Ligi Daraja ya Kwanza yahamishia vita kwa makocha
Muktasari:
Kocha Mkuu wa timu ya maafande wa JKT Oljoro, Emmanuel Massawe ameeleza kuwa mchezo wao dhidi ya Dodoma FC utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Jamuhuri, lazima wapate ushindi ili kufufua matumaini ya kwenda Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Arusha. Kocha Mkuu wa timu ya maafande wa JKT Oljoro, Emmanuel Massawe ameeleza kuwa mchezo wao dhidi ya Dodoma FC utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Jamuhuri, lazima wapate ushindi ili kufufua matumaini ya kwenda Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mchezo huo ambao utawakutanisha mwalimu na mwanafunzi wake wakati kocha Julio Kihwelu akiwa na timu ya Mwadui, Massawe ndio alikuwa kocha msaidizi wa timu hiyo na sasa wanakutana kila mmoja akitafuta heshima kwa timu yake kwa kuonyesha mbinu zao.
"Mchezo utakuwa mgumu kwani ni timu ambazo zote zinahitaji matokeo ya pointi tatu na siyo vinginevyo ili kuweka mazingira rafiki hasa kwa Oljoro iliyoshuka daraja mwaka 2014 kutoka Ligi Kuu Bara kabla ya kutupwa SDL kama adhabu," alisema Massawe.
Aliongeza kuwa anazifahamu mbinu na falsafa ya bosi wake huyo wa zamani hivyo tayari amewapa wachezaji mbinu na ametengeneza njia ya kwenda kummaliza Julio katika dimba la Jamhuri.
Endapo Oljoro itashinda mchezo huo atafikisha pointi 9 sawa na timu ya Dodoma huku akiiombea mabaya Alliance inayoongoza kundi hilo ikiwa pointi 10 ipoteza mchezo wao dhidi ya Transit Camp.