyo.
Dokta Harrison Mwakyembe-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
“Taarifa za kifo cha mtangazaji mahiri na maarufu nchini, Ephraim Kibonde wa Clouds, zimenishtua sana. Ni pigo la pili kubwa kutokea katika kipindi kifupi - si tu kwa Clouds Media peke yao, bali kwa tasnia nzima ya habari nchini.
“Wakati tunasubiri kutoka kwa madaktari kujua chanzo cha kifo chake na vilevile mipango ya mazishi yake, nitumie nafasi hii kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, Wana-Clouds Media na Wana-habari wote kwa ujumla, kwa msiba huu mkubwa. Bwana alitoa, sasa ametwaa; Jina la Bwana lihidimiwe!”
Haji Manara-Ofisa Habari wa Simba
Eeh Mungu ehhh!!
Ni kweli umemchukua brother Kibonde? Innalillah!! Kweli kabisa duniani sio mahali pa kudumu na sote tupo njiani.”
Elizabeth Michael ‘Lulu’-Mwigizaji
“Katika kila furaha na huzuni, katika kila tabu na mateso, katika kila mema na mabaya, wewe ni Mungu na utabaki kuwa Mungu. Hatuwezi kusema zaidi. Hatuwezi kusema pungufu. #RIP Kibonde”.
Nikk Wapili-Mwanamuziki
“Daah Jamani Jamani.....Pumzika Kwa amani. Ni kazi ya Mola. ..Daah.”
Profesa Jay-Mwanamuziki
“Daah hii habari imenishtua sana. R.I.P Kaka Ephraim Kibonde.”
Jerry Muro-Mkuu wa Wilaya Arumeru
“Sisi tulikupenda sana, ila Mungu amekupenda zaidi. Pumzika kwa amani kaka yetu na rafiki yetu Ephraime Kibonde, Mungu wa faraja anyooshe mkono wake awape faraja ya kweli familia ya Kibonde na ndugu zetu @cloudsfmtz @cloudstv.”