BELLINGHAM : Mtoto wa straika ndondo anayenukia Man United
Muktasari:
Hii imewaacha mashabiki wa Man United wakiwa na maswali lukuki vichwani mwao, Je, Bellingham ni nani? Kwa nini timu yao inataka kutumia fedha nyingi namna hiyo kumsajili? Au ana nini cha ajabu? Majibu ya maswali hayo utayapata hapa;-
BIRMINGHAM ,ENGLAND . MASHABIKI wanamtaka Bruno Fernandes, lakini Manchester United inapambana sokoni kuhakikisha inamnasa kiungo kinda wa Birmingham City, Jude Bellingham, 16, tena kwa dau la Pauni 30 milioni.
Ndiyo hivyo, wakati mashabiki wakisikitishwa na kuyeyuka kwa dili la Fernandes, vigogo wa Old Trafford hawana habari na akili yao yote ipo kwa mtoto huyo wa miaka 16 tena anayecheza Ligi Daraja la Kwanza.
Hii imewaacha mashabiki wa Man United wakiwa na maswali lukuki vichwani mwao, Je, Bellingham ni nani? Kwa nini timu yao inataka kutumia fedha nyingi namna hiyo kumsajili? Au ana nini cha ajabu? Majibu ya maswali hayo utayapata hapa;-
Ni nani?
Bellingham alizaliwa Juni 29, 2003 katika Mji wa Stourbridge, West Midlands, England akiwa mtoto wa kwanza wa Mark Bellingham, Sajent wa polisi na straika wa zamani wa mechi za mchangani ‘ndondo’.
Alijiunga na Birmingham City akiwa na miaka minane na amekuwa na timu hiyo tangu wakati huo, mdogo wake Jobe naye yuko kwenye Akademi ya timu hiyo.
Alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha vijana chini ya miaka 23, wakati akiwa na umri wa miaka 15 katika mchezo dhidi ya wenzao wa Nottingham Forest, Oktoba 2018, aliingia uwanjani katika dakika ya 60 na kufunga bao pekee la pambano hilo katika dakika ya 87.
Kufikia Machi 2019 alikuwa ameshafunga mabao matatu katika mechi 10, hivyo alipandishwa kikosi cha kwanza kwa ajili ya pambano dhidi ya West Brom, hii ilikuwa Machi 29 2019.
Julai 2019, alisaini mkataba wa udhamini na Birmingham City uliomuingizia kiasi cha Pauni 145 kwa wiki na alifanikiwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi za kujiandaa na msimu mpya nchini Ureno.
Kuelekea kwenye msimu wa 2019/20 alipewa jezi namba 22 na Agosti 6 mwaka jana aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza mechi katika kikosi cha Birmingham akiwa na miaka 16 na siku 38, akivunja rekodi ya miaka 16 na siku 139 iliyowekwa na Trevor Francis mwaka 1970.
Wiki mbili baadaye Agosti 31, aliingia zikiwa zimesalia dakika 30 mchezo kuisha kuchukua nafasi ya Jefferson Montero na kufunga bao la ushindi wakati Birmingham City ikitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stoke 2-1. Kwa bao hilo aliandika rekodi nyingine ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga bao kwenye kikosi cha timu hiyo.
Wiki mbili baadaye alianza kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Charlton na kufunga bao pekee la ushindi kwenye ushindi wa bao 1-0 na kushinda tuzo ya Mchezaji Mdogo wa Ligi Daraja la Kwanza wa Mwezi Novemba 2019.
Kwa ujumlaBellinhgam amecheza mechi 23 za Ligi Daraja la Kwanza akifunga mabao matatu na kupiga pasi moja ya bao akiwa na kikosi cha Birmingham.
Aina ya uchezaji
Bellingham ni kiungo mpambanaji, anayejua kukaba, kumiliki mpira na muda wote hupenda kuanzisha mashambulizi na kulisha washambuliaji kwa kupiga pasi za kupenyeza.
Kitu kingine kikubwa kuhusu kinda huyu ni kuwa licha ya kuwa na umri mdogo ila ni mtulivu sana akiwa mpira na hata anapokuwa mbele ya goli hana papara.
Lakini, kiungo huyo pia anaweza kucheza kama kiungo wa kushoto na kulia pia, kinachomfanya aweze kucheza kama kiungo wa pembeni ni kasi yake na uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga ambazo huwaacha wapinzani wakiwa hawana la kufanya.
Kama unatafuta viungo wa Ligi Kuu England ambao Bellingham anafanana nao kiuchezaji basi nenda kawatazame Georginio Wijnaldum, Abdoulaye Doucoure na John McGinn.
Kali kuliko
Jude ni mtoto wa kwanza wa Mark Bellingham, ambaye kwa sasa ni Sajenti wa polisi, lakini ujana wake alikuwa straika hatari wa timu za mtaani.
Unaambiwa katika ujana wake Mark alikuwa hatari sana anadaiwa kuchezea jumla ya timu 15 za mtaani na kufunga jumla ya mabao 700 katika mechi 850 za kitaa ‘ndondo’.
Soka la kimataifa
Bellingham hadi sasa amechezea Timu za Taifa za Vijana za England chini ya miaka 15, 16 na 17 huku kwa nyakati tofauti akivaa kitambaa cha unahodha katika vikosi hivyo.