Msako wa Simba Ligi Kuu
Muktasari:
- Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kileleni mwa msimamo kwa alama 27 baada ya kushinda mechi zote tisa ilizocheza, wakati Namungo inayoshika nafasi ya sita ikiwa na alama 15, inahitaji matokeo yatakayoiwezesha kusogea karibu na timu zinazoshindania nafasi za juu.
WAKATI Simba ikiendelea kutengeneza mazingira ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mchezo wake dhidi ya Namungo FC unaotarajiwa kupigwa leo Jumatatu, Novemba 2, 2026, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam saa 1:00 usiku, unatarajiwa kuwa miongoni mwa michezo yenye mvuto mkubwa kutokana na nafasi na malengo tofauti ya timu hizo.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kileleni mwa msimamo kwa alama 27 baada ya kushinda mechi zote tisa ilizocheza, wakati Namungo inayoshika nafasi ya sita ikiwa na alama 15, inahitaji matokeo yatakayoiwezesha kusogea karibu na timu zinazoshindania nafasi za juu.
Hata hivyo, mbali na tofauti ya pointi na nafasi kwenye msimamo, historia ya timu hizo inaipa Simba nafasi ya kuingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri zaidi, huku Namungo ikiwa na kazi kubwa ya kubadili rekodi yake dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Katika michezo 14 iliyopita ya mashindano mbalimbali tangu mwaka 2020, Simba imeshinda mara tisa na kutoka sare mara tano, huku Namungo ikiwa haijawahi kuifunga Simba.
Hata katika michezo 12 ya Ligi Kuu iliyopita, Simba imeshinda mara saba na kutoka sare mara tano, jambo linaloonyesha namna ambavyo imekuwa na wakati mgumu kuchezewa na Namungo katika historia ya timu hizo.
Lakini pamoja na rekodi hiyo, mchezo wa leo una umuhimu mkubwa kwa pande zote mbili kutokana na hesabu za msimamo wa ligi.
Simba ikishinda, itaifanya ifikishe pointi 30 baada ya mechi 10, ikiendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 tangu kuanza kwa msimu huu.
Matokeo hayo yatazidi kuipa nafasi ya kujitenga kileleni, kwani itakuwa na pengo la pointi saba dhidi ya Azam FC yenye alama 23, huku ikizidi kuikimbia Yanga ambapo kabla ya mechi ya jana, tofauti ya pointi ni tano.
Hiyo ina maana kwamba Simba haitakuwa ikipigania ushindi wa kawaida pekee, bali pia itaongeza nguvu katika mbio za kuwania ubingwa mapema, huku wapinzani wake wakilazimika kuendelea kufuatilia matokeo yake.
Kwa upande wa Namungo, ushindi utakuwa na thamani kubwa zaidi ya pointi tatu, kwani utaifanya ifikishe alama 18 na kupanda hadi nafasi ya nne.
Pia itakuwa fursa ya kihistoria kwa timu hiyo kutoka Lindi kuvunja mwiko wa muda mrefu wa kushindwa kuifunga Simba.
Sare nayo haitakuwa matokeo mabaya kwa Namungo, kwani itafikisha pointi 16 na kuendelea kujijengea nafasi nzuri katika sehemu ya juu ya msimamo.
Lakini sare kwa Simba, itakuwa pigo katika mwenendo wake wa ushindi mfululizo, ingawa itaendelea kubaki kileleni ikiwa na alama 28.
Kupoteza kwa Simba hakutaiondoa kileleni moja kwa moja, lakini kutatoa nafasi kwa Azam na Yanga kupunguza pengo la pointi.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema: "Kiukweli haitakuwa mechi rahisi, ukiangalia Namungo ni moja ya timu ngumu na timu nzuri sana kwenye ligi. Na hata ukiangalia mechi zao tatu za mwisho, wameweza kuwa na ushindi wa asilimia 100. Lakini sisi kama Simba tumejipanga, maandalizi yetu yanakwenda vizuri kabisa kuhakikisha tunapata alama zote tatu katika mchezo wa kesho (leo) pamoja na ugumu na uzuri waliokuwa nao Namungo."
Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema: "Tunajua tuna mchezo mgumu na mzito kesho (leo), tunacheza na timu nzuri yenye wachezaji wazuri, yenye kila kitu kizuri na ndio wanaoongoza ligi yetu. Kwa hiyo ni mechi ambayo ni muhimu sana kwetu sisi. Moja ya kanuni ya fair play ni kumuheshimu mpinzani wako, kwa hiyo si kwamba tuna hofu, ni kuheshimu. Kubwa ni kwamba tumejiandaa vizuri kucheza na timu nzuri ili mwisho wa yote tucheze vizuri na kupata matokeo yaliyokuwa mazuri.”
Akizungumzia kitendo cha Namungo kupoteza mechi nyingi dhidi ya Simba, Mgunda amesema: "Kupoteza mechi kwanza ni matokeo ya mchezo. Ukweli ni kwamba, toka nimekwenda Namungo hatujawahi kupata matokeo mazuri, hilo liko wazi na tunaelewa hivyo. Ndio maana nimekwambia kwamba kesho (leo) tunacheza na timu nzuri, tumelitambua hilo, tunalielewa hilo, na tumejiandaa vizuri kucheza nao ili mwisho wa yote tucheze vizuri na kupata matokeo yaliyokuwa mazuri."
Namungo itamkosa mshambuliaji wake, Gamba Matiko ambapo ripoti zinasema mechi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania alipata maumivu kidogo ya enka.
