Kisa kocha Orlando, Simba yaomba ulinzi Afrika Kusini
Muktasari:
- Katika nyakati hizi ambazo wanajiandaa na mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho Aprili 24, 2022 Simba imeiomba Serikali ya Tanzania na Serikali ya Afrika Kusini kuipatia ulinzi wakiwa safarini na wakiwa Afrika kusini.
KLABU ya soka ya Simba imesikitishwa na shutuma za uongo za kocha msaidizi wa timu ya Orlando Pirates Mandla Ncikazi alizozitoa baada ya mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika ambapo Orlando ilipoteza kwa bao moja kwa bila.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez timu hiyo imechukizwa na maneno kashfa yaliyotolewa na Kocha Ncikazi ambayo yanatanabaisha ukosefu wa taaluma na ukiukwaji wa maadili katika kazi yake ya ukocha.
Maneno ya Kocha huyo yanakinzana na ukweli ambao Simba tumekua tukiiushi kwa kutoa huduma bora kwa wageni wote wanaokuja kucheza nasi hapa Tanzania.
“Simba tulishangazwa na vitendo vya Orlando tangu kuwasili kwao Tanzania ambapo kama wenyeji tuliandaa mazingira yote rafiki kwa ajili yao ikiwemo Usafiri wa Basi kubwa, na gari ndogo lakini kwa sababu zao walikataa kutumia huduma tulizowaandalia” ilisema taarifa hiyo na kuongeza.
“Vilevile tuliwashauri kukaa Hoteli ya karibu na mji lakini kwa matakwa yao walichagua kukaa nje ya mji ambapo ni mbali na Uwanjani hali iliyopelekea kuchelewa mazoezi kwa zaidi ya saa moja lakini pamoja na hayo maofisa wa Uwanja wa Benjamini Mkapa waliwaruhusu kufanya mazoezi licha ya kuwa muda wakikanuni kwa timu kufanya mazoezi ulishamalizika”.
“Ajabu ni kwamba Kocha Ncikazi hayaoni yote haya na kuamua kuipaka matope klabu yetu ambayo tunajivunia ukarimu na uungwaana kwa wageni wetu wote”.
Katika kile kinachoonekana kuwa Orlando walidhamiria kufanya vurugu Tanzania siku ya mchezo yaani April 17 waligoma kutumia mlango rasmi wa kuingilia vyumba vya kubadilishia nguo na baadala yake wakatumia mlango wa kuingilia chumba cha mikutano ya Wanahabari ambapo kiuhalisia hii si tabia ya timu kubwa.
Kwa kadhia hizo Orlando wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa matendo yao.
Kihistoria Afrika kusini na Tanzania tuna uhusiano mzuri tangu enzi za ubaguzi wa rangi nchini kwao ambapo Tanzania ilikuwa sehemu ya kuwasaidia kupigania uhuru wa Nchi hiyo kupambana na udhalimu waliokua wanafanyiwa watu wa Afrika kusini.
“Lakini kashfa za Kocha Ncikazi zinaonesha wazi kuwa hajui lolote kuhusu uhusiano chanya uliopo baina ya pande hizi mbili”.
“Maneno ya Kocha Ncikazi ni hatari kwa maendeleo ya mpira wa miguu wa Afrika kwa sababu ameshindwa kuheshimu wapinzani wala hafuati misingi ya halisi ya mpira wa miguu (Fair play)”.
“Simba kwa uzoefu wetu tunaamini Kocha anaweza kujitetea kufuatia matokeo mabaya aliyopata ili kutafuta huruma ya mashabiki lakini Kocha Ncikazi amevuka mipaka na amedhamiria kuchafua taswira nzuri ya Simba na Tanzania kwa kutoa tuhuma za uongo”.
Kufuatia Kashfa hizo zilizotolewa na Kocha Ncikazi, klabu ya Simba itawasilisha malalamiko rasmi kwenda kwa Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na kupitia balozi za nchi zote mbili kuelezea yale yote yaliyoelezwa na Kocha huyo.
Katika nyakati hizi ambazo wanajiandaa na mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho Aprili 24, 2022 Simba imeiomba Serikali ya Tanzania na Serikali ya Afrika Kusini kuipatia ulinzi wakiwa safarini na wakiwa Afrika kusini.
“Vitisho visivyokua vya moja kwa moja vilivyotolewa na Kocha Ncikazi havipaswi kupuuzwa na ndio maana tunalazimika kuomba ulinzi katika kipindi chote tutakachokua nchini Afrika kusini Mpira ni mchezo wa kuheshimiana na Simba haitovumilia kuvunjiwa heshima na kila mmoja anapaswa kuwa makini na maneno yake iii kuepusha madhara kwa jamii yetu na tunaamini hii inaweza kuwa somo kwetu sote iii tusichupe mipaka ya kiugwana” ilisema taarifa hiyo.