Usajili Simba kama Ulaya tu
SIMBA kweli imeamua. Achana na matokeo ya mchezo wao wa jana wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, uliopigwa jijini Mwanza, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba chini ya Mwenyekiti wao Mohammed ‘MO’ Dewji, wamekuja na mpango mmoja kamambe juu ya usajili ya kikosi chao.
Wajumbe hao kwa kauli moja wameamua kwamba usajili ya msimu ujao kwa kikosi chao utafanywa kama unavyofanyika katika klabu nyingi barani Ulaya ama klabu zilizoendelea kisoka Afrika, lengo likiwa ni kutengeneza Simba mpya, kali na itakayoleta ushindani ndani na katika mechi za kimataifa.
Kikao hicho kilichofanyika kwa siri kubwa, miongoni mwa ajenda iliyojadiliwa kwa muda mrefu ni aina mpya ya majembe mapya ambayo Simba wataanza kuyashusha mara baada ya msimu kumalizika ili kuongeza makali ya timu ifanye vizuri katika mechi za kimataifa na mashindano ya ndani.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori ndiye aliyefichua mchongo mzima kuwa Wajumbe wa Bodi walipendekeza sera mpya ya usajili ambayo wameichukua kutoka katika timu kubwa Ulaya na Afrika ambazo zimeendelea katika maeneo mbalimbali.
Magori alisema sera hiyo mpya ambayo wajumbe muda si mrefu wataipitisha katika kufanya usajili wa majembe mapya ya msimu ujao, itakuwa na mambo sita, ambayo kati ya hayo wanaweza kuyatumia yote au machache ili kupata wachezaji watakaoiongeza nguvu timu na si kufanya usajili ilimradi.
“Jambo la kwanza katika sera mpya ya usajili inatakiwa kuangaliwa kama aina ya usajili inafanana na malengo ya timu, baada ya hapo tunaangalia bajeti ya klabu katika usajili ni kiasi gani na tunaweza kuwapata wachezaji wa aina gani kulingana na pesa yetu,” alisema.
“Tumefuatilia usajili wa klabu nyingine Afrika na kuona ni lazima uongozi utenge bajeti ya usajili ambayo inakuwa wazi kila mtu anaifahamu na hata usajili ambao unafanywa unalingana na kiasi cha pesa ambacho klabu inacho,” alisema Magori.
“Suala la nne ambalo lipo katika sera hiyo mpya msimu huu tutaangalia upungufu uliojitokeza msimu uliopita unaendana na usajili wa wachezaji wapya ambao tunataka kuufanya? Hii ni kwa sababu hatutakuwa tena na usajili ule wa kugombania mchezaji,” alisema.
Magori alifunguka la tano kuwa sera mpya itaangalia usajili wa mchezaji mpya ana umri gani na nafasi yake ambayo anacheza na umri aliokuwa nao vinaendana na kama atakuwa na umri mzuri kulingana na nafasi ambayo tunataka kuongeza nguvu huyo tutamsajili.
Alisema suala la sita sera inataka kila kwenye usajili ambao timu utakuwa unafanya lazima kuwa mtu mwenye sauti ya mwisho mwenye kuamua mchezaji mpya wa kusajiliwa kulingana na nafasi ambayo tunahitaji na vile vigezo ambavyo vimewekwa.
“Hapa kwenye maamuzi ya mwisho ndiyo tunaweza kuongezeka nafasi nyingine kwani Bodi ya Wakurugenzi ndiyo itakuwa na maamuzi ya mwisho kulingana na ripoti ya mwalimu kulingana na wachezaji wapya ambao atakuwa anawahitaji,” alisema.
“Sera hiyo mpya inaonesha pia kama si Bodi ya Wakurugenzi basi benchi la ufundi linaweza kuwa na maamuzi na kauli ya mwisho katika usajili bila kuingiliwa kama alivyokuwa akifanya Arsene Wenger pale Arsenal, vilevile sera itatuwezesha kuchagua njia ya viongozi ndio kuwa wenye kauli ya mwisho.
“Jambo la mwisho sera mpya inaonesha tunaweza kuunda kamati maalumu ambayo watachanganyika watu mbalimbali kufanya usajili ambao wao ndio watakuwa wenye kauli ya mwisho baada ya kocha kutoa mapendekezo yake, au tunaweza kuunda kamati maalumu iliyokuwa na makocha wazoefu nchi na nje ya nchi akiwepo na kocha wetu hao ndio watakuwa kila kitu katika usajili.”