Kagera yaachana na Kaseja, Kaze, Maxime watajwa kumrithi
Muktasari:
- Kaseja anaondoka kikosini humo akijivunia kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu Bara, huku akiwa kocha wa pili kuachana na waajiri wake msimu huu baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa TRA United, Ettiene Ndayiragije raia wa Burundi.
UONGOZI wa Kagera Sugar, umefikia makubaliano ya pande mbili kuachana na Kocha Mkuu, Juma Kaseja kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ya timu hiyo katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kagera Sugar inakuwa timu ya pili Ligi Kuu kuachana na kocha wake, ikifuata nyayo za TRA United iliyotangulia kutangaza kusitisha mkataba wa Ettiene Ndayiragije ambaye nafasi yake imechukuliwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Hatua hiyo inakuja baada ya Kagera kuanza vibaya msimu huu, ikiwa haijapata ushindi katika mechi sita ilizocheza, ikikusanya pointi mbili kupitia sare dhidi ya Singida Black Stars na Fountain Gate.
Katika mechi hizo, Kagera ilianza kwa kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba, kisha ikatoka sare ya 1-1 na Singida Black Stars, ikafungwa 6-2 na Geita Gold, ikapoteza kwa Mashujaa 2-1, ikapokea kipigo cha 2-0 dhidi ya Azam na mchezo wa mwisho ikatoka sare ya 1-1 na Fountain Gate.
Uamuzi huo ni kile alichotarajia kocha huyo na kipa wa zamani wa Yanga, Simba, Kagera Sugar na Taifa Stars, ambapo hivi karibuni aliliambia Mwanaspoti kuwa amejipanga kisaikolojia kwa lolote kutokana na matokeo yasiyoridhisha.
Wakati Kaseja akitimka hayo, inaelezwa kuwa hadi sasa uongozi unaendelea na mazungumzo ya mwisho na aliyekuwa Kocha wa zamani wa timu hiyo, Mecky Maxime ili kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho ambacho leo Jumanne kitarejea kambini kuendelea na mazoezi.
Pia Mwanaspoti limenasa taarifa kuwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo na Cedric Kaze kwa ajili ya kumpa jukumu la kuiongoza timu hiyo.
“Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na makocha wengine akiwemo Kaze. Kama mambo yatakamilika vizuri, anaweza kutangazwa kuwa kocha mpya wa Kagera wakati wowote.
"Kagera inataka kumpata kocha mpya haraka ili aanze kazi ya kuipa mwelekeo mpya timu ambayo kwa sasa ipo kwenye nafasi ya 15 ikiwa na pointi mbili baada ya mechi sita," kilisema chanzo.
Ofisa Habari wa Kagera Sugar, Stephen Julius, amethibitisha uwepo wa taarifa za kuachana na Kaseja akikiri ni mambo machache yamebaki kwa pande zote kumalizana, akieleza kuwa matarajio yao ni kuona timu ikifanya vizuri.
Kuhusu tetesi za warithi wake, amesema ni mapema kwakuwa mchakato unaendelea na ndani ya siku mbili watatangaza kocha mpya wa kuungana na timu kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Oktoba 8, 2026.
“Ni kweli tarifa zipo ila inakamilishwa taarifa za mkataba hadi jioni huenda tukamalizana, tatizo ni suala la matokeo, kujua nani anakuja ni mapema ila ndani ya siku mbili tutatangaza kwakuwa mchakato unaendelea.
“Matarajio yetu ni kufanya vizuri kuanzia mchezo ujao dhidi ya Mbeya City kwakuwa maandalizi yatakuwa mazuri, timu inatarajia kurejea kambini kesho (leo) Jumanne kuendelea na mazoezi,” alisema ofisa huyo.
Licha ya wawili hao kuachana, Kaseja atabaki na historia klabuni hapo baada ya kuirudisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu huu 2026-2027 kufuatia kushuka nayo 2024-2025.