Ndemla aiwahi Simba Uturuki
HIVI unavyosoma habari hii ni kwamba kiungo matata wa Simba, Said Ndemla tayari yupo Uturuki akiiwahi kambi ya timu hiyo, baada ya kumaliza vuta nikuvute baina yake na mabosi wa Msimbazi juu ya kusaini mkataba mpya.
Ndemla amesaini mkataba wa miaka miwili na fasta akapandishwa ndege kuwahi kambi hiyo ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara..
Awali Ndemla licha ya kuwepo katika kikosi kilichocheza Kombe la Kagame alikuwa hajasaini mkataba kwani hawakufikia makubaliano jambo lililofanya ashindwe kujiunga na wenzake nchini Uturuki ambako wamepiga kambi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu.
Mabosi wa Simba baada ya kuona hivyo waliamua kumuweka chini kiungo huyo na kumuuliza mahitaji yake na ndipo wakafanikiwa kusaini dili hilo jioni ya Jumatano.
Baada ya Mwanaspoti kuzinyaka taarifa hizo lilimtafuta Mwanasheria wa mchezaji huyo, Kelvin Erick, alilithibitishia Mwanaspoti kwamba mteja wake amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.
“Kweli Ndemla ataendelea kuwa na Simba kwasababu amesaini mkataba wa miaka miwili, ishu yake ya kwenda Sweden tutaiangalia dirisha dogo au mwishoni mwa msimu kwanza lakini hapa ninavyoongea anajiandaa kupaa Uturuki (usiku wa juzi Jumatano),” alisema.
Naye Kiungo mpya wa Simba, Hassan Dilunga aliyekuwa akisubiri Simba imalizane na timu yake ya Mtibwa, naye yupo mbioni kuondoka kwenda Uturuki kwani viza yake imetoka.
Mtu mmoja wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti kwamba baadhi ya viongozi wa usajili wa klabu hiyo walihakikisha wanampa pesa za usajili Dilunga aende Uturuki mapema kwani viza ilikuwa imekatwa mapema.
“Dilunga jana (juzi Jumatano) alienda kuonana na viongozi wa Simba, lakini walimwambia aende Uturuki pesa watamuwekea kwasababu hawezi kuendelea kubaki nchini huku Viza ikiwa imekatwa, Dilunga alionekana kuwa mzito na jioni wakamuingizia pesa zake na alijiunga na wenzake kuondoka,”alisema.
Mwanaspoti lilimtafuta Meneja wa mchezaji huyo Zuberi Kambi, alikiri mchezaji wake kuondoka na fungu la mwisho la wachezaji wa Simba, baada ya kumalizana na viongozi wa klabu ya Simba.