Fomu za Urais Simba kaa la moto
Muktasari:
Gharama za fomu za Urais Simba ni Sh 500,000 wakati zile za ujumbe ni Sh300, 000
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kufungwa uchukuaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi Simba hadi leo hakuna mwanachama yeyote aliyejitokeza kuwania fomu za kuwania Urais.
Mwenyekiti wa Uchaguzi wa klabu hiyo, Boniface Lyamwike alisema hadi mchana wa leo ni mjumbe mmoja tu ameongezeka baada ya jana kuwa na idadi ya wajumbe sita.
Alisema pia katika akidi ya kugombea nafasi ya ujumbe katika klabu hiyo ambao inataka wajumbe watano wanne wanaume na mmoja mwanamke hadi sasa hakuna mwanamke hata mmoja aliyejitokeza kuchukua fomu.
"Nafikiri siku ya leo bado haijaisha hadi jioni huenda akajitokeza mwanachama ambaye anatamani kuwania nafasi ya Urais, siku mbili zilizobaki mbona ni nyingi sana wito wangu kwa wanachama ni kuwaomba kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kuhakikisha klabu yetu inafika mbali zaidi kimaendeleo," alisema.
Utoaji fomu za kuwania nafasi za ujumbe na urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu linatarajiwa kufungwa Jumatatu.