Kina Aveva wakwama tena
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema inahitaji muda wa kulipitia jalada ili iweze kutoa uamuzi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwasilisha maombi ya kutaka Mahakama hiyo isitishe usikilizwajwaji wa shauri hilo.
Septemba 20, DPP aliwasilisha ombi hilo kutokana kusudio la kukata rufaa iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika rufaa hiyo DPP, anapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea Aveva na Kaburu mashtaka ya utakatishaji fedha na kuwapa masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema ameshindwa kutoa uamuzi leo kwa kuwa hakujipa muda wa kutosha hivyo analipitia upya jarada la kesi hiyo ili aweze kutoa maamuzi.
" Kutokana na kubanwa na majukumu nahitaji muda wa kutosha nalipitia upya jarada la shauri hili ili niwezi kutoa maamuzi," alisema Simba.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Oktoba 11 mwaka huu atakapokuja kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwaa na mashitaka tisa ambapo Septemba 19 mahakama hiyo iliwaondolea mashtaka mawili ya utakatishaji fedha kwakuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuyathibitisha.
Mahakama ilitoa masharti ya dhamana kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila watakaosaini dhamana ya Sh 30 milioni kila mmoja.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliawakuta na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha.