Vaibu la Simbu akipokewa kishujaa Dar
Muktasari:
- Lakini lile vaibu la ukaribisho wake hapa nchini liliteka hisia za wengi wakiwamo abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JKNIA), alfajiri ya kuamkia jana.
MWANARIADHA Alphonce Simbu yupo nchini akitokea Japan alikoshinda medali ya dhahabu katika riadha.
Lakini lile vaibu la ukaribisho wake hapa nchini liliteka hisia za wengi wakiwamo abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JKNIA), alfajiri ya kuamkia jana.
Simbu ambaye ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda mbio za marathon zilizofanyika Tokyo, Japan, wiki iliyopita alipokewa kwa shamrashamra na mamia ya Watazania ikiwemo familia yake.
Kabla ya ndege aliyopanda kutua majira ya saa nane usiku, mapema mabasi kadhaa makubwa ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliwasili uwanjani hapo huku vikundi mbalimbali vya ngoma vikisubiri ujio wake.
Kuonyesha kwamba lilikuwa ni vaibu la aina yake, abiria mbalimbali ambao waliokuwa na ratiba za kusafiri waliokuwapo katika eneo hilo hususan wale wa mataifa ya kigeni walionekana kuulizia nini kinaendelea, na hata walipojibiwa bado kila mmoja alitamani kumuona mwamba huyo akiinyaga ardhi ya Tanzania.
Baada ya saa tatu za hekaheka uwanjani hapo hatimaye Simbu aliwasili na kupokewa na mamia ya watu wakiwemo maofisa mbalimbali wa jeshi, na Mwanaspoti lililokuwapo lilibahatika kufanya naye mahojiano mafupi kabla hajaondoka akisindikizwa na wananchi.
“Nimefurahi kwa sababu Watanzania wengi wamejitokeza kwa ajili ya mapokezi haya. Niseme kuwa medali hii ni kwa ajili ya Watanzania wote. Hii ni hatua kubwa na furaha kwetu sote. Ushindi huu unadhihirisha kwamba mchezaji yeyote wa Kitanzania anaweza kufanya lolote katika mashindano yoyote ya kimataifa,” alisema.
Aliongeza kuwa ushindi wake unapaswa kuwa chachu kwa wanariadha na wachezaji wa michezo mingine nchini, akiwatia moyo wasikate tamaa.
“Kwa mchezo wa riadha hata mashindano yawe makubwa kwa kiasi gani ukitia juhudi na ukajiandaa unaweza kushinda. Sio rahisi, lakini kujituma kunasaidia sana. Niwasihi wachezaji wa Kitanzania kuamini kuwa wanaweza,” alisema.
Baada ya kutua na kutumia saa moja na nusu katika uwanja wa ndege, Simbu alipanda gari lililonakshiwa kwa picha zake na kwenda Hoteli ya Blue Sapphire iliyopo Vingunguti - umbali mfupi kutoka ilipo JKNIA
USHINDI BAB’KUBWA
Katika mashindano hayo yaliyofanyika Tokyo, Simbu alishinda kwa tofauti ndogo zaidi kwenye historia ya marathoni duniani akimshinda Mjerumani Amanol Petros kwa sekunde 0.03.
Simbu na Petros walimaliza kwa muda sawa wa saa 2:09:48, lakini teknolojia ya picha ilionyesha Mtanzania huyo ndiye aliyeingia wa kwanza kuingia mstari wa mwisho. Muitaliano Iliass Aouani alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:09:53.
Ushindi huo ulimpandisha chati Simbu kutoka kumiliki medali ya shaba aliyoshinda London, Uingereza 2017 hadi dhahabu, huku akitimiza ndoto aliyoiweka kwa zaidi ya miaka 10.
“Hii medali nimeitafuta kwa miaka 10. Mara ya kwanza nilishiriki mwaka 2015 China nikakosa, 2017 London nikapata shaba, nikaendelea kujaribu na kukosa, lakini sikukata tamaa. Niliapa kujaribu tena na tena. Hata Wakenya walishangaa kuona Mtanzania akishinda,” alisema Simbu.
SAFARI YA MAANDALIZI
Simbu anasema maandalizi yake yalihusisha mazoezi katika mazingira tofauti, ikiwemo kukimbia kwenye vilima ili kukabiliana na changamoto za kimbinu na hali ya hewa.
“Kabla ya Tokyo nilijifunza kutokana na changamoto za Paris (Ufaransa) mwaka jana. Nilifanya mazoezi kwenye nyuso tofauti na kwenye vilima, na hilo ndilo lililofanya tofauti Japan,” anasema.
Kwa sasa bingwa huyo anadai kwamba atakaa na kocha wake pamoja na viongozi wa timu kuangalia mwelekeo wa mashindano yajayo akisisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbeleni.
MKEWE AZUNGUMZA
Furaha ya ushindi wa Simbu katika mashindano ya dunia imeigusa kwa kiasi kikubwa familia, huku mkewe Rehema Daudi akisema safari ya mumewe haikuwa rahisi, kwani kwa muda mrefu alikuwa na kiu ya kutwaa medali hiyo na kama walikuwa wakimpa moyo kila mara.
“Nilimpa moyo kwa kumwambia nenda Mungu atafanya, na kweli Mungu ametenda,” anasema Rehema.
Anasema siri ya mafanikio ya Simbu imekuwa katika mazoezi yenye bidii, nidhamu na maombi na mara kwa mara amekuwa akimhimiza mumewe kujitahidi na kuwa mwaminifu katika maandalizi.
“Ujue ukifanya mazoezi na kumuomba Mungu yeye anafanya. Kiu yake zaidi ilikuwa ni kupata hii medali ambayo amepata sasa,” anasema.
KOCHA AFICHUA JAMBO
Kocha wake kutoka JWTZ, Anthony Mwingereza amezungumzia siri ya maandalizi ya Simbu yaliyomfikisha kwenye hatua hiyo.
Mwingereza ambaye ndiye kocha mkuu wa timu ya riadha ya JWTZ anasema Simbu amekuwa akifanya mazoezi katika kambi ya kikosi cha 977 na yanakuwa ya kina ndiyo maana yamezaa matunda makubwa.
“Kwanza nina furaha mchezaji amefanya vizuri na amewatoa kimasomaso Watanzania. Tangu riadha ianze kushiriki mashindano makubwa kuanzia mwaka 1954 haijawahi kutokea Mtanzania kushinda medali hii,” anasema Mwingereza.
Anasema medali zilizowahi kupatikana awali zilikuwa kupitia Filbert Bayi katika mashindano ya Jumuiya ya Madola, lakini kiwango cha dunia kilikuwa hakijafikiwa na Mtanzania yeyote.
“Kubwa kama hii ni ya kwanza kwa Tanzania, na hii ni kwa sababu mchezaji ameandaliwa kwa kina na makocha chini ya ulezi wa kikosi 977 ambako ndipo kambi ilipo. Haya ndiyo yametuletea matunda mazuri,” anasema kocha huyo.
Kwa mujibu wa Mwingereza, maandalizi hayo yamehusisha nidhamu ya kijeshi, umoja wa wachezaji na mpango maalumu wa mazoezi uliolenga kumwandaa Simbu kukabiliana na changamoto za mashindano makubwa ya kimataifa. Kwa matokeo hayo, Tanzania imeandika ukurasa mpya katika historia ya michezo.
KWA VIONGOZI
Simbu aliwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwapa hamasa wanamichezo, na pia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda kumpa muda wa kufanya maandalizi akiwa askari wa jeshi hilo.
“CDF amekuwa akitupatia muda wa kutosha kwa ajili ya kufanya mazoezi. Namshukuru pia kocha na wachezaji wenzangu kwa mshikamano tuliokuwa nao.”