Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

#WC2018: Tuache kumfuatilia Mbappe turudi kwa Adam Salamba?

Muktasari:

  • Kombe la Dunia linafanyika mara moja kila baada ya miaka minne. Dunia huwa inasubiri kwa hamu. Kila kampuni huwa inafikiria namna ya kunufaika na Kombe la Dunia. Mtu mmoja au wawili wanajaribu kuchomeka kalenda ya Kagame katika michuano hii.

VITA ya Daud na Goliath. Najaribu kufikiria namna aliyeipanga Michuano ya Kagame ifanyike wakati wa Kombe la Dunia. Alikuwa anafikiria nini? Alikuwa anafikiria kuanzisha vita ya Daud na Goliath. Vita ya Mike Tyson aliye katika ubora wake dhidi ya Francis Cheka.

Kombe la Dunia linafanyika mara moja kila baada ya miaka minne. Dunia huwa inasubiri kwa hamu. Kila kampuni huwa inafikiria namna ya kunufaika na Kombe la Dunia. Mtu mmoja au wawili wanajaribu kuchomeka kalenda ya Kagame katika michuano hii.

Michuano yote duniani imesimama kwa sasa kupisha Kombe la Dunia. Dakika chache kabla ya pambano la Argentina na Ufaransa lililokuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani kote, Tanzania ikiwemo, Simba ilikuwa inasubiri kucheza na timu dhaifu kutoka Somalia.

Hakuna michuano yoyote ya klabu katika Kanda za Afrika Magharibi, Afrika ya Kati, Afrika Kaskazini na kwingineko ambapo kuna michuano kama hii inaendelea. Si Afrika tu, bali duniani kwa jumla. Kama kuna watu wachache wamesikia kuwa Tanzania kuna michuano ya namna hii, basi wanaangua vicheko.

Hata wachezaji wa Simba na wale wa Somalia walikuwa wanasubiri kwa hamu kutazama mechi ya Argentina na Ufaransa. Ni michuano ya aina gani hii Kagame? Imeanza wakati dunia ikisubiri mechi tamu za mtoano za Kombe la Dunia.

Michuano ya aina hii ni dhaifu kihisia na kibiashara. Kwa mfano, soka ni mchezo wa hisia na kishabiki. Unawezaje kutawala na mazungumzo ya Simba kuishinda timu ya Somalia wakati jioni yake Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakitolewa katika fainali za Kombe la Dunia?

Kibiashara, kwa mfano, unawezaje kuzishawishi kampuni kuwekeza katika michuano hii wakati wa Kombe la Dunia? Kampuni zitanufaika na nini? Macho ya wafuatiliaji wengi wa soka kwa sasa yanapitia katika biadhaa ambazo zipo katika matangazo ya televisheni zinazoonyesha Kombe la Dunia. Unamshawishi vipi mtu kuweka pesa zake katika matangazo ya Kagame.

Ukiona watu wanaingiza michuano ya Kagame katika hatua hii ya Kombe la Dunia ndipo unagundua kwanini michuano imepoteza umaarufu wake. Mikakati ni duni na tunaishi kwa mazoea. Hasa kwa yule bosi ambaye anaamini kwamba ukipeleka Kagame Tanzania, basi Simba na Yanga zina mashabiki wengi na watafuatilia.

Lakini hapohapo ndio utagundua kwamba mabosi wa soka wa ukanda huu hawaoni aibu kwanini timu zetu za taifa hazishiriki Kombe la Dunia. Ingekuwa vipi kama Uganda na Kenya zingeshiriki fainali za Kombe la Dunia? Kuleta ratiba hii katika nyakati hizi ni ishara ya kujivunia kwamba hatuhusiki na Kombe la Dunia.

Lakini pia kumbe wachezaji wa ukanda huu pia hawahusiki na Kombe la Dunia. Ingekuwa vipi kama Gor Mahia, Simba, Azam na timu nyingineo zingekuwa zina wachezaji wanaoshiriki Kombe la Dunia. Michuano ingesonga mbele?

Ukosefu huu huu wa mikakati na ubunifu ndio ambao kwa kiasi kikubwa umepunguza umaarufu wa michuano yenyewe. Hii inamaanisha kuwa hata katika nyakati ambazo sio kama hizi za Kombe la Dunia, bado michuano hii imepoteza umaarufu. Ndipo unapogundua kwanini tangu mwaka 2002 zawadi ya Dola 30,000 kwa bingwa wa michuano imebakia palepale. Hakuna watu wa kututoa katika zawadi na hizi na kutupeleka mbele zaidi.

Labda tunahitaji kubadili Katibu Mkuu wa Cecafa ili aje mwingine ambaye ana mawazo mapya. Labda tunahitaji kubadili muundo wa Cecafa na kwenda katika mawazo mapya. Tukibaki hapa tulipo tutaendelea kukwama.

Haiwezekani katika hali ya kawaida kabisa tukaondoa ushabiki katika mambo anayofanya Kylian Mbappe kwa ajili ya kurudisha akili zetu kwa Adam Salamba. Sawa, tunapaswa kupenda vitu vya nyumbani lakini tukumbuke kuwa Kombe la Dunia ni kilele cha mchezo unaopendwa zaidi na sisi pamoja na mashabiki wote duniani.

Wanaoshiriki na wasioshiriki wote wanaelekeza macho yao katika Kombe la Dunia, iweje sisi tukachomekea Kagame Cup wakati Kombe la Dunia likiendelea? Inashangaza sana na tunaonekena watu wa ajabu. Mbona michuano ya Ligi Mabingwa ya Afrika pamoja na ile ya Kombela Shirikisho imesimama? Wanaondaa wana akili timamu. Wamepisha kitu kizito.