Dante aamua kuubeba mzigo Yanga
Muktasari:
Katika nafasi ambayo anacheza Juma Abdul (beki wa kulia) awali alikuwa anacheza na Hassan Kessy, lakini Kessy aliondoka kikosini hapo baada ya kushindwa kuafikiana katika suala zima la maslahi ya mkataba mpya hali iliyofanya kubaki Abdul pekee katika nafasi hiyo.
BEKI Andrew Vincent ‘Dante’ anayekipiga katika klabu ya Yanga, amewatuliza mashabiki wa timu yake kwamba ikitokea beki mwenzake Juma Abdul amepata tatizo katika msimu ujao anaweza kuziba pengo hilo bila wasiwasi.
Katika nafasi ambayo anacheza Juma Abdul (beki wa kulia) awali alikuwa anacheza na Hassan Kessy, lakini Kessy aliondoka kikosini hapo baada ya kushindwa kuafikiana katika suala zima la maslahi ya mkataba mpya hali iliyofanya kubaki Abdul pekee katika nafasi hiyo.
Dante aliliambia Mwanaspoti kwamba hakuna iwapo itatokea tatizo katika nafasi ya beki wa kulia basi anaweza kuziba pengo kwani nafasi hiyo alikuwa akiicheza mara kwa mara alipokuwa Mtibwa Sugar.
“Ninja anazidi kukomaa kadri siku zinavyosonga mbele na hilo ni jambo bora kwani itazidi kuongeza utulivu safu yetu ya ulinzi, ikitokea Juma kapata tatizo mimi nitacheza nafasi ile kwasababu nilipokuwa Mtibwa nilikuwa naicheza nafasi hiyo nakumbuka mechi dhidi ya Yanga, niliweza kupambana na Andrey Countinho vizuri kwahiyo wasiwe na wasiwasi,” alisema.
Akizungumzia kikosi chao katika msimu ujao, alisema watu wengi wamekuwa wakiwaangalia kwa uoga na kuona kama watakuwa wasindikizaji kitu ambacho ni tofauti.
“Unajua katika mashindano mengine kiukweli ile kwenda na kurudi nayo ilichangia kwasababu wachezaji tulikuwa hatupati kitu sawa, naamini kabisa tukikaa kwa pamoja katika maandalizi ya Ligi Kuu basi tutaonyesha kitu cha tofauti, hilo hata katika mechi ya marudiano limeonekana kwasababu maandalizi ya mechi ya kwanza na ya marudiano ni tofauti hata mchezo ulivyokuwa hapa nyumbani ulionekana,” alisema.
Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu kwamba timu hiyo itaenda kuweka kambi mkoani Morogoro kwaajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi 22 Agosti.
KESSY ASAINI MIAKA MIWILI
Kessy alitimkia Nkana Rangers ya Zambia ambapo jana amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo. Kessy alishindwa kusaini mkataba mpya na Yanga baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kimasilahi ambapo aliwapa masharti ya kumpa Sh 50 milioni pamoja na gari la thamani.
Yanga hawakuwa na kiasi hicho na kuacha kubembelezana naye na ndipo alipoamua kutimkia Zambia akiwa mchezaji huru.