Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AWESU AWESU : Kwa Simba,Yanga dau tu unaambiwa

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya mahojiano na kiungo huyo aliyefunguka mambo mbalimbali kuhusu soka, huku akidai kucheza amerithi kutoka kwa wazazi na ndio maana hakupata changamoto ya kukatazwa kujihusisha nalo.

KWA asilimia kubwa ya mastaa wanaocheza soka la kulipwa huko Ulaya wamekuzwa kwenye maadili ya soka, na ni kutokana na ushirikiano wa wazazi wao kuwasaidia baada ya kuonyesha vipaji.Hilo linafanyika majuu na ndio maana vipaji vingi vinazaliwa na kukuzwa kwa kufuata maadili hayo.

Kwa upande wa Afrika ni wazazi wachache wanaamini katika soka kutokana na wengi kuwa na imani kuwa elimu ya darasani ndio kila kitu kwenye maisha. Basi unaambiwa kiungo wa Kagera Sugar, Awesu Awesu ni mmoja wa Watanzania wachache waliopewa ushirikiano na wazazi baada ya kubaini kuwa ana kipaji cha soka.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na kiungo huyo aliyefunguka mambo mbalimbali kuhusu soka, huku akidai kucheza amerithi kutoka kwa wazazi na ndio maana hakupata changamoto ya kukatazwa kujihusisha nalo.

NAMBA ZOTE HADI KIPA

Kwenye soka ni nadra kukuta mchezaji wa nafasi zote uwanjani kwani wengi wao wanaweza kucheza nafasi tatu au nne. Mfano ni mkongwe Erasto Nyoni anayeweza kucheza nafasi zote za beki na kiungo, lakini Awesu anacheza zote hadi ile ya golikipa. “Hakuna mwalimu ambaye naweza nikasema kanibadilisha namba uwanjani, nacheza nafasi zote kuanzia kipa hadi mshambuliaji, hili nimefundishwa tangu nikiwa na umri mdogo,” anasema.

“Katika nafasi zote nimeshawahi kupangwa japo wengi wananitambua kwa nafasi ya kiungo ambayo nimeitumikia kwa muda mrefu. Kwa sasa huwezi kuamini nachezeshwa nafasi ya winga na ndio iliyonifanya nikafunga mabao matano nikiwa Kagera Sugar.”

ALIANZA NA LAKI AKIWA NA MIAKA 10

Pamoja na kuonyesha jitihada za kupambana zaidi na soka, huku shule akiipa kisogo, kiungo huyo wa Kagera Sugar anasema fedha zake za kwanza kumiliki kwenye soka hana hana hata kitu kimoja alichonunua kama kumbukumbu kwani zilikuwa ni ndogo na alizitumia kula vitu mbalimbali.

“Nakumbuka timu yangu ya kwanza nikiwa na umri mdogo, nilifuatwa na Arizona ambao walinipa laki moja kama fedha ya kutaka kuichezea timu hiyo, sikuwashirikisha wazazi wangu, nilizitumia mwenyewe na rafiki zangu, hilo wala halikuwakatisha tamaa wazazi zaidi walitaka niendelee kupambana.”

SOKA BADO LINAMDAI

Hakuna mafanikio yenye mwisho kwani kila mwanadamu akipata kile alichokiomba kesho tena ataomba zaidi, hivyo ndivyo ilivyomkuta Awesu ambaye alikuwa anatamani kucheza Ligi Kuu Bara akitokea Zanzibar, na sasa hilo amefanikiwa, lakini anasema kuwa bado analidai soka na pia linamdai.

“Ndio kwanza naanza kupata mafanikio japo kidogo namshukuru Mungu, ila siwezi kukubali kuwa tayari limeshanilipa. Kuna vitu vingi sijavikamilisha, nalidai japo hata soka lenyewe linanidai kutokana na kutofanikiwa kufanya kitu kikubwa kwenye mchezo huo,” anasema.

MKONO ULILETA BALAA

Hakuna kazi inayokosa changamoto, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kila mwanadamu mwenye uchu wa mafanikio kuanza kwa changamoto na ndipo hutimiza ndoto yake.

Awesu, nyota kiraka wa Kagera Sugar amefunguka kuwa pamoja na kupenda soka kuna mwaka alitamani kuachana nalo baada ya kuvunjika mkono akiwa uwanjani.

“Nakumbuka nikiwa Skuli ya Mwembemakumbi (Zanzibar) nacheza na wenzangu nilivunjika mkono ambao uliniweka nje ya soka muda mrefu kitu ambacho kilinifanya nisipende tena, lakini namshukuru baba yangu, mzee Awesu hakutaka kukubali hilo, alinirudisha tena uwanjani hadi sasa nacheza.”

HUMWAMBII KITU KWA STEPHEN CURRY

Kila mwanadamu ana starehe yake mbali na kile anachokifanya mfano unaweza ukawa mwalimu na bado ukapenda kufuatilia soka au muziki, basi unaambiwa Awesu akiwa mapumziko huwa hakai mbali kufuatilia masuala ya mpira wa kikapu.

“Nikitulia zangu nyumbani basi vitu vyangu vikubwa ambavyo navifanya havihusiani kabisa na soka kwa sababu ni mapumziko, hivyo nabadilisha mazingira kwa kufanya vitu tofauti, napendelea kucheza gemu na kuangalia mpira wa kikapu,” anasema.

“Ni mpenzi mkubwa wa Curry ambaye anakipiga katika timu ya Golden State Warriors, huniambii kitu kuhusu hiyo timu naifuatilia sana na navutiwa zaidi na mchezaji wao huyo ambaye muda mwingine huwa ananishawishi kuupenda huo mchezo kwa kutamani kucheza siku moja.”

MAKUBWA UWANJANI

“Sikuwahi kutokewa na hali kama hiyo kwa sababu kocha amekuwa akinitumia katika nafasi mbalimbali uwanjani, jambo ambalo linasababisha nisikutane na hali ngumu kwenye mchezo wowote ule ambao tumecheza hadi sasa,” anasema.

“Halafu kusumbuliwa na mchezaji mwenzako uwanjani ni kukosa umakini au nidhamu, wote tunacheza nafasi moja hivyo kila mmoja anakuwa na mbinu zake za kumtoka mpinzani, kusumbuliwa sikupi nafasi zaidi najitahidi kupambana kuhakikisha naweza kuisaidia timu kupata matokeo.”

SESEME SIO WA HAPA BASI TU

Awesu anamtaja Abdallah Seseme kama moja wa viungo bora nchini.

“Nimecheza misimu minne au mitano kama sikosei kwenye soka la Tanzania Bara na nimefanikiwa kukutana na timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu. Kwa michezo niliyocheza na timu hizo ni mchezaji mmoja tu ninayemwelewa na namuona mbali kama atapata nafasi ya kutoka,” anasema

“Hakuna zaidi ya kiungo mwenzagu Abdallah Seseme, nampenda sana na napenda kucheza naye kwa sababu tumecheza pamoja muda mrefu, anajua nataka nini na mimi najua anataka nini tukiwa uwanjani, nafasi nyingi za kufunga nilizozipata nimetengenezewa na mchezaji huyo nikiwa Mwadui FC sasa nipo Kagera Sugar lakini bado namuelewa.”

SIMBA, YANGA DAU TU

Kwa wachezaji wa hapa nchini mara nyingi ndoto zao kubwa ni kuona wanacheza moja ya timu kati ya Simba na Yanga na wakifanikiwa kupita hapo ndipo wanafungua milango ya kutoka nje kwenda kucheza soka la kulipwa. Awesu anasema: “Ikitokea hali kama hiyo kwangu nitasaini timu yoyote kati ya hizo (Simba na Simba), muhimu kwamba nipate nafasi ya kucheza, na kama ikitokea timu nyingine zaidi ya hizo basi nitasaini tu, kitu kingine muhimu ni fedha kwani naendesha maisha yangu kwa kucheza soka.”

“Sijawahi kuwa na mapenzi na timu yoyote kwamba naweza kuchagua kuichezea, naangalia maslahi, timu itakayonilipa vizuri hata ikiwa Daraja la Kwanza naichezea.”