Mtibwa Sugar inakwamia hapa ubingwa Ligi Kuu
KIWANGO kilichoonyeshwa na Mtibwa Suagr, msimu wa 1999/2000 kilitoa taswira ya kuzipa changamoto Simba na Yanga kutochukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kirahisi, zikijua upinzani upo kutoka timu nyingine.
Wakati Mtibwa inalitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, Yanga ilikuwa ikilishikilia mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 96,97 na 98, hata hivyo wakata miwa hao hawakuweza kuiendeleza rekodi hiyo.
Ukiachana na kuchukua ubingwa mara moja tangu ipande mwaka 1988, imekuwa ikianza vizuri ligi ya VPL, lakini msimu unapokuwa unaelekea ukingoni timu hiyo imekuwa ikisuasua kupata matokeo.
Msimu ulioisha hali ilikuwa mbaya kwa timu hiyo, kwani imeponea chupuchupu kushuka daraja, baada ya kujikuta ikifanya hovyo mechi zake nyingi.
Mwanaspoti limefanya utafiti wa kwa nini Mtibwa Sugar, imeshindwa kukata kiu ya wadau wa soka nchini, walioitarajia kuona inakuwa kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa dhidi ya klabu kongwe Simba na Yanga kama ilivyotwaa taji hilo 1999/2000.
KUUZA WACHEZAJI
Mtibwa Sugar ni kama kituo cha soka, ikitengeneza wachezaji wazuri wamekuwa wakichukuliwa mfano misimu ya hivi karibuni Simba na Yanga zimekuwa zikiwachukua nyota wanaong’aa katika kikosi hicho.
Simba iliwachukua Shiza Kichuya, Ibrahim Mohamed, Mzamiri Yassin, Said Mohamed ‘Nduda’, Salim Mbonde, Ally Shomary, Julias Mrope, Hassan Kessy ambapo kabakia Mzamiru, wengine wameishatimkia timu nyingine.
Kwa upande wa Yanga katika usajili wa msimu huu, imemchukua Shomary Kibwana, miaka ya nyuma kidogo walichukuliwa Said Bahanuzi, Hussein Javu, Shaban Kado, Juma Abdul na Andrew Vicent ‘Dante’.
Kitendo cha kutokaa na wachezaji kwa muda mrefu, kinachangia kikosi hicho kushindwa kuwa imara kama matarajio ya wadau wao, wanaotamani kuona inazipa changamoto Simba na Yanga kunyakua taji la ligi ya VPL.
NI NYUMBANI KWA WACHEZAJI
Pamoja na kuwauza wachezaji wao, wanapokwama wanakokwenda wamekuwa wakirejea ndani ya kikosi hicho kama nyumbani, baadhi yao ni Javu, Henry Joseph, Kado, Nduda, Bahanuzi na Kessy, hata hivyo Joseph kaondoka kwa sasa nakujiunga na Ndanda, Bahanuzi yupo mtaani.
KOCHA MEXIME ATOA NENO
Mecky Maxime licha yakuinoa timu hiyo, pia aliichezea kipindi cha nyuma, anasema bado ana imani kubwa na timu hiyo, kuzipa changamoto Simba na Yanga, endapo upepo ukiwakalia vizuri kama ilivyokuwa kipindi amabacho walitwaa ubingwa.
“Zipo sababu mbili za kwanini Mtibwa Sugar imeshindwa kushindania taji la ligi ya VPL dhidi ya Simba na Yanga, kwanza upepo mbaya ambao unaweza kuikumba kila timu ikajikuta inafanya vibaya, tofauti na matarajio ya wengi,”anasema Mexime nakuongeza kuwa.
“Ukiachana na kukumbwa na upepo mbaya, kitendo cha timu hiyo kubomolewa kila mara kwa maana ya kuchukuliwa wachezaji wao, kinachangia kikosi kushindwa kuwa imara kwani kila muda kocha anakuwa anaanza upya kutengeneza kombinesheni ya wachezaji,”anasema.
KATWILA ASEMA LAKE
Kocha wa timu hiyo, Zuber Katwila anasema ngumu kufananisha timu ambazo zina wachezaji wazoefu na wao ambao wanapandisha vijana mara kwa mara ambao wanakuwa wanachipukia kwenye ligi hiyo.
“Ukiachana na hilo, Simba na Yanga zilikuwa zikisajili mastaa kutoka nje, viongozi wetu walikuwa na uwezo wakusajili kutoka kwao ndio maana ushindani ulikuwa wa hali ya juu, tofauti na sasa ambapo unaona nguvu zipo kwa ajili ya kukuza vipaji vya wachezaji ambao wapo chini wanatakiwa kwenda juu,”anasema.
Ukiachana na hilo, anasema wachezaji nao wakati mwingine wanakosa moyo wa uzalendo wakupambania timu yao, kuhakikisha inapata matokeo mazuri kama ilivyokuwa zamani ambapo licha yakupata kidogo, ila uwezo ulikuwa mkubwa zaidi.
BAYSER ATOA NENO
Timu hiyo imekuwa ikikamata nafasi za katikati, karibu misimu mingi iliyoshiriki ligi ya VPL, jambo linalotafsiriwa na baadhi ya wadau kuwa huenda wanauza mechi.
Fununu hizo zimepingwa vikali na mkurugenzi wa timu hiyo, Jamal Bayser kwamba haamini kama kuna wachezaji ambao hawataki kuonekana wanafanya vizuri ili kujitengenezea nafasi yakufika mbali, hasa miaka hii ambayo soka ni biashara inayolipa.
“Sidhani kama kuna kitu hicho, mchezaji auze mechi ili iweje. Hayo ni maneo ya watu na hata kama kingekuwepo na tabia hizo, tungeshajua na kuchukua hatua kali,”anasema.
WACHEZAJI NAO WAMETOA NENO
Straika wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Juma anasema kipindi cha sasa hakuna wachezaji ambao wanaoweza kupambania timu kuchukua ubingwa ama ufungaji bora.
“Tofauti na miaka yetu ambapo Simba na Yanga zilikuwa zinaihofia Mtibwa Sugar, mimi nimejiunga nayo baada ya kutoka kuchukua taji hilo msimu wa 1999/2000 nimeikuta timu ya moto,”anasema Juma nakuongeza kuwa.
“Hilo lilinifanya nitamani kufanya kitu, ndio maana nilichukua ufungaji bora mara mbili 2003 nilimaliza na mabao 18 na 2006 nilimaliza na mabao 25, lakini sasa hivi huoni jambo hilo, wachezaji wanaridhika hawajitumi kwa bidii,”anasema.
HENRY JOSEPH
Henry Joseph ni kiungo ambaye amekaa na timu hiyo, miaka mitano mfululizo, anasema changamoto inayofanya Mtibwa Sugar, ishindwe kuwa mshindani wa mataji ya ubingwa dhidi ya Simba na Yanga ni ushindani.
“Nimekaa na timu miaka mitano kwa mfululizo, nilichokiona kwa nini tunashindwa kutwaa mataji ya ubingwa ni ugumu wa ligi ndio maana Simba na Yanga unaona jinsi ambavyo zinashindana kusajili, lengo nikuwa na kikosi ambacho kitawafikisha kwenye malengo yao,”anasema kiungo huyo.