Makomandoo wa Simba walinda uwanja wa Kambarage
Muktasari:
Simba ni mabingwa watetezi wanaenda katika mchezo huo wakiwa wamevuna pointi mmoja katika michezo miwili iliyopita ugenini
Shinyanga. Mashabiki wa Simba walioongozana na timu yao mjini Shinyanga wamefikia Uwanja wa Kambarage kwa lengo la kuulinda uwanja kabla ya mechi dhidi ya Mwadui hapo kesho Jumapili.
Ni kawaida kwa mashabiki wa Simba kufika kwenye uwanja ambao timu yao itatumia kuweka ulinzi wakihofia mambo yanayodaiwa kuwa ni ushirikina.
Mashabiki hao walifika uwanjani hapo na kuzungukazunguka uwanjani wakionekana kuukagua uwanja huo utakaochezwa mechi yao kesho Jumapili.
Jana Ijumaa benchi la ufundi chini ya kocha wao Mbelgiji Patrick Aussems naye alifika uwanjani hapo wakati Mwadui wakiendelea na mazoezi.
Hata hivyo mashabiki hao hawakuwa tayari kuzungumzia lolote juu ya kile walichokifuata uwanja hapo wakati timu yao itafanya mazoezi yake leo saa 10 jioni.
Baada ya kumaliza mambo yao, mashabiki hao waliondoka uwanjani hapo.