Baada ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania, Simba yalia na umri U-20
Muktasari:
- Ombi hilo amelitoa baada ya Simba U-20 kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania U-20 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa leo Ijumaa, Novemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kocha msaidizi wa Simba U-20, Jeremia Gerald, ameliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuongeza makali katika uthibitishaji wa umri wa wachezaji wanaoshiriki Ligi ya Vijana chini ya miaka 20.
Ombi hilo amelitoa baada ya Simba U-20 kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania U-20 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa leo Ijumaa, Novemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Gerald amesema pamoja na kuipongeza TFF kwa kuandaa mashindano hayo, bado kuna umuhimu wa kuweka vigezo na mifumo madhubuti zaidi ya kuhakikisha wachezaji wanaoshiriki wana umri unaostahili.
“Tunashukuru TFF kwa nafasi wanazotoa kupitia ligi za vijana, lakini bado tunaomba waendelee kuongeza vikwazo vigumu ili tupate uhalisia kabisa wa umri sahihi katika ligi yetu ya U-20,” amesema Gerald.
Gerald amesema Simba iliingia kipindi cha pili ikiwa na mpango wa kuongeza mabao baada ya kupata bao la kuongoza, lakini mabadiliko waliyoyafanya hayakuzaa matunda yaliyotarajiwa.
Amesema walitaka kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ili kupata bao la pili na la tatu, lakini Polisi ilitumia vizuri makosa yao na kugeuza matokeo.
“Goli moja si goli, tulitamani kuongeza la pili na la tatu. Kwa hiyo ilibidi tufanye mabadiliko ili kuongeza nguvu mbele, lakini haikuwa bahati yetu,” amesema.
Kwa upande wa Polisi Tanzania, kocha wake Aloyce Mwanyilu, amesema ushindi huo umetokana na mabadiliko ya mbinu aliyoyafanya kipindi cha pili baada ya kubaini maeneo ambayo Simba ilikuwa ikifanya makosa.
Mwanyilu amesema walikuwa na muda mfupi wa maandalizi, takribani wiki moja, hivyo waliingia uwanjani kwa tahadhari huku wakijaribu kwanza kuifahamu Simba.
Amesema walibaini wapinzani wao walikuwa na nguvu kupitia pembeni, lakini baada ya dakika 55 walibaini walikuwa wakifanya makosa walipowekewa presha.
“Pamoja na kwamba tulikuwa chini, tukiwashambulia kwa kasi kidogo walikuwa wanafanya makosa. Kwa hiyo kipindi cha pili tukaamua kuongeza straika ili tuwashambulie zaidi. Baada ya kuongeza straika tuliona wanafanya makosa zaidi, ndiyo ikapelekea kupata goli la kwanza na la pili,” amesema.
Mwanyilu amesema ushindi huo umewaongezea morali na kujiamini wachezaji wake kuelekea michezo inayofuata, huku akiahidi kurekebisha upungufu uliojitokeza.
Aidha, ameipongeza TFF kwa mfumo wa mashindano hayo akisema unawapa vijana nafasi ya kucheza mechi nyingi katika hatua ya makundi kupitia michezo ya nyumbani na ugenini.
Amesema mfumo huo unasaidia wachezaji kupata uzoefu na kuonyesha vipaji vyao, huku timu nane zikitarajiwa kuingia hatua ya robo fainali.