Prime
Hatimaye Doumbia afunguka, aahidi makubwa Msimbazi
LICHA ya kushindwa kufunga bao katika mechi mbili za kwanza za Kombe la CECAFA Kagame, mshambuliaji mpya wa Simba, Ibrahim Doumbia, amesema hana presha yoyote kwani anaamini ni suala la muda kabla hajaanza kuonyesha makali yake akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi.
Doumbia ni mmoja wa nyota wapya waliotua Msimbazi dirisha hili la usajili kuelekea msimu wa 2026-2027 akitokea Olympique Dcheira ya Mali ambako alikuwa mfungaji bora 2025-2026 kufuatia kufunga mabao 17 katika mechi 24 za ligi, huku akiongeza mabao manne kwenye Kombe la Mali na kumaliza msimu akiwa na jumla ya mabao 21 katika mashindano yote.
Akiwa huko alijijengea sifa ya mshambuliaji mwenye nguvu, kasi na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja katika safu ya ushambuliaji, jambo lililomfanya Simba kumchukua kwa lengo la kuongeza makali kuelekea msimu wa 2026-2027.
Kwa sasa mshambuliaji huyo ni sehemu ya kikosi cha Simba kilichoweka kambi Kigali, Rwanda, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya kupitia michuano ya CECAFA Kagame.
Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi bado hawajafumania nyavu baada ya kutoka suluhu dhidi ya Mogadishu City na Jamus SC katika michezo yao miwili ya Kundi B.
Licha ya hali hiyo, Doumbia alisema haoni sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa kikosi bado kiko katika hatua ya kujenga maelewano, akisisitiza kila siku inayopita inaongeza uelewano kati yake na wachezaji wenzake.
“Ni jambo la kawaida katika kipindi cha maandalizi, bado tunazoeana, lakini kila siku tunaelewana zaidi. Ninaamini muda si mrefu kila kitu kitakuwa sawa na nitakuwa tayari kuisaidia timu kufikia malengo yake,” alisema Doumbia.
Mshambuliaji huyo alisema tangu atue Simba amevutiwa na ubora wa kikosi alichokikuta, akieleza kuwa ushindani uliopo ndani ya timu utawasaidia wote kuongeza kiwango na kuifanya Simba kuwa na nguvu zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa.
“Nimekutana na kundi la wachezaji wenye ubora mkubwa, kila mmoja ana hamu ya kushinda na hilo linanipa imani kuwa tutakuwa na msimu mzuri. Kazi yetu ni kuendelea kufanya mazoezi na kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi,” alisema.
Mbali na hilo, Doumbia alisema ana hamu kubwa ya kukutana na mashabiki wa Simba, akieleza kuwa amesikia mengi kuhusu mapenzi yao kwa timu na anaamini atafanya kila linalowezekana kuwafurahisha kwa mabao na ushindi.
“Ninasubiri kwa hamu kucheza mbele ya mashabiki wa Simba. Nimeambiwa wanaipenda sana timu yao na ninaahidi nitafanya kila niwezalo kuwasaidia kufurahia msimu huu,” alisema.
Kocha wa Simba, Steve Barker, naye ameonyesha kuvutiwa na kile alichokiona kutoka kwa mshambuliaji huyo katika siku za mwanzo za maandalizi.
Kocha huyo alisema Doumbia tayari ameonyesha dalili za kuwa silaha muhimu kwenye safu ya ushambuliaji kutokana na uwezo wake wa kuwapita mabeki na kutengeneza hatari langoni.
“Nafikiri atawapa wakati mgumu mabeki wa timu nyingi, unaweza kuona uwezo wake wa kuwapita wapinzani, nimefurahishwa na kile nilichokiona kutoka kwake, ingawa bado tuna kazi kubwa ya kuboresha timu,” alisema Barker.
Doumbia katika mechi ya kwanza dhidi ya Mogadishu City, aliingia dakika ya 76, kisha dhidi ya Jamus akiingia mwanzoni mwa kipindi cha pili na kucheza kwa dakika 45.
Kwa sasa Simba inajiandaa na mchezo wake wa mwisho wa Kundi B dhidi ya Singida Black Stars, mechi ambayo ni ya lazima kushinda ili kuendelea kuwa na matumaini ya kutinga hatua ya nusu fainali ya CECAFA Kagame.
Endapo Wekundu hao wa Msimbazi watashinda, watasubiri matokeo ya mchezo mwingine kuona kama watafuzu kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya pili. Iwapo Simba itashindwa dhidi ya Singida Black Stars kesho itaagana na michuano hiyo.