Mtanzania atoa wito soka la walemavu
Muktasari:
- Msimu wa 2023/2024 alicheza mechi 21 akifunga mabao nane na asisti 10, baada ya kuonyesha kiwango bora timu hiyo ikamuongezea mkataba wa mwaka mmoja akaitumikia tena msimu wa 2024/25 kisha msimu uliofuata akajiunga na Kahramanmaras.
KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Kahramanmaras inayoshiriki Ligi Kuu ya Walemavu Uturuki, Ramadhan Chomelo ametoa wito kwa wadau wa michezo nchini kuwekeza kwenye soka la walemavu ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuonyesha vipaji vyao.
Chomelo alibainisha michezo Tanzania inazidi kukua kwa kasi kubwa, lakini bado soka la walemavu halijapewa kipaumbele kinachostahili kulingana na uwezo na matokeo yanayopatikana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo amesema Uturuki anakocheza hivi sasa, kuna zaidi ya Watanzania sita wanaokipiga kwenye ligi hiyo na kuonyesha viwango vikubwa ambavyo vinaileta heshima kubwa taifa, ambao ni Hebron Tiger, Emmanuel Nakare wanaokipiga Sisli Yeditepe na wengineo.
“Ukweli ni kwamba michezo nyumbani inakuwa, lakini wadau wanapaswa kutazama na upande wa soka la walemavu. Mfano hapa Uturuki tuko Watanzania zaidi ya sita tunaocheza na sote tumetokea nyumbani,” amesema Chomelo.
Nyota huyo ameongeza kuwa kama wadau, makampuni na serikali watawekeza zaidi kwenye ligi ya ndani ya walemavu, itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza mchezo huo na kuibua vipaji vingine vingi vipya vinavyoweza kujikimu kimaisha kupitia soka.
Alifafanua kuwa uwepo wa Ligi Kuu imara ya Walemavu Tanzania sio tu utaimarisha timu ya taifa ya mchezo huo (Tembo Warriors), bali pia utafungua milango ya usajili wa kimataifa kwa wachezaji wengi wa Kitanzania kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Kabla ya kujiunga na timu hiyo Chomelo aliwahi kukipiga Konya Amputee na alisaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2022.
Ndani ya misimu miwili aliisaidia timu hiyo kufunga mabao saba na asisti 16 kwenye mechi 26 za ligi
Msimu wa 2023/2024 alicheza mechi 21 akifunga mabao nane na asisti 10, baada ya kuonyesha kiwango bora timu hiyo ikamuongezea mkataba wa mwaka mmoja akaitumikia tena msimu wa 2024/25 kisha msimu uliofuata akajiunga na Kahramanmaras.