Kagere kiroho safi Yanga
Muktasari:
- Lakini kubwa ni kwamba yule Mfungaji Bora wa msimu wa pili mfululizo wa michuano ya SportPesa Super Cup, Meddie Kagere, amewaambia mabosi wa Yanga kuwa waache woga na waende mezani kuzungumza naye kwani yupo tayari kutua katika timu hiyo.
MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kufurahi kwa sasa, kwanza ni baada ya kusikia wanachama na mabosi wa klabu hiyo wameamua kuunda kikosi kazi cha kusaka fedha ili kuiwezesha klabu kusajili majembe ya maana Jangwani.
Lakini kubwa ni kwamba yule Mfungaji Bora wa msimu wa pili mfululizo wa michuano ya SportPesa Super Cup, Meddie Kagere, amewaambia mabosi wa Yanga kuwa waache woga na waende mezani kuzungumza naye kwani yupo tayari kutua katika timu hiyo.
Yanga imekuwa na nia ya kumnasa straika huyo aliyefunga mabao manne kwenye mechi tatu za Gor Mahia katika michuano hiyo na kutetea Kiatu cha Dhahabu alichokinyakua pia mwaka jana jijini Dar es Salaam na mabao yake matatu.
Straika huyo mzoefu aliyefunga bao moja wakati Gor Mahia ikiichapa Simba 2-0 katika mchezo wa fainali, alisema akili yake kubwa alikuwa ameweka kwenye michuano hiyo, lakini sasa yupo tayari kuanza kuzungumza kuhusu hatma yake.
Mzaliwa huyo wa Uganda anayeichezea timu ya taifa ya Rwanda, alisema anafahamu baadhi ya timu za Tanzania zinahitaji huduma yake kwa sasa hivyo kama wamedhamiria kweli waende mezani wakamalizane.
Alisema hana tatizo kuondoka Gor anayomaliza nayo mkataba mwezi ujao na kwenda kutafuta changamoto mpya endapo timu inayomhitaji itakuwa na ofa ya maana mezani.
“Sina woga na sijawahi kuogopa changamoto mpya. Niko tayari kwenda Tanzania ama sehemu nyingine yenye ofa nzuri,” alisema Kagere ambaye ametengeneza pacha hatari ya ushambuliaji kwenye kikosi cha Gor sambamba na Jacques Tuyisenge.
“Niliweka akili yangu kubwa kwenye mashindano haya. Sikutaka sana kuzungumza kuhusu hatma yangu ya baadaye. Nashukuru kwamba nimekuwa mfungaji bora, hii ina maana kubwa sana kwangu.
“Sasa kama kuna hizo timu za Tanzania ambazo zina nia ya kweli, zije mezani tuzungumze. Mkataba wangu na Gor Mahia unamalizika mwezi ujao, naweza kuondoka kama mchezaji huru kama Yanga wananitaka waje tu kwa sasa sina tatizo,” alisema.
Pamoja na staa huyo kuweka wazi kuwa yupo tayari kujiunga na Yanga ama klabu nyingine yoyote nchini, Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Dylan Kerr ameendelea kusisitiza kuwa nyota huyo bado yupo kwenye mipango yake.
Changamoto kubwa kwa Yanga na Azam kumnasa straika huyo ni mshahara wake kwa mwezi ambapo sasa Gor Mahia inamlipa dola 2,000 (Sh4.4 milioni) hivyo zinabidi kuongeza kwa kiwango kikubwa ili kumshawishi atue nchini.