TRA UNITED VS FOUNTAIN GATE
Wakati macho mengi yakielekezwa kwenye pambano la Simba na Namungo ambalo litafunga siku, mchezo wa mapema saa 8:00 mchana, ni ule wa TRA United dhidi ya Fountain Gate, ambao utapigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Huu ni mchezo unaoweza kuwa na athari kubwa katika mapambano ya timu zinazotaka kujiepusha na hatari ya kushuka daraja, hasa Fountain Gate inayoshika mkia wa msimamo ikiwa na alama sita baada ya kucheza mechi 10.
TRA United yenyewe ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi tisa, hali inayoifanya nayo kuhitaji ushindi ili kujiondoa katika mazingira ya presha yanayoendelea kuzikabili timu za sehemu ya chini ya msimamo.
Takwimu zinaonyesha TRA imekuwa na mwanzo usioridhisha sana, ikiwa imeshinda mchezo mmoja, sare tano na kupoteza mara tatu, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu nane.
Fountain Gate ina hali ngumu zaidi baada ya kushinda mchezo mmoja, kutoka sare mara tatu na kupoteza mechi sita. Timu hiyo imefunga mabao matano na kuruhusu 14, jambo linaloonyesha changamoto iliyopo katika safu zake za ushambuliaji na ulinzi.
Pamoja na hali hizo, historia ya timu hizo inaonyesha Fountain Gate imekuwa na matokeo mazuri zaidi inapokutana na TRA United.
Katika michezo sita iliyopita ya Ligi Kuu, Fountain Gate imeshinda mara mbili, TRA United imeibuka na ushindi mmoja, huku michezo mitatu ikiisha kwa sare.
Hiyo inaifanya Fountain Gate kuingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kukutana na TRA, lakini hali ya sasa ya msimamo inamaanisha haitakuwa na nafasi ya kupoteza pointi kirahisi.
TRA ikishinda itafikisha alama 11 na kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kusogea kuelekea katikati ya msimamo, huku ikiimarisha nafasi yake dhidi ya timu zinazopambana kujinasua katika eneo la chini.
Fountain Gate ikipata ushindi utaifanya ifikishe pointi tisa na kuipa nafasi ya kujiondoa mkiani, huku ikifufua matumaini ya kurejea kwenye ushindani wa ligi.
Sare inaweza kuonekana kuwa matokeo yasiyotosha kwa Fountain Gate kutokana na mahitaji yake ya pointi, kwani itafikisha saba na kuendelea kubaki katika mazingira magumu.
Hata hivyo, kipigo kitakuwa na athari kubwa zaidi kwa timu hiyo, kwani itaendelea kuwa na alama sita na kuongeza presha katika harakati zake za kujiokoa.
MASHUJAA VS PAMBA JIJI
Katika mchezo mwingine wa leo saa 10:15 jioni utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Mashujaa FC itakuwa mwenyeji wa Pamba Jiji katika pambano ambalo kila upande unahitaji ushindi kwa sababu tofauti.
Mashujaa inayoshika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi tisa, inataka kutumia mchezo huo kujisogeza karibu na timu zinazoshindania nafasi za juu, wakati Pamba Jiji iliyopo nafasi ya 14 ikiwa na alama sita, inahitaji pointi ili kuondoka katika mazingira ya hatari.
Mashujaa imekuwa na matokeo ya kupanda na kushuka msimu huu, ikiwa imeshinda mechi nne na kupoteza tano bila kutoka sare, huku ikiwa imefunga mabao 10 na kuruhusu 15.
Kwa upande mwingine, Pamba Jiji imekuwa na changamoto ya kupata ushindi, ikiwa imefanikiwa kushinda mara moja, kutoka sare tatu na kupoteza michezo sita kati ya 10 iliyocheza.
Timu hiyo imefunga mabao 10 na kuruhusu 16, takwimu zinazoonyesha kuwa inahitaji kuongeza umakini katika safu zote ili kurejesha ushindani wake.
Historia ya timu hizo katika Ligi Kuu inaonyesha hakuna iliyofanikiwa kutawala nyingine kwa kiwango kikubwa.
Katika michezo minne iliyopita ya ligi hiyo, Mashujaa imeshinda mara moja, Pamba nayo imeshinda mara moja, huku mechi mbili zikiisha kwa sare.
Hata hivyo, rekodi ya jumla inayojumuisha michezo ya madaraja ya chini inaipa Pamba faida, kwani katika mechi 10 zilizopita imeshinda mara tano, Mashujaa mara tatu na sare zikiwa mbili.
Hiyo inaonyesha kuwa licha ya tofauti ya nafasi katika msimamo wa sasa, Pamba ina kumbukumbu ya ushindani mzuri inapokutana na Mashujaa.
Ushindi kwa Mashujaa utaifanya ifikishe pointi 15 na kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupanda kuelekea kundi la juu, huku ikiendelea kujiweka mbali na timu zinazopambana kujinasua mkiani.
Pamba nayo ikishinda itafikisha alama tisa na kuongeza nafasi ya kupanda katika msimamo, jambo ambalo litakuwa muhimu katika kurejesha matumaini ya kujiweka salama.
Sare itakuwa na faida fulani kwa Mashujaa, ambayo itafikisha pointi 13 na kusogea mbele zaidi, lakini kwa Pamba itakuwa matokeo yanayoacha maswali kuhusu uwezo wake wa kupata ushindi unaohitajika.