Huu ndio utamu wa Ndondo Cup, asikwambie mtu
Mashabiki wa Mtoni City wakiwa wamepagawa kwa kusherekea katika mchezo wao dhidi ya wauza matairi kwenye mfululizo wa michuanoya sports Extra Ndondo Cup2016 inayoendelea jijini Dar es Salaam. PICHA NA OMAR FUNGO
Muktasari:
Lakini kama kawaida ya michuano hiyo hapakosekani viroja, juzi mashabiki wa Friends Rangers baada ya kuona plani A, imefeli walipocheza na Misosi ya Manzese, iliyowafunga bao 1-0 katika uwanja wao wa nyumba, wakasaka plani B na yenyewe ikayeyuka.
HATUA ya makundi ya michuano ya Sports Extra Ndondo Cup, inatarajia kumalizika Juni 26, mwaka huu na timu shiriki zinaendelea kupambana ili kutinga robo fainali.
Lakini kama kawaida ya michuano hiyo hapakosekani viroja, juzi mashabiki wa Friends Rangers baada ya kuona plani A, imefeli walipocheza na Misosi ya Manzese, iliyowafunga bao 1-0 katika uwanja wao wa nyumba, wakasaka plani B na yenyewe ikayeyuka.
Friends Rangers washangilia bao hewa
Baada ya Friends Rangers, kufungwa kipindi cha kwanza, cha pili walikuja na kasi ya kuhakikisha wanaufurahisha umati wa mashabiki wake waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Juhudi za nyota wao wanaokipiga Ligi ya VPL, wakiongozwa na Haruna Moshi ‘Boban na Nsa Job, zilipogonga mwamba kuzifuma nyavu, masela wakaona isiwe tabu wakachukua mpira na kuutumbukiza nyavuni kisha wakaingia uwanjani na kuanza kushangilia hali iliyomchanganya refa na kukaa kimya kwa dakika kama tatu.
Kipa wa Misosi FC, alianza kulalamika na kumwambia mwamuzi siyo bao kwani mpira ulipita pembeni kidogo masela wakajichanganya na kuutumbukiza nyavuni ndiyo ikawa salama yao, ingawa walimmaindi na kumwahidi kipigo akitoka hali iliyomtoa kwenye mudi ya mchezo.
Mshika kibendara aonja joto ya jiwe
Masela kweli sio watu, baada ya kuona jahazi la Friends linazama, masela walihamishia hasira zao kwa mshika kibendera aliyekataa bao lao ambalo mwamuzi wa kati alionekana kulikubali.
Kitendo hicho kiliwakera masela wakamvutia pembeni na kumchanganya kwenye kundi la watu wengi na kuanza kumpa za uso, polisi wakafanya jitihada zao na kumwokoa na kumkimbiza katikati ya dimba na kusimamisha mpira kwa dakika kadhaa.
Mabaunsa wa Friends, walijitahidi kuwazima masela wao huku wakiwasihi kwamba wamefunga waachane na hayo mambo, kisha mshika kibandera akaendelea na kazi yake kwa uoga, huku wakiwa wanamwambia maneno ya shombo asitembee kwa kujitanua wanaweza kukinukisha tena.
Mandata nao hawajambo
Mwanaspoti lilimfuata polisi mmoja kuzungumzia hali ya usalama wao kwa nyomi la watu kama wale ambao walijaa na Uwanja wa Makurumla na wengine wakalazimika kupanda juu ya nyumba za watu ili kuangalia kilichokuwa kinaendelea
Polisi.
“Dada unaona mkanda huu, unaweza kutandika watu wengi sasa sisi tulikuwa sita tungewashushia kipigo hadi wangeomba poo,” alijieleza, lakini wakati fujo zikiendelea walikuwa wapole na kuwaomba masela kwa ustaarabu huku wakisaidiana na mabaunsa wao.
Masela wa Misosi waomba ulinzi Polisi
Unaambiwa hii ilikuwa zaidi ya mtanange, masela wa Manzese walipoona hali si shwari walikimbilia kwa mapolisi na kuomba kuhakikishiwa hali ya usalama vinginevyo na wao watapita mtaa kwa mtaa kuwaliza.
Kanuti atia neno
Katika stori mbili tatu na mwandishi wa Mwanaspoti, Daudi Kanuti alipoulizwa juu ya usalama wa watu katika kundi kama lile alijibu kuwa: “Tunaogopa mapolisi kuja na mbwa uwanja kama huu maana anaweza kuwazuru mashabiki ila tunajitahidi hivyo hivyo hapa siyo kama Uwanja wa Bandari,”
Mwanaspoti lilimshuhudia mshika kibendera akiwa anaugulia maumivu ya usoni baada ya kumaliza game, alipouliza akajibu: “Hii ndiyo changamoto ya kazi dada,” alisema
Ratiba
Mechi za ndondo zitaendelea leo Alhamisi Black Six itaumana na Keko Machungwa Uwanja wa Airwing na Madiba itaumana na FC Kauzu Uwanja wa Bandari.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz