Uhondo wa ngumi na mambo kumi ya kuvutia

Muktasari:
- Sikia, mchezo huo ulianza miaka mingi sana. Masumbwi ni mchezo maarufu zaidi kati ya michezo yote ya mapambano duniani.
KWA nini unashangaa sasa kuona kuna mchezo wa ngumi? Kwa nini watu wapigane wakati hawajakosana? Inakuwaje ngumi zinapigwa na watu kutoana damu, ngeu au hata kusababisha vifo? Umeshawahi kujiuliza ilikuwaje mchezo wa ngumi za kubondana bila kukasirishana, lakini mkaishia kusababishiana maumivu ya mwili.
Sikia, mchezo huo ulianza miaka mingi sana. Masumbwi ni mchezo maarufu zaidi kati ya michezo yote ya mapambano duniani.
Nyota wengi kama Muhammad Ali walipata umaarufu kupitia masumbwi, hali iliyogusa maisha ya watu hata nje ya ulingo. Wakati mabingwa walivuma kuna mapambano ya kusisimua yamepata umaarufu mkubwa duniani, lakini pia kuna mambo mengi ya kushangaza ambayo hayajulikani sana na hufanya mchezo huo kuvutia zaidi. Hapa kuna mambo 10 ya kushangaza kuhusu mchezo huo ambayo si vibaya ukayajua.
1. MIAKA 5000 ILIYOPITA
Je unajua kwamba masumbwi yalianza zaidi ya miaka 5,000 iliyopita? Watu wengi wanaona masumbwi kama mchezo wa kisasa, lakini kwa hakika ulianza zamani sana. Picha za kwanza za masumbwi zipo kwenye michoro ya kale ya takriban miaka 5,000 huko Mesopotamia kwenye bonde la mito Tigris na Euphrates iliyopo kati ya Irak na Syria. Wagiriki waliingiza masumbwi kwenye michezo yao ya Olimpiki mwaka 688 KK. Wakati huo, mabondia hawakuwa wakivaa glovu kama ilivyo sasa - walikuwa wakifunga mikono kwa ngozi za wanyama. Hii ilimaanisha mapambano makali bila kinga yoyote.

2. NGUMI ZILIANZA MAPAMBANO YA KIKATILI
Ni jambo la kushangaza kwamba glovu za masumbwi hazikuanzishwa kama kinga. Katika Roma ya Kale, mabondia walivaa glovu zilizojulikana kama cestus ambazo zilikuwa na misumari. Ngumi moja ingeweza kumuua mtu. Magwiji wa ulingoni walipigana vikali hadi kufa. Leo hii, matumizi ya glovu yamebadilika kabisa; husaidia kulinda wapinzani na mikono ya mabondia dhidi ya majeraha makubwa. Lakini, kwa mujibu wa ripoti ya British Medical Association, glovu hazipunguzi majeraha ya ubongo na huenda hata zinazidisha. Kwa sasa, kampuni za vifaa vya masumbwi zinatengeneza glovu za kisasa zenye ubora wa hali ya juu ili kuboresha mchezo huo.
3. KUNA LUGHA MAALUMU
Masumbwi yana lugha yake yenye maneno ambayo huwachanganya wanaoanza. Maneno kama southpaw na orthodox yanaelezea mitindo tofauti ya kusimama ulingoni. Southpaw ni bondia anayepigania kwa mkono wa kushoto mbele, huku orthodox ni bondia wa mkono wa kulia. Pia kuna msemo maarufu wa throwing in the towel (kutupa taulo), ambao umetokana na masumbwi. Timu ya bondia ikiona amechoka au ameumia vibaya hutupa taulo ulingoni kuashiria kusimamisha pambano.
4. SHERIA ZILIVYOBADILI
Mwaka 1867, Sheria za Marquess of Queensberry ziliweka msingi wa masumbwi ya kisasa zinazotumika kwenye mapambano ya ngumi za kulipwa na ridhaa. Kabla ya hapo, ngumi zilipigwa mikono wazi chini ya Sheria za London Prize ambapo zingedumu kwa saa nyingi, hata kama mabondia walikuwa wamejeruhiana. Hata hivyo sheria mpya ziliweka madaraja ya uzito, raundi za dakika tatu na kuanzisha matumizi ya glovu. Pia zilikataza mieleka na kufanya masumbwi kuwa mchezo wa kusimama na kupigana ngumi. Sheria hizo zilitungwa na mwanamichezo wa Wales, John Graham Chambers.

5. NGUMI JIWE
Je unajua kwamba ngumi ya bondia inaweza kuwa na nguvu kuliko mkwaju wa fimbo ya mpira wa magongo? Mabondia wanaofanya mazoezi haswa ya kupigana hupiga ngumi kali sana. Utafiti mojawapo unasema bondia wa uzito wa juu anaweza kupiga kwa nguvu ya inayoweza kutikisa ukuta wa mawe. Ndiyo maana mabondia wa viwango vya juu duniani hujifua vikali ili kujiandaa na mapigano ya nguvu.
6. OLIMPIKI BILA MADARAJA
Mchezo wa ngumu uliwahi kuwa katika Olimpiki bila madaraja ya uzito. Inaelezwa kwamba masumbwi yalipoanzishwa kwa mara ya kwanza kwenye Michezo ya Olimpiki ya kisasa 1904 hakukuwa na madaraja ya uzito. Hali hiyo ilisababisha mabondia wa uzito mdogo kupambana na wa uzito mkubwa - jambo ambalo kwa sasa linachukuliwa kama siyo haki. Baadaye madaraja ya uzito yaliwekwa ili kuimarisha usalama na usawa kwa kupiganishwa mabondia wa ukubwa na uzito unaolingana. Mwaka 2021, michuano ya wanawake ya masumbwi ilianzishwa kwenye Olimpiki, ikiwa ni hatua kubwa kwenye usawa wa kijinsia.

7. SUGAR RAY ROBINSON
Umewahi kulisikia jina hilo? Sugar Ray Robinson anafahamika kama mfalme wa pound for pound. Ingawa Muhammad Ali alipata umaarufu mkubwa katika ulingo, lakini wataalamu na wabobezi wengi wa mchezo wa ngumi wanaamini Sugar Ray Robinson ndiye bondia bora wa pound for pound wa muda wote. Bondia huyo alipigana miaka ya 1940 na 1950, na kuwa na rekodi ya ushindi mara 174, kupoteza 19, sare 6 na ushindi wa KO mara 69. Neno pound for pound lilianzishwa ili kumwelezea kwa sababu uwezo wake na nguvu vilikuwa vya kipekee bila kujali uzito wake. Hata Muhammad Ali aliwahi kusema Robinson ndiye ‘MFALME.’

8. KNOCKOUT YA HARAKA
Mchezo wa ngumi una vitu vingi vya maajabu, lakini unajua kwamba kuna knockout ya haraka zaidi katika mchezo huo ukiachana na hizi unazozijua wewe? Sikia hii, kuna bondia mmoja miaka ya 1888 aliwahi kuguswa tu tena bila kipigo akaanguka na hakuamka tena - tukio lililokuwa la sekunde moja. Lakini unalijua sakata jingine la mtu aliyeitwa Ali-Liston? Moja ya matukio ya ajabu kwenye historia ya masumbwi ni pale Muhammad Ali alipomwangusha Sonny Liston 1965 kwa kile kilichoitwa ‘phantom punch’. Pambano hilo lilimalizika kwa utata mkubwa wengine wakidai Liston alijilaza, huku miongoni mwao wakiwamo waliosema kasi ya Ali ilifanya ngumi ionekane hafifu kuliko ilivyokuwa. Hii ni moja ya knockout za haraka zaidi kwenye historia ya mapambano ya ubingwa wa dunia wa uzito wa juu.
9. PAMBANO REFU
Maajabu ya ngumi bwana! Pambano refu zaidi la masumbwi lilidumu kwa zaidi ya saa saba. Pambano hilo lilifanyika Aprili 6, 1893 kati ya Andy Bowen na Jack Burke, ambapo lilikuwa la raundi 110 zilizopigwa kwa zaidi ya saa saba. Wakati huo hapakuwa na kikomo cha raundi, hivyo walipigana hadi mmoja ashindwe kuendelea. Hakuna aliyemwangusha mwenzake, na hivyo pambano liliisha kwa sare baada ya wote kuchoka na kushindwa kuendelea.
10. WANAWAKE KITAMBO SANA
Masumbwi ya wanawake yana historia ndefu isiyotambulika. Masumbwi ya kinamama licha ya kuwa na historia ndefu, lakini hayakutambulika sana miaka ileee - ya kweusi. Pambano la kwanza la wanawake lilirekodiwa London, Uingereza 1722 kati ya Elizabeth Wilkinson na Hannah Hyfield. Ingawa wanawake wamepitia changamoto nyingi kutambulika kwenye mchezo huo, lakini rasmi masumbwi ya wanawake yaliingizwa kwenye Michezo ya Olimpiki 2012. Nyota kama Katie Taylor na Claressa Shields walifungua njia kwa wanawake kwenye mchezo huo.
Kwa Kumalizia. Masumbwi yamejaa mambo mengi ya kuvutia. Historia yake inaonyesha jinsi mchezo huuo ulivyobadilika kutoka enzi za kale hadi kuanzishwa kwa sheria za kuokoa maisha. Mabondia wengi mashuhuri wameibuka kwenye mchezo huo, na historia imejaa matukio ikiwamo kuanzishwa kwa masumbwi kwa wanawake kwenye Olimpiki.

FAHAMU ZAIDI
Mchezo wa ngumi una rekodi moja ya maisha ya kazi kukiwa na takwimu nne. Ukifuatilia masumbwi ya kisasa utaona rekodi za mabondia zikitajwa kwa mfululizo wa namba nne kama vile 26-12-1-1, lakini hii inamaanisha nini? Kila namba ina maana yake. Mpangilio huwa uleule - ushindi, kushindwa, sare, mapambano yaliyofutwa.
BUM NI NINI?
Katika ulimwengu wa masumbwi, BUM sio kile unachokifikiria. BUM inamaanisha ‘Below Usable Measure’ (chini ya kiwango kinachokubalika). Hivyo, kama utaitwa BUM kama bondia, inamaanisha umepigana mapambano yasiyozidi 12 au umepoteza asilimia 25 au zaidi ya mapambano yako ya kitaaluma. Kama unavyoweza kudhani kuitwa BUM siyo jambo la kujivunia katika mchezo wa masumbwi.
KONA YA KO AU CHINA-CHINNED
Bondia anayeitwa ‘china-chinned’ ni yule aliyepoteza asilimia 10 au zaidi ya mapambano yake kwa kupigwa knockout (KO). Ingawa utambulisho huo ni wa zamani na si sahihi sana siku hizi, bado unatumika kwenye ulimwengu wa masumbwi. Katika hali halisi, bondia anayepigwa KO hupata majeraha ya aina mbalimbali ambayo sio lazima yahusishe taya.
MADARAJA YA UZITO KIBAO
Kama msemo katika masumbwi usemavyo ‘pigana na mtu wa saizi’ uzito wako. Katika masumbwi, hilo limepewa uzito mkubwa kwa kuweka madaraja 17 ya uzito. Kama bondia wa mashindano, huruhusiwi kupambana na bondia nje ya daraja lako la uzito. Kuanzia Super Brainweight wa uzito wa kilo 47.6 hadi Heavyweight wa uzito wa kilo 90.7 na zaidi - kuna daraja la uzito kwa kila mtu mwenye ndoto ya kuingia ulingoni.