Kisa mkataba: Tayari Solskjaer apigwa zengwe Old Trafford
Muktasari:
Kumteua Solskjaer kuwa kocha wa kudumu ni kucheza kamari lakini tayari kuna klabu ziliwahi kufanya hivyo na kufanikiwa kama vile Barcelona na Real Madrid.
Manchester, England. Kwenye riziki hapakosi fitina. Ole Gunnar Solskjaer amepewa kazi ya kudumu pale Manchester United lakini kuna watu wameanza kupenyeza maneno ya chinichini kwamba United imefanya makosa kumpa kibarua cha kudumu staa wake huyo wa zamani.
Juzi Solskjaer alianza rasmi kuwa kocha wa kudumu wa United katika pambano dhidi ya Watford pale Old Trafford lakini staa wa zamani wa Tottenham na Timu ya Taifa ya England, Jermaine Jenas amedai United huenda imefanya makosa.
Jenas amedai United itajuta kutompa kazi ya kudumu Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino huku akidai rekodi za Solskjaer katika klabu zake mbili alizopita zinatia wasiwasi licha ya kuanza vema kazi yake United.
“Nilikuwa na furaha kuona Manchester United imemthibitisha Ole Gunnar Solskjaer kuwa kocha wake, lakini nadhani ingemteua Mauricio Pochettino. Ukiangalia kwa jumla na mambo ambayo inataka kufanikiwa, rekodi yake na hadhi yake klabuni vilimfanya awe mgombea wa nafasi hiyo,” anasema Jenas.
“Msinikariri vibaya. Solskjaer amefanya kazi nzuri sana, amerudisha historia ya klabu hiyo na alama ya klabu hiyo huku kiwango uwanjani kikiongezeka. Katika mbinu za uwanjani alifanya vizuri katika mechi kama vile dhidi ya Tottenham, dhidi ya Arsenal katika Kombe la FA na PSG katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Kwa vigezo hivi anastahili.”
“Hata hivyo, hakuwa chaguo la kwanza mwezi Desemba na nashangaa kwanini klabu haikuchukua maamuzi magumu kubakia katika mpango wake wa awali. Labda ilihofia huenda isimpate Pochettino. Ukiangalia rekodi za Solskjaer katika klabu za Cardiff na Molde usingemuweka katika orodha ya makocha wa juu,” aliongeza Jenas.
Jenas ambaye soka lake liliathiriwa na majeraha ya mara kwa mara aliongeza fitina zake kwa Solskjaer akidai mpaka sasa jina lake kama kocha haliwezi kuvutia majina makubwa kusaini Old Trafford tofauti na ilivyo kwa baadhi ya makocha wengine wakubwa England.
“Wakati United itakapokuwa inataka kuwasaini mchezaji mkubwa kama Neymar, nadhani hawatakuwa katika faida kubwa. Inabidi upambane na makocha kama Jurgen Klopp na Pep Guardiola. United kama klabu imekuwa kivutio kwa wachezaji wengi wakubwa lakini wachezaji wakubwa wanataka kucheza chini ya makocha wenye rekodi nzuri na mvuto,” alisema Jenas.
Wakati Jenas akisema hayo, mwandishi mkongwe wa Gazeti la Daily Mail, Oliver Holt amedai United itafanikiwa na Solskjaer endapo tu itaanza kujali zaidi matokeo ya uwanjani kuliko masuala la kifedha.
Holt amedai ni kweli kumteua Solskjaer kuwa kocha wa kudumu ni kucheza kamari lakini tayari kuna klabu ziliwahi kufanya hivyo na kufanikiwa kama vile Barcelona na Real Madrid.
“Watu wanaosema uteuzi wa Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wa kudumu wa Manchester United ni bahati nasibu wako sahihi. Naamini kila uteuzi wa kocha ni bahati nasibu. Pep Guardiola alikuwa kama bahati nasibu wakati Barcelona ilipomfanya kocha wa kwanza akitokea timu B. Ni kama Zinedine Zidane alipopewa kazi Santiago Bernabeu mara ya kwanza,” alisema Holt.
“Hakuna kitu kama uhakika katika suala la menejimenti. Uhakika walikuwa nao United wakati walipomteua Jose Mourinho. Alitazamiwa kuja kufanya mambo makubwa lakini angalia jinsi ambavyo aliigeuza klabu kuwa majanga,” aliongeza Holt.