Kocha Simba ni huyu hapa
Muktasari:
- Mabosi wa Simba wameamua kumshusha kimya kimya Kocha Patrick Aussems kutoka Ubelgiji ili kufanya mazungumzo ya kuchukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre waliyeachana naye mwezi uliopita baada ya kuinoa timu hiyo kwa miezi sita tu.
ACHANA na bao tamu la kichwa alilotupia kimiani Meddie Kagere wakati akiisaidia Simba kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida United katika mechi ya Kombe la Kagame, habari ya mjini ni ujio wa Kocha Mkuu Mpya wa timu hiyo.
Mabosi wa Simba wameamua kumshusha kimya kimya Kocha Patrick Aussems kutoka Ubelgiji ili kufanya mazungumzo ya kuchukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre waliyeachana naye mwezi uliopita baada ya kuinoa timu hiyo kwa miezi sita tu.
Mwanaspoti lililokuwa likimfuatilia kwa karibu, linafahamu Kocha huyo aliyewahi kuzitoa timu kadhaa zikiwamo za Ligi Kuu ya Ufaransa, ES Toyes AC na Stade de Reims pamoja na mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2012, AC Leopards ya Congo alitua nchini tangu Jumapili. Mbelgiji huyo aliyezaliwa Februari 6, 1965 na aliyecheza kama beki enzi zake za uchezaji akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 3, aliishuhudia Simba ikiinyuka APR ya Rwanda kwa mabao 2-1 huku straika mpya wa timu hiyo Meddie Kagere akitupia bao la ushindi kabla ya jana kuwepo tena Uwanja wa Taifa, straika huyo akifunga bao jingine. Habari zilizopenyezwa kwa Mwanaspoti ni kwamba, Kocha huyo yupo katika mazungumzo ya mwisho ya mabosi wa Simba kabla ya kupewa kazi ya kuinoa timu hiyo itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazoanza Desemba mwaka huu.
Awali ilielezwa kuwa, majina kadhaa ya makocha maarufu duniani akiwamo Johnathan ‘Johnny’ McKinstry wa Ireland ya Kaskazini aliyeahi kuinoa timu za taifa za Rwanda na Sierra Leone, waliomba kazi Msimbazi, lakini wasifu wa Patrick ukawavutia mabosi.
Inaelezwa mara ya Mbelgiji huyo aliyeanza kucheza soka miaka ya 1970 na kustaafu 1993 akipita klabu za RCS Vise, Standard Liege, KAA Gent, RFC Seraing zote za kwao Ubelgiji na ES Troyes AC ya Ufaransa kutua nchi alikabidhiwa Katibu Mkuu wa Simba, Dk Arnold Kashembe na kuitembelea kambi na mazoezi ya timu hiyo.
Chanzo chetu makini kinasema kuwa, aliomba kuiona timu ikicheza na kupelekwa Uwanja wa Taifa Jumatatu Simba ilipoifumua APR kisha jana akaenda tena akiwa na Dk Kashembe na kumshuhudia Kagere akifunga bao tamu la kichwa lililosawazishwa baadaye na Singida kupitia Danny Lyanga na kuzifanya timu hizo zitoke sare ya 1-1 katika Kagame.
Katika mchezo huo Simba ilianza kuandika bao dakika ya 16 kwa kichwa kabla ya Lyanga kusawazishwa kwa bao la kideoni akibinuka tiktak dakika ya 35’ na kufanya timu zote kumaliza mechi zao za Kundi C zikiwa na pointi saba kila moja, ila Simba ikifaidika na mabao mengi ya kufungwa dhidi ya wapinzani wao.
PATRICK NI NANI?
Patrick Winand Aussems alizaliwa, Februari 6, 1965 katika mji wa Moelingen, Ubelgiji na kuicheze RCS Vise kati ya 1974-81, klabu iliyokuja kufilisika mwaka 2014. Patrick alikipiga pia Standard Liege (1981-88), kisha kutua K.A.A Gent (1988-19), R.F.C Seraing (1989-90) na ES Troyes AC (1990-93).
Baada ya kustaafu mwaka 1993 kama Kocha Mchezaji wa Troyes inayoshikili Ligue1, alijitosa jumla kuwa kocha ndani ya klabu hiyo hadi 1995 alipotua Saint Lousienne ya Re Union.
Klabu nyingine alizofundisha ni Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C, Shenzhen Ruby, Chengdu Blades na kutua kwa waliokuwa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012 AC Léopards akimpokea Joseph Omog aliyekuwa ameletwa nchini kuinoa Azam FC. Alianza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2013-15 ambapo chini yake aliisaidia Leopards kubeba taji la Ligi Kuu ya Congo msimu wa 2014 bila upoteza mechi na iliruhusu kufungwa bao moja tu na kuifikisha timu hiyo katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho ikipoteza mbele ya Sewe Sports ya Ivory Coast hiyo ikiwa imeng’oka Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huo. Alipotoka AC Leopard alichukuliwa El Hilal ya Sudan kabla ya kutemwa miezi michache baada ya timu kupata matokeo mabaya na kutua timu ya taifa ya Nepal aliyoinoa kati ya 2015-16. Anasifika kwa soka la kushambulia sambamba na kujilinda na kama atamalizana na mabosi wa Simba iliyo chini ya Bilionea wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji ni wazi Wekundu wa Msimbazi watakimbiza sana, kwani Patrick ni bonge la kocha.