Viwanja virekebishwe na wachezaji wapumzike
Muktasari:
- Mambo yakienda kama ilivyopangwa, Ligi Kuu itarejea Januari mara baada ya kufikia tamati kwa Fainali za AFCON lakini mambo yanaweza kwenda tofauti na ligi yetu ikarejea kabla ya kumalizika kwa AFCON.
KWA sasa Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa muda kupisha mechi za Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 ambazo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itashiriki.
Mambo yakienda kama ilivyopangwa, Ligi Kuu itarejea Januari mara baada ya kufikia tamati kwa Fainali za AFCON lakini mambo yanaweza kwenda tofauti na ligi yetu ikarejea kabla ya kumalizika kwa AFCON.
Wakati huu ambao Ligi Kuu yetu imesimama, kijiwe kingependa kushauri mambo mawili ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi katika muda huu ambao ligi haichezwi.
Kwanza ni maboresho ya viwanja kadhaa vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu hasa katika maeneo ya kuchezea yakidhi hadhi na thamani ya ligi na timu shiriki.
Kuwa na viwanja visivyo na maeneo mazuri ya kuchezea siyo sifa nzuri kwetu Tanzania ambako leo hii tunajivunia kuwa na miongoni kati ya ligi tano bora barani Afrika, pia tunajitambulisha kama nchi ya kimpira.
Kijiwe kinaamini muda huu wa mapumziko unatosha kutumika vyema na wamiliki wa viwanja, klabu na wadau wengine wa mpira wa miguu kuboresha viwanja vyetu ili viwe na hadhi inayoendana na ukubwa wa nchi na ligi yetu kimataifa.
Eneo la kuchezea katika baadhi ya viwanja lina changamoto ya ukavu na nyasi kutostawi vizuri hivyo kuweka mbolea na maji ya kutosha kutasaidia kupunguza tatizo na pengine kuliondoa kabisa.
Lakini wachezaji ambao hawajapata fursa ya kwenda katika Fainali za AFCON, wanatakiwa kutumia vyema mapumziko haya kwa kutojihusisha na mitindo mibaya ya maisha ambayo itaathiri viwango vyao ligi ikirejea.
Mapumziko mazuri katika kipindi hiki yatawasaidia kuifanya miili iimarike vyema na hivyo pale msimu utakapoendelea, warudi uwanjani wakiwa katika hali nzuri.