Geita Gold FC matumaini kibao wakiwavaa Wasudan
Dar es Salaam. Matajiri wa madini, Klabu ya Geita Gold leo Jumapili, Septemba 11, 2022 wanarusha karata yao ya kwanza katika michuano ya kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa kuwavaa Hilal Alsahil ya Sudan Kaskazini.
Geita Gold FC ambao watakuwa ugenini katika mechi hiyo ya raundi ya mchujo wa kwanza mzunguko wa kwanza, mechi yao itaanza saa 2 katika uwanja wa Al-Hilal, jijini Khartoum.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari mwandamizi wa timu hiyo, Hemed Kivuyo matajiri hao wa dhahabu kutoka Geita, waliondoka nchini alfajiri ya Septemba 9, 2022 kwa ndege kupitia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kivuyo amesema timu hiyo imeondoka na msafara wa wachezaji 22, viongozi watano wakiwamo benchi la ufundi, Kocha Mkuu, Freddy Felix Minziro na kocha msaidizi Julius Wandiba.
“Timu imeondoka kwa morali kubwa na mwalimu ametuahidi kwamba atahakikisha anacheza mchezo wa kujihami zaidi ili wasifungwe na wakirejea nchini tumalize mchezo.
“Tunawashukuru TFF wametusaidiaa kukamilisha taratibu zote za covid, lakini pia tunawashukuru wafadhili GGML kwa kugharamia kambi ya timu pamoja na kuwalipia tiketi na safari nzima ya timu kuelekea Sudan,” amesema.
Aidha, mshambuliaji wao tegemeo, George Mpole hakusafiri na timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa na matatizo ya kiafya.
Geita Gold FC ambao wamefadhiliwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini Geita (GGML), kabla ya kuondoka walipiga kambi jijini Dar es Salaam na wanatarajiwa kurudiana na Wasudan hao siku nne baada ya mechi hiyo ya kwanza.
Mshindi wa mchezo huo kati ya Geita Gold na Hilal Alsahil atakutana na Pyramids FC ya nchini Misri kwenye hatua inayofuata.
Geita Gold ambao walipanda daraja msimu wa 2020/2021, wawanashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa.