Kagere, Bocco wapewa somo
Muktasari:
- Mgosi, ambaye kwa sasa ni Kocha wa Simba B, aliwataka mastraika wa timu hiyo, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi, kutuliza akili zao akisema mashabiki wanataka matokeo mazuri uwanjani na sio ukubwa wa majina.
MANAHODHA wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Nassor Masoud ‘Chollo’, wametoa angalizo kwa mastaa wa timu hiyo kuelekea mchezo wao dhidi ya Mbabane Swallow utakaopigwa keshokutwa Jumatano.
Wamesema kwa sasa Simba inahitaji kuvunja rekodi ya kufika mbali na siyo kiki za mchezaji mmoja mmoja ambazo zinaweza kusababisha uchoyo na ubinafsi, jambo ambalo halitakuwa na manufaa kwa timu.
Mgosi, ambaye kwa sasa ni Kocha wa Simba B, aliwataka mastraika wa timu hiyo, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi, kutuliza akili zao akisema mashabiki wanataka matokeo mazuri uwanjani na sio ukubwa wa majina.
Alimchambua Bocco na Kagere walichokifanya kwenye mechi dhidi ya Lipuli, akisema utulivu hafifu ndio chanzo cha kudondosha pointi mbili baada ya kuambulia sare.
“Okwi, Kagere na Bocco ni washambuliaji wenye uwezo wa hali ya juu, wanaweza kubadili matokeo muda wowote ila katika mechi dhidi ya Lipuli walikamia sana na hilo ni tatizo. Kama mtu huwezi kufanga basi toa pasi kwa aliyekuwa kwenye nafasi nzuri.
“Simba ya sasa inahitaji matokeo mazuri sio ukubwa wa majina uwanjani, mashabiki na wanachama wanatamani kuona rekodi za kimataifa zinavunjwa,” alisema.
Naye Chollo alisema anakiamini kikosi cha Simba kina wachezaji wenye uzoefu, lakini wanahitaji umakini zaidi na kuweka uzalendo mbele.
“Kuna mambo matatu hapa umakini, kujitambua na uzalendo, basi naamini Simba itafika mbali kimataifa na kuweka rekodi zake,” alisema.
BOCCO ANENA
Kwa upande wake, Bocco aliwataka mashabiki kuachana na matokeo ya Lipuli na kugeukia mechi hiyo ya kimataifa ili kupata ushindi.
“Tunahitaji kuyajenga yajayo na kuachana na matokeo yaliopita, ili kufanya vitu vya tofauti katika michuano ya CAF, tuna nafasi ya kufika mbali,” alisema.