Mziba awapa somo washambuliaji Yanga
Muktasari:
Yanga iliondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa na Zesco ya Zambia katika mchezo wa raundi ya pili na kushushwa kwenye Shirikisho.
WAKATI Yanga ikianzia nyumbani Oktoba 27 kuikabiri Pyramids ya Misri baada ya kushushwa Kombe la Shirikisho, mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Abeid Mziba amewapa mchongo washambuliaji wa timu hiyo.
Yanga itacheza na Pyramids nyumbani kabla ya kurudia Novemba 3 mjini Cairo mechi ambayo Yanga inahitaji ushindi ili kujihakikisha kutinga hatua ya makundi kwenye shirikisho.
Mziba amewapa mchongo washambuliaji wa Yanga kuelekea kwenye mechi hiyo akiwasisitiza kuutumia mchezo huo kutengeneza majina yao.
"Pyramids imeshikilia tiketi ya Yanga kimataifa, ni mechi ya kufa na kupona, lakini ndiyo ya kuwatengenezea majina washambuliaji wa timu hiyo.
"Tangu msimu umeanza, binafsi sijaona jambo ambalo wamelifanya la kuibeba timu, hivyo basi wajipange kwa Wamsri waonyeshe kiwango bora, wathibitishe uwezo wao kule," alisema akibainisha kuwa kwenye safu ya ulinzi hakuna tatizo japo nao wanapaswa kuongeza umakini.
Alisema wapinzani hao wa Yanga sio timu nyepesi, timu yake hiyo ya zamani isipofanya maandalizi ya kina isishangae kufungwa nyumbani na ugenini.