Kwa Kangwanda ni Chama, Musonda
Muktasari:
- Kangwanda aliyeifungia Yanga bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba uliofanyika Zanzibar, amesema tayari alikuwa akiifahamu klabu hiyo kabla ya kujiunga nayo kutokana na taarifa alizokuwa akizipata kupitia wachezaji hao.
NYOTA wa Yanga, Albert Kangwanda, amefichua namna Wazambia wenzake, Clatous Chama na Kennedy Musonda walivyochangia kufanya uamuzi wa kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania.
Kangwanda aliyeifungia Yanga bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba uliofanyika Zanzibar, amesema tayari alikuwa akiifahamu klabu hiyo kabla ya kujiunga nayo kutokana na taarifa alizokuwa akizipata kupitia wachezaji hao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kangwanda amesema mara baada ya kupata nafasi ya kujiunga na Yanga, hakusita kufanya mawasiliano na Wazambia hao ili kufahamu zaidi kuhusu timu hiyo na mazingira yake.
Amesema aliamini kujiunga na Yanga kungekuwa fursa muhimu ya kukuza kipaji chake na kupiga hatua nyingine katika soka, akieleza kuwa ubora wa kikosi na ushindani uliopo ndani ya klabu hiyo ni sehemu ya mambo yaliyomvutia.
Akizungumzia mchango wa wachezaji hao wawili, Kangwanda amesema kila mmoja alikuwa na nafasi yake na alitoa mchango wake kwa klabu, akieleza kuwa yeye anachotakiwa kufanya ni kujifunza kutoka kwa waliomtangulia na kuacha alama yake.
“Wote wawili walifanya sehemu yao na kutekeleza majukumu yao. Ni wachezaji tofauti, mmoja ni mshambuliaji na mwingine ni winga ambaye pia anaweza kucheza namba 10. Wote waliipa klabu mchango wao, hivyo ninachotakiwa ni kuanzia hapo na kuacha alama yangu,” amesema.
Kangwanda ambaye amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja katika Ligi Kuu Bara msimu huu, amesema ameridhishwa na maisha yake Tanzania, akieleza kuwa amepokelewa vizuri na watu wanaomzunguka na tayari anajisikia kuwa nyumbani